Tuesday 30 May 2017

ZINGATIA HAYA PALE UNAPOTAKA KUJENGA NYUMBA YA NDOTO YAKO.


Makala hii ni maalumu kwa wale ambao wana mpango wa kujenga nyumba za kisasa kwa gharama nafuu na katika hali ya usalama na kujiamini zaidi. Majengo ni moja kati ya mahitaji ya lazima ya mwanadamu ili aweze kuishi na kufanya shughuli zake za kimaendeleo katika hali ya usalama. Zaidi ya hapo nyumba zimekuwa ni mali katika mfumo wa maendeleo ya jamii na uchumi. 






Zaidi ya yote majengo yamekuwa ni kichocheo na alama ya maendeleo katika nchi na jamii kwa ujumla. Katika hali na umuhimu wa majengo hivyo kila Mtanzania anapaswa atimize hitaji la kuwa na nyumba katika hali yeyote aliyokuwa nayo. Lengo langu katika safu hii ni kuona kila Mtanzania anaachana na mawazo ya kuishi au kufanya shughuli zake kwenye majengo yasiyostahili, lazima uwepo utofauti wa makazi ya wanyama na makazi ya binadamu. Katika kutekeleza wajibu huu bado zipo sababu nyingi zinazochangia kukwamisha mafanikio miongoni mwetu. Zifuatazo ni sababu chache tu miongoni mwa sababu nyingi ambazo kwa kiasi kikubwa zinawakwamisha watanzania wengi kufikia ndoto za kuwa na nyumba za ndoto zao. Leo nitazungumzia changamoto za Kutokutumia wataalamu, kutokuwa na mpango kazi na maandalizi ya kutosha, Usimamizi usio bora na imara na zaidi ya yote kujenga kiholela 

1. TUMIA WATAALAMU 

Maendeleo ya sayansi na teknolojia katika fani mbalimbali duniani yameleta matokeo chanya katika maendeleo na ubunifu katika idara za ujenzi. Karne ya sasa hatujengi kwa mazoea tena, hali hii ndiyo imechochea kuzalishwa kwa wataalamu wa ujenzi duniani kote. Majengo ya kisasa yanajumuisha matumizi tofauti na yenye mifumo mbalimbali kukidhi matumizi halisi ya jengo husika. Ni muhimu sana kupata ushauri wa wataalamu kabla na wakati wa ujenzi wa nyumba ya ndoto zako. Kutokutumia wataalamu kutakuweka katika hatari usiyoijua, hii ni kutokana na wengi kujenga kwa mazoea kwa kujua au kwa kutokujua kuwa wana hatarisha uwekezaji wanaoufanya. 

Nayasema haya kwa kuwa napata huzuni sana ninapowaona watanzania wakilalama pale linapotokea janga kwenye nyumba aliyoitegemea kuendeshea maisha yake na familia kwa ujumla ikiangamizwa kwa dakika kadhaa kwa sababu zilizoweza kuzuilika na kufahamishwa endapo angewashirikisha wataalamu wa ujenzi. Nakusihi sana ukumbuke jambo hili kabla hujaanza kutekeleza ndoto zako ili ufanikishe kwa uhakika na usalama zaidi. 

SOMA; Yafahamu Mambo Muhimu Yanayoathiri Gharama Za Ujenzi Na Namna Ya Kupanga Mipango Bora Kabla Hujajenga Nyumba Yako. 

2. UJUE MPANGO KAZI KABLA YA UJENZI 

Jambo hili nimelisema sana na leo nalisema tena, ujenzi hugharimu fedha nyingi sana tofauti na wengi wanavyotarajia. Mchanganuo wa gharama na Mpango kazi ni dira ya rasilimali katika ujenzi. 

