Tuesday, 4 July 2017

Hawa ndio waliosamehewa kulipa kodi ya majengo

ULIPAJI wa kodi ya majengo, umeonekana kutengeneza mjadala miongoni mwa wadau wakiwamo wanasiasa, ambao walikaririwa hivi karibuni wakilalamika kuwa katika baadhi ya maeneo, wamekuwa wakitozwa kinyume na sheria.


Miongoni mwa viongozi waliokaririwa ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto. Akizungumza hivi karibuni kwenye kikao cha baraza la biashara la Mkoa wa Kigoma, Zitto alipigia kelele viwango vya kodi vinavyotozwa akisema ni tofauti na tangazo la serikali lililotolewa na kutangazwa kwenye gazeti la serikali.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ndiyo yenye mamlaka ya kukusanya kodi ya majengo; kazi ambayo ilianza kuitekeleza katika majiji, manispaa na miji kama ilivyoainishwa na Gazeti la Serikali namba 276, Septemba 30. Kwa sasa inaendelea kukusanya kodi kwenye majiji manne, manispaa 18 na miji saba hatua inayotokana na mabadiliko ya sheria tatu zilizo chini ya Sheria za Fedha ya mwaka 2016.
Kodi hukusanywa kwa kutumia taarifa za walipa kodi zilizokabidhiwa kutoka kwa serikali za mitaa. Awali, kodi hizi zilikusanywa na serikali za mitaa, lakini kuanzia Julai mwaka jana, mamlaka ndiyo imepewa kutathimini, kukadiria na kukusanya kodi za majengo. “TRA inasimamia ukusanyaji huo wa kodi ya majengo huku ikiwa inakiuka sheria ya ukusanyaji iliyotolewa kwenye tangazo hilo,” alikaririwa Zitto.
Diwani wa kata ya Kigoma Mjini, Hussein Kalyango anamuunga Zitto mkono akisema, awali wakati ukusanyaji ukifanywa na halmashauri, kodi hiyo ilikuwa ikitozwa kwa pamoja kwa majengo yote yaliyopo kwenye kiwanja kimoja lakini kwa sasa kila jengo kwenye kiwanja hicho hicho linatozwa bei yake.
Kalyango anasema, kulingana na TRA inavyosimamia ukusanyaji huo kwa sasa, kila jengo linatozwa kwa bei yake kwa viwango tofauti na hivyo mwenye nyumba anaweza kujikuta akilazimika kulipa kati ya Sh 100,000 hadi Sh 300,000.
Hata hivyo, katika kikao hicho cha baraza la biashara, Kaimu Meneja wa TRA mkoa Kigoma, Adiel Mero anasema mamlaka inakusanya mapato hayo kulingana na sheria iliyoagiza kufanyika kwa jambo hilo na inawatumia wathamini waliokuwa wakifanya uthamini kwenye halmashauri.
TRA inasemaje? Katika mahojiano kati ya gazeti hili na Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi, Richard Kayombo, anayo majibu juu ya malalamiko haya na taarifa nyingine muhimu kwa umma huku akisisitiza kuwa TRA imepewa kisheria mamlaka ya kukusanya kodi hiyo.
Anasema: Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imepewa jukumu la kusimamia na kukusanya kodi ya Majengo kuanzia Julai 1, 2016 kwa mujibu wa mabadiliko ya Sheria ya Kodi ya Majengo Na. 2 Sura ya 289, Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa Na. 9 Sura ya 290 na Sheria ya Mamlaka ya Mapato Tanzania Na. 9 Sura ya 399. Hii imeainishwa kwenye Sheria ya Fedha ya mwaka 2016.
Nini maana ya Kodi ya Majengo? Kodi ya majengo ni tozo kwa mujibu wa sheria kwenye majengo au nyumba ambazo zimekamilika, zinakaliwa (watu wanaishi) na kumilikwa kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi na sheria nyingine za nchini.
Majengo husika yanapaswa yawe yamefanyiwa uthamini. Mamlaka ya Serikali za Mitaa zimepewa jukumu la kuchagua wathamini wa majengo ambao watatayarisha jedwali au orodha ya majengo/nyumba katika maeneo ya miji na manispaa na majiji.
TRA kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali za Mitaa wameajiri wathamini kwa kutayarisha orodha kwa ajili ya kutoza kodi hiyo ya majengo. Nani anapaswa kuwa mthamini? Mthamini wa Majengo anatakiwa awe amesajiliwa na sheria ya wathamini wa majengo kama mthamini. Awe Ofisa Mwajiriwa wa Mamlaka ya utozaji kodi ya majengo na awe ofisa wa serikali katika Idara ya Uthamini aliyeteuliwa na waziri husika.
Taarifa zinazohitajika wakati wa uthamini ni jina la mmiliki, anuani kamili, namba ya kiwanja/jengo. Wathamini watatakiwa kuonyeshwa hati ya kiwanja kwa maeneo yaliyopimwa au leseni ya makazi kwa maeneo ambayo hayajapimwa.
Pia ankara za maji au umeme huoneshwa kwa uthibitisho wa mmiliki wa jengo/nyumba. Wathamini huthibitisha mwaka ambao jengo limejengwa, michoro iliyotumika kwenye ujenzi.
