MKUU mpya wa Mkoa wa Kilimanajaro, Anna Mghwira, amemhakikisha Rais John Magufuli na Watanzania kwa jumla kuwa katu yeye sio mpinzani katika masuala yanayohusu maendeleo na maslahi ya taifa.
Aliyasema hayo jana Ikulu katika hafla ya kuapa mbele ya Rais Magufuli kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro baada ya Rais kumteua hivi karibuni kuziba nafasi ya Said Meck Sadick aliyemwomba Rais kujiuzulu akisisitiza kuwa, changamoto za kiafya alizo nazo hazitamwezesha kuendana na kasi ya maendeleo katika Serikali ya Awamu ya Tano.
Mghwira alisema anavyofahamu yeye ni kwamba, kazi za mkuu wa mkoa ni kusimamia shughuli za maendeleo kwenye mkoa na akaongeza kuwa, hakuna chama kinachopinga maendeleo ya kila eneo la nchi na nje ya mipaka ya nchi.
“Nimesema hii ni heshima kwa taifa letu, ni heshima kwa umoja wa nchi yetu, na ni heshima kwa siasa za umoja wa nchi yetu… Kumekuwa na minong’ono mingi sana kuwa Rais analeta nini; kuteua watu wanaoitwa wapinzani, mimi sio mpinzani wa maendeleo,” alisema Mghwira.
Katika hafla hiyo, Rais Magufuli alimtaka aende akachape kazi ili kuwaondolea kero wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro, licha ya kuwapo baadhi ya watu watakaomsema na kumbeza kwa kumwonea wivu.
Rais alisema alimchunguza Mghwira na kujiridhisha kuwa ana uwezo wa kuwatumikia wananchi wote bila tatizo. Alisema ingawa wapo wanasiasa wengi kutoka vyama vya upinzani wanaomwomba awateue kwenye nyadhifa mbalimbali serikalini, amekuwa akiwakatalia kwa vile anataka upinzani uendelee kuwepo nchini.
Katika hafla hiyo, Rais Magufuli alisema hawezi kuteua watu wanaosema sema ovyo, bali anateua mtu anayejua na kuamini kwa dhati kuwa, akimpeleka sehemu atafanya kazi kwa niaba ya Watanzania wote.
Alisema anajua kitendo cha kumteua Mghwira katika wadhifa huo kitazua maneno mengi kutoka kwa wana CCM na wanachama wa vyama vya upinzani kutokana na sababu mbalimbali hasi ukiwamo wivu, lakini akamtia moyo kuwa astahimili yote kwa kuwa hawezi kuepuka kusemwa.
Rais alisisitiza kuwa, yeye hateui watu wa hivi hivi, bali huwachunguza hadi kuridhika na uwezo na umakini alio nao mtu. “Kusemwa utasemwa tu, umeshaingia humu wengine watakuonea wivu, wapo watakaokuonea wivu wa kwenye chama chako, wapo wana CCM watakaokuonea wivu kwa sababu walitaka nichague tu kutoka CCM.”
“Wapo watakaokuonea wivu kutoka Chadema kwa sababu sikuchagua kutoka huko, pamoja na kwamba wako wengi wanaoniombaomba; mpaka wabunge, lakini nimesema hapana, nataka upinzani uwepo,” alisema Rais Magufuli.
Akaongeza, “Wapo watu kila kitu ni kupinga tu, mimi siteui watu wanaopiga piga kelele, nateua mtu ambaye najua nikimpeleka mahali atafanya kazi kwa niaba ya Watanzania, nenda ukafanye kazi, katumikie Watanzania, kamtangulize Mungu, kafanye kazi kwa niaba ya Watanzania,” alisema Mafuguli baada ya kumwapisha Mghwira.
Rais Magufuli alimtaka Mkuu wa Mkoa huyo mpya kwenda kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa ili kuondoa kero zinazowakabili wananchi wa Kilimanjaro, bila kujali itikadi za vyama vya siasa, dini, makabila na kanda wanazotoka.
Alimhakikishia ushirikiano wa kutosha wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yake na akamtaka asikubali kuyumbishwa na mtu yeyote katika kuwahudumia wananchi. Mghwira aliyeapishwa jana ndiye Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha ACT-Wazalendo na anakuwa mwanachama wa pili wa chama hicho kuteuliwa na Rais Magufuli kushika nyadhifa serikalini.
Alikuwa mmoja wa wagombea wa urais katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 kupitia ACT-Wazalendo, ikiwa ni mara ya kwanza kwa chama hicho kuingia katika kinyang’anyiro cha Uchaguzi Mkuu.
Mwanachama mwingine aliyeteuliwa kutoka ACT-Wazalendo ni Profesa Kitila Mkumbo ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji. Mwanasiasa huyo alilazimika kujiuzulu uanachama wa chama hicho ili akatumikie wadhifa wake huo mpya.
Wakati huo huo, Kamati ya uongozi ya Chama cha ACT-Wazalendo leo inakutana kwenye kikao kutafakari namna ambavyo Mghwira atatekeleza majukumu ya kichama na pia ya ukuu wa mkoa.
Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi wa Chama hicho, Ado Shaibu alisema kwa uteuzi huo ni wazi Rais Magufuli ameona viongozi wa upinzani wana uwezo wa kufanya kazi nzuri.
“Kwa kuzingatia unyeti na majukumu ya ukuu wa mkoa kamati ya uongozi ya chama itakutana kesho (leo) kutafakari pamoja na mambo mengine namna ambayo atatekeleza majukumu yake ya chama na majukumu mapya ya ukuu wa mkoa,” alisema Ado. Imeandaliwa na Shadrack Sagati na Regina Mpogolo
No comments:
Post a Comment