Mpango kazi wa ujenzi ni silaha yenye nguvu sana kabla na wakati wa ujenzi, Ni muhimu sana kuunda na kuweka mtaalamu wa kuratibu mpango kazi ili kuepuka matumizi mabaya ya rasilimali ambazo zilipaswa kutumika na kukidhi mahitaji husika. Mpango kazi ni njia pekee itakayo kufanya utoe maamuzi sahihi kwa kila hatua ya ujenzi. Watu wengi wameishia njiani na kutofikia ndoto zao kwa wakati na sababu mojawapo huwa ni kutokuwa na mpango kazi uliyo sahihi. Katika ujenzi muda, fedha na ubora ni ngao na rasilimali pekee inayosimamiwa na wataalamu wa ujenzi kuhakikisha lengo linafanikiwa. Migogoro mingi inayotokana na ujenzi sababu kuu mojawapo huwa ni rasilimali fedha. Jipange vema katika fedha kabla na wakati wa ujenzi kuepuka changamoto zisizo na ulazima. 

3. UJUE USIMAMIZI IMARA 

Tatizo la usimamizi katika ujenzi limekuwa ni jambo mtambuka katika ufahamu wa watanzania wengi katika kufikia ubora wa majengo. Kwa kiasi kikubwa wengi hutafuta mafundi wenye uzoefu na kuwakabidhi kila kitu kuanzia mipango hadi usimamizi. Lakini changamoto kubwa ni mabadiliko ya haraka yanayotokea katika sayansi ya uhandisi ujenzi, mapinduzi ya usanifu majenzi yanayoendelea kutokea hapa Tanzania si kila mtu anaweza kuyamudu. Umuhimu wa kutumia wataalamu unabaki kuwa ni jambo la lazima katika usalama wa ujenzi wako. Karne ya sasa tunalazimika kufanya mambo kwa weledi zaidi, epuka ubadhirifu, wizi na matumizi mabaya ya rasilimali wakati wa ujenzi kwa kutumia wataalamu wa usimamizi majenzi. Uaminifu na ushirikiano katika ujenzi ni msingi wa mafanikio, hivyo ni lazima uzingatiwe kuepuka migongano isiyo na ulazima. Nayasema haya kwa sababu wengi wameumizwa sana na jambo hili, tatizo kuu ni kuweka wasimamizi wasio na weledi katika ujenzi, msimamizi asiye na weledi katika ujenzi atashauri na kusimamia asichokijua. 

SOMA; Ufahamu Ujenzi Wa Gharama Nafuu Wa Nyumba Bora Za Kisasa 

4. EPUKA UJENZI HOLELA 

Kila jambo ndani ya jamii linaratibiwa na utaratibu fulani katika kukidhi vigezo vya ubora na usalama wa matumizi kwa watumiaji. Hata katika ujenzi zipo kanuni na taratibu mbalimbali zinazoratibu mfumo wa ujenzi ili kuweza kufikia ubora na usalama kwa watumiaji. Zipo bodi mbalimbali na taasisi za serikali zinazosimamia taratibu kuhakikisha ujenzi unazingatia vigezo vilivyowekwa ili kukidhi mahitaji husika. Lakini kwa kiasi kikubwa jambo hili limekuwa changamoto kubwa kwa watanzania wengi, wananchi wengi hawana uelewa mkubwa wa taratibu zinazopaswa kuzingatiwa kabla na wakati wa ujenzi. Katika hili wengi wameumia kwa kujua au kwa kutokujua. 

Vilio vingi vimesikika na bado vitaendelea kusikika endapo hakutakuwa na mbinu mbadala wa kuhakikisha kila Mtanzania anajenga na kuishi sehemu salama. Ingawa kwa jambo hili tatizo lipo kwa pande zote, wasimamizi na wananchi kwa ujumla lakini bado tunayo fursa ya kujipanga upya katika kufanikisha tunaishi katika mazingira na makazi salama. Katika hili huna budi kufuata taratibu zote ili ufurahie maisha kwa kuwa ujenzi ni uwekezaji ambao unapaswa kuwa sehemu salama ili kuepukana na hatari zinazoweza kuepukika. 



CHANZO:: http://www.amkamtanzania.com/

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!