Kwa upande wa majengo makubwa, inapaswa ielezwe matumizi yake iwapo ni makazi au biashara. Watapima eneo la jengo ili kupata ukubwa wake. Iwapo jengo ni la ghorofa, eneo la kila sakafu ya ghorofa litapimwa na kujumlishwa ili kupata eneo la sakafu zote. Wamiliki wa nyumba /majengo watatambuliwa kwa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN).
Maeneo yanayohusika TRA inakusanya kodi hii katika majiji ambayo ni Arusha, Tanga, Mbeya na Mwanza. Manispaa zinazohusika ni Kinondoni, Ilala, Temeke, Ubungo, Kigamboni, Dodoma, Kigoma Ujiji, Ilemela, Mtwara Mikindani, Morogoro, Tabora, Moshi, Shinyanga Musoma, Singida, Sumbawanga Iringa, Bukoba, Songea na Lindi.
Kwa upande wa miji ambayo wakazi wake wanawajibika kisheria kulipa kodi ya majengo ni Bariadi, Geita, Kibaha, Njombe, Korogwe, Mpanda, Kahama na Babati.
Mamlaka imetengeneza mfumo wa kukusanyia kodi huu ambao una uwezo wa kuandaa na kutoa hati ya madai ya kodi ya majengo na hivyo kumwezesha mteja kulipia katika benki yoyote ya kibiashara.
Mfumo wa benki umeunganishwa na mfumo wa malipo ya kodi. Hivyo mlipakodi akishalipa benki, taarifa zote zinaingia katika mifumo ya TRA na kufuta deni la mlipakodi husika.
Viwango vya kodi ya majengo Tozo za kodi ya majengo vinatofautiana kutokana na sheria ndogo zilizotungwa na mamlaka za serikali za mitaa husika hali inayofanya kuwapo viwango tofauti kulingana na eneo husika.
“Maeneo ndani ya jiji moja tozo zinatofautiana vivyo hivyo tozo ndani ya manispaa moja na mji mmoja zinatofautiana. Kodi zote katika maeneo husika zitatolewa kwa hati ya madai itakayotolewa na ofisi ya TRA eneo husika,” anasema Kayombo.
Taarifa ya TRA kuhusu viwango, inaonesha mfano wa manispaa za Dar es Salaam, zimeidhinisha kiwango cha kodi ya majengo ni Sh 15,000. Aidha, kodi hii hutozwa mara moja tu kwa mwaka. Mwaka wa serikali unaanza Julai ya kila mwaka na kuishia Juni ya kila mwaka.
Hivyo basi kodi ya mwaka wa Serikali 2016/17 mwisho wake wa kulipa ni Juni 30. Baada ya tarehe hiyo kupita, kodi zote za majengo zitalipwa na riba na adhabu kwa mujibu wa sheria, ikiwa ni pamoja na taratibu za kisheria zitatumika kukusanya kodi hiyo. Inaruhusiwa kufanya pingamizi kwa mamlaka za utozaji kodi ya majengo zilizowekwa kisheria katika eneo husika.
Pingamizi linaweza kufanywa na mmiliki au mwakilishi aliyechaguliwa kisheria na mwenye nyumba/jengo. Wenye msamaha Wenye msamaha wa kulipa kodi ya majengo ni nyumba kwa matumizi ya Rais, majengo yanayomilikiwa na kutumiwa na serikali kwa matumizi ya umma; majengo yanayomilikiwa na taasisi za dini ambayo hayatumiki kwa shughuli za biashara au kiuchumi kwa kujipatia faida.
Majengo mengine yenye msamaha wa kulipa kodi ni maktaba za umma na majengo ya makumbusho; makaburi na nyumba za kuteketeza maiti; majengo ya kuongozea ndege ya umma na majeshi isipokuwa majengo mengine yenye shughuli tofauti na hizo.
Kayombo anataja pia majengo yenye maeneo ya viwanja vya michezo vinavyotumika kwa matumizi ya taasisi za elimu; majengo ya shughuli za reli; yanayomilikiwa na asasi zisizo za kiserikali yasiyotumika kwa shughuli za biashara au kujipatia faida/kipato; yanayomilikiwa na serikali, taasisi za serikali na taasisi nyingine za aina hiyo yasiyotumika kwa shughuli za biashara au kujipatia kipato/faida.
Pia nyumba/majengo yanayomilikiwa na serikali za mitaa na taasisi zake ambazo hazitumiki kwa shughuli za biashara au kujipatia kipato/faida. Mtu mwenye umri wa zaidi ya miaka 60 au mwenye ulemavu asiye na kipato, pia wamepewa msamaha wa kodi ya majengo kwa nyumba moja ambayo ingepaswa kulipiwa.
Lakini pia, waziri mwenye dhamana amepewa mamlaka ya kuamua majengo yoyote na kutoa tangazo kwenye gazeti la serikali. Kayombo anasema mikakati ya TRA katika kuboresha ukusanyaji wa kodi ya majengo ni kufanya uthamini wa majengo ili kuwa na viwango ambavyo ni rafiki.
Mamlaka inasema pia itaimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa shughuli za ukusanyaji wa kodi ya majengo; Kutoa elimu kwa jamii kuhusu ulipaji wa kodi ya majengo; Kuhakikisha inashughulikia pingamizi za kodi ya majengo katika muda muafaka na kuboresha daftari jedwali/orodha ya uthamini ili kuwa na takwimu sahihi

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!