Sunday, 14 May 2017

Zijue haki za mtoto anayeishi na mama gerezani

MKATABA wa Haki ya Mtoto unanukuu utangulizi wa Tamko la Haki za Mtoto unaosema, “Mtoto, kutokana na kutokukomaa kimwili na kiakili, anahitaji ulinzi na matunzo maalumu, ikiwa ni pamoja na ulinzi wa kisheria, kabla na baada ya kuzaliwa.”'


Hii pamoja na mambo mengine inamaanisha kuwa, hata wanaozaliwa gerezani na wale wanaokuwa wanakwenda na mama zao gerezani, wana haki ya kuendelea kubaki na mama zao katika magereza.
Sera inayotekelezwa sasa na Jeshi la Magereza inaeleza utaratibu mzima ambao Jeshi hilo linatakiwa kuufuata katika kuwahudumia watoto waliofungwa, walio mahabusu na pia waliozaliwa, waliokwenda na mama zao gerezani. Mkataba wa Mtoto pia unaelekeza kuwa mtoto hatakiwi kutenganishwa na wazazi wake isipokuwa tu, katika mazingira maalumu.
Hii ipo kwenye Ibara ya 9. Kanuni za Viwango vya Chini kuhusu Matunzo ya Wafungwa za Mwaka, 1955 (Kanuni za Mandela) zimeeleza kwa jumla mambo yanakubalika kama kanuni nzuri za utendaji katika utunzaji wa wafungwa na uendeshaji wa magereza.
Kanuni ya 23 inasema kuwa, sehemu maalumu ya kuishi itatengwa katika magereza ya wanawake kwa ajili ya matunzo kwa wakinamama wajawazito kabla na baada ya kujifungua na kuwekwa utaratibu ambao watoto watazaliwa katika hospitali nje ya magereza.
Hata hivyo kama mtoto atazaliwa gerezani, taarifa hili isitajwe katika cheti chake cha kuzaliwa na hii ni kwa ajili ya ustawi wa mtoto katika makuzi yake. Kanuni hiyo inaelekeza mtoto kuwekwa sehemu ya kulea watoto itakayokuwa na watu wenye ujuzi ikiwa watoto wachanga watabaki magerezani na mama zao.
Huu ni wakati ambao watoto hao wachanga hawako katika uangalizi wa mama zao, ndipo watawekwa katika sehemu maalum na kutunzwa.
Endapo itatokea kuwa wanawake walioko gerezani na watoto wao wanahitajika kupekuliwa, basi upekuzi huo usifanyike mbele ya watoto na ufanyike kwa kuzingatia heshima na pia maslahi bora ya mtoto, vinginevyo kuwe kuna sababu ya msingi ya kutofanya hivyo.
Kanuni ya 20 ya Kanuni za Sheria ya Mtoto (Makazi ya Kuzuizi), Mwaka 2012 pia inasema kuwa lazima kuwe na maeneo maalum kwa ajili ya utunzaji wa watoto na watoto wachanga ambao wako na mama zao.
Endapo mwanamke yuko kizuizini ataruhusiwa kuendelea kukaa na mtoto au watoto wake, ikiwa mtoto au watoto hao wako chini ya miaka miwili wakati mama akiwa amefikishwa gerezani, vinginevyo kama mama ataamua yeye mwenyewe vinginevyo.
Mkuu wa Gereza Kuu la Wanawake Kingolwira, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza, Loyce Ruhembe, anasema gereza hilo lina uwezo wa kuchukua wanawake 64. Anasema katika gereza hilo anaruhusiwa kuchukua wafungwa wanaokuja na watoto wao na pia wajawazito.
“Tunapokuwa na watoto hawa wanaokuja na mama zao au wanaozaliwa pale gerezani, Serikali inawatunza kwa kuwapa maziwa, nguo na vitu vingine vya kuwasaidia watoto hao,” anasema. Anasema gereza hilo pia lina shule ya awali iliyojengwa kwa ajili ya watoto wa wafungwa ingawa na watoto wa askari magereza wanasoma hapo na kwamba, waalimu ni askari.
Anasema katika gereza hilo, wanajishughulisha na mambo mbalimbali ya urekebishaji ambazo ni pamoja na ushonaji, kilimo cha uyoga, ufugaji wa sungura na kuku.
Kanuni za Umoja wa Mataifa za Matunzo ya Wafungwa wa Kike zinaeleza pia kuwa, wakati wa kupokelewa gerezani, wanawake wenye jukumu la kulea watoto wataruhusiwa kuwekewa utaratibu kwa watoto kwa kuzingatia maslahi bora ya watoto.
Aidha, maamuzi ya kuruhusu watoto kubaki na mama zao katika magereza yatazingatia maslahi bora ya watoto. Watoto wanaoingia gerezani na mama zao, hawatachukuliwa kuwa ni wafungwa na wanawake wafungwa atapewa muda wa kutosha kuwa na watoto wao.
Kanuni pia zinaeleza kuwa, watoto wanaoishi na mama zao magerezani watapatiwa huduma za afya na makuzi yao yatasimamiwa na wataalam wa watoto kwani malezi ya watoto yanatakiwa kukaribiana, kadri inavyowezekana, na malezi ya watoto nje ya magereza.
Nyingine ni maamuzi kuwa ni lini mtoto atenganishwe na mama yake yatategemea na tathmini ya mtoto mwenyewe na kwa kuzingatia maslahi bora ya mtoto na pia sheria za nchi.
“Kuondolewa kwa mtoto katika gereza kutafanyika kwa uangalifu mkubwa na hasa baada ya kupatikana kwa matunzo mbadala ya mtoto huyo,” anasema. Inaeleza pia kuwa, baada ya mtoto kutengenishwa na mama, huwekwa chini ya uangalizi wa familia au ndugu au matunzo mengine.
Mama atapewa fursa ya kutosha ya kukutana na mtoto wake, ikiwa ina maslahi bora ya mtoto na usalama wa jamii hautaathirika. Anasema wanawake wajawazito au wanaonyonyesha katika magereza watapatiwa ushauri kuhusu afya zao na lishe kupitia mpango utakaoandaliwa na kusimamiwa na mtaalam wa afya.
Chakula cha kutosha na kinachotolewa kwa wakati, mazingira salama, mazoezi ya kila mara yawepo na kutolewa bila malipo kwa wanawake wajawazito, watoto, watoto wachanga na wakina mama wanaonyonyesha. Aidha, wanawake wanaonyonyesha hawatakatishwa tamaa ya nyonyesha watoto wao vinginevyo kuwe kuna sababu muhimu za kiafya za kufanya hivyo.
Sera ya magereza inaeleza pia kuwa adhabu za kufungiwa au za kinidhamu za kutengwa hazitatolewa kwa wanawake wajawazito, wenye watoto wachanga na wanaonyonyesha na adhabu za kinidhamu kwa wafungwa wanawake wenye watoto hazitahusisha adhabu za kuzuia kukutana na familia zao na hasa watoto wao.
Kwa mujibu wa kanuni hizo, ni wajibu wa Jeshi la Magereza, pamoja na mambo mengine, kuhakikisha kuwa ikiwa watoto watabaki na mama zao magerezani, jitihada zifanyike kuwaelimisha askari magereza na wafanyakazi wengine kuhusu makuzi ya mtoto na makuzi yake.
“Jitihada zifanywe ili kuwa na program maalumu kwa ajili ya wanawake wajawazito, wanaonyonyesha, na wengineo wenye