KIBAHA: Siku chache tangu kupita kwa Siku ya Mtoto wa Afrika, mwanafunzi wa darasa la tano, Abuu Hussein (11) wa Shule ya Msingi Miembe Saba wilayani Kibaha, mkoani Pwani ambaye ni yatima yamemkuta mazito kufuatia kusumbuliwa na vidonda mguuni.
Kutokana na hali hiyo, yuko hatarini kupata ulemavu endapo hatapata matibabu ya haraka.
Akizungumza na gazeti hili nyumbani kwa bibi yake huko Miembe Saba, mwanafunzi huyo alisema ana miezi mitatu ameshindwa kwenda shuleni kutokana na maumivu makali yanayomkabili yaliyosababishwa na vidonda.
Hussein ambaye ni yatima akiishi na bibi yake, Tatu Kiumbo (65) alipata tatizo hilo miezi mitatu iliyopita alipokuwa akicheza mpira na wenzake na kuanza kusikia maumivu kwenye mguu wake wa kulia.
“Yalianza maumivu mguuni na bibi alifikiri labda nimeumizwa na wenzangu, hali iliyomfanya anikande lakini maumivu yaliendelea kwa siku kadhaa na baadaye ilitokea kama kajipu, lakini kalikuwa kanauma sana,” alisema Hussein.
Aliendelea kusema kuwa bibi yake alimpeleka hospitali ambayo ni Kituo cha Afya cha Mkoani ambacho kwa sasa kimepandishwa hadhi na kuwa Hospitali ya Wilaya, alitibiwa na kuandikiwa dawa za kunywa pamoja na kupaka.
“Baada ya kupasuliwa siku chache baadaye vikatokea vidonda vingine vingi ambavyo vilikuwa vikitoa maji na mguu ukaanza kuvimba na kusababisha nishindwe hata kusimama,” alisema Hussein.
Bibi wa yatima huyo, Tatu alisema kuwa mjukuu wake kwa sasa haendi hospitali baada ya kuambiwa awe anatumia dawa kwa kunywa na kupaka baada ya kusafisha vidonda kila siku ambapo kwa sasa ana zaidi ya wiki tatu anatibiwa nyumbani.
Tatu alisema kuwa mjukuu wake amekuwa akipata maumivu makali usiku ambapo inambidi kumpa dawa za kutuliza maumivu.
“Kwa sasa wote tunauguzana kwani na mimi nashindwa kumhudumia vizuri, nami naumwa presha ambayo imenisababishia kushindwa hata kutembea huku muda mwingi nikiwa nimelala tu, naomba watu watusaidie maana hali yetu ni mbaya,” alisema Tatu.
Alisema kuwa hana msaada wowote kwani anaishi na watoto wa ndugu zake ambao nao hawana kazi ya aina yoyote, maisha yao yakitegemea misaada ya majirani.
Kwa upande wake mjomba wa mwanafunzi huyo, Idd Mikidadi ambaye amekuwa akimpeleka hospitali na kumrudisha, alisema angalau kwa sasa amepata nafuu kwani alikuwa hawezi hata kusimama na mguu ulikuwa ukitoa maji .
Mikidadi alisema kuwa kama kuna msaada wa kumsaidia mtoto huyo ili apate matibabu zaidi itakuwa ni vizuri kwani anateseka na kwa sasa hata masomo amesimama kutokana na tatizo hilo.
Akizungumzia tatizo hilo, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Miembe Saba, Hamis Shomary alisema kuwa baada ya kupata taarifa hizo walikwenda na kamati ya serikali ya mtaa kumuona mtoto huyo na kuweka mpango wa kumpeleka hospitali kwa matibabu zaidi.
Shomary alisema kuwa tatizo kubwa kwenye familia hiyo ni uwezo ndiyo umesababisha mtoto huyo asipate matibabu ya uhakika na kusababisha mguu wake kuzidi kuwa kwenye hali mbaya.
Naye Katibu wa Kamati ya Mtaa kwa watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu, Mwanahamis Saadi alisema kutokana na tatizo hilo, watahakikisha wanashirikiana na wadau ili mtoto huyo apatiwe matibabu ya kina.
Saadi alisema kuwa hata kama itatokea wadau wameshindwa kumchangia, watajitolea wao na kamati ya mtaa ili kuhakikisha Abuu anapata matibabu ili arejee shuleni na ndoto zake ziweze kutimia.
Aliyeguswa na tatizo la mwanafunzi huyo, awasiliane na bibi yake kwa namba 0718 56 95 77.
No comments:
Post a Comment