Wednesday, 7 June 2017

Pedeshee Ndama akiri tena kutakatisha fedha kiasi cha $540,000

Image may contain: one or more people

Mfanyabiashara 'Pedeshee Ndama' kwa mara nyingine tena amekiri kosa la kutakatisha fedha ambazo ni dola za Marekani 540,000.

Kabla ya kukiri kosa hilo Ndama aliomba akumbushwe mashitaka yake, Mahakama iliridhia ombi hilo na aliposomewa hati ya mashtaka 6, alikana mashtaka 5 na kukiri shtaka la 6 la kutakatisha fedha.




Awali, Mei 23 mwaka huu, Ndama alikiri kosa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilipanga kusikiliza maelezo ya awali Mei 29, lakini aliomba muda wa kujadiliana na mawakili wa utetezi hadi Mei, 30, mwaka huu alipokumbushwa mashtaka yake na kukana kutakatisha fedha hizo.


Hata hivyo, hali ilikuwa tofauti jana katika mahakama hiyo iliyoketi jana chini ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa, baada ya Ndama kuomba kukumbushwa mashtaka yake na aliposomewa, alikiri kwa mara nyingine kutakatisha fedha hizo.

Wakili wa Serikali, Esterzia Wilson, alimkumbusha Ndama mashitaka yanayomkabili baada ya wakili wa utetezi, Jeremiah Ntobesya, kuomba mteja wake kukumbushwa mashitaka hayo.

Mahakama iliridhia ombi hilo na aliposomewa hati ya mashtaka sita, alikana mashtaka matano na kukiri shtaka la sita la kutakatisha fedha.

Katika shitaka la kutakatisha fedha, Ndama anadaiwa kuwa kwa tarehe tofauti jijini Dar es Salaam, kati ya Februari 26 na Machi 31, 2014, akiwa mwenyekiti na mtiaji saini pekee wa kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Company Limited na akaunti ya benki ya kampuni hiyo iliyoko benki ya Stanbic, alijihusisha moja kwa moja katika uhamishaji fedha dola za Marekani 540,000.

Ilidaiwa kuwa alizitoa fedha hizo taslim huku akijua au alipaswa kujua kuwa fedha hizo ni za kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Hata hivyo, Ndama alikana mashitaka mengine ikiwamo la kudaiwa kuwa Februari 20,2014, akiwa jijini Dar es Salaam, alighushi nyaraka ya kibali cha kusafirisha madini na sampuli za madini kwa kusudi la kuonyesha kuwa kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Company Limited iliruhusiwa kusafirisha maboksi manne ya dhahabu ya kilogramu 207, yenye thamani ya Dola za Marekani 8,280,000 kwenda Australia kwa kampuni ya Trade TJL DTYL Limited wakati akijua si kweli.

Pia Ndama anadaiwa kuwa Machi 6, 2014, Dar es Salaam, alighushi kwa kutengeneza hati ya kibali cha Umoja wa Mataifa Ofisi ya Dar es Salaam, akijaribu kuonyesha kuwa kilogramu 207 za dhahabu kutoka nchini Congo zinazotarajiwa kusafirishwa na kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Company Limited kwenda Australia kwa kampuni ya Trade TJL PTYL Limited, zimesafirishwa bila jinai
yoyote wakati akijua ni kosa kisheria.

Aidha, anadaiwa kuwa Februari 20, 2014, alighushi fomu ya forodha yenye namba za usajili R.28092 akionyesha kampuni ya Muru imeilipa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) dola za Marekani 331,200 kama kodi ya uingizaji wa bidhaa ambazo zina uzito wa kilogramu 207 za dhahabu zenye thamani ya dola za Marekani 8,280,000 kutoka Congo.

Katika shitaka jingine, Ndama anadaiwa kuwa Februari 20, 2014, alighushi nyaraka ya bima kutoka Phoenix of Tanzania Assurance Company Ltd, akionyesha kampuni ya Muru imeyawekea bima makasha manne yaliyokuwa na dhahabu hizo.

Anadaiwa kuwa kati ya Februari 26 na Machi 3, 2014, akiwa Dar es Salaam, kwa njia ya udanganyifu alijipatia kutoka kwa kampuni ya nchini Australia ya Trade TJL DTYL Limited dola za Marekani 540,000 baada ya kudanganya atawapa na kusafirisha dhahabu hizo.

Awali, Ndama aliposomewa maelezo ya awali, baada ya kukiri kosa hilo, alikana maelezo mengi ya msingi yanayounda shitaka hilo.

Kutokana na hali hiyo, Hakimu Nongwa aliamuru kesi hiyo kuendelea kusikilizwa kwa kuwa nia ya Ndama ya kukiri kosa
ilikuwa na shaka.


Chanzo: Nipashe

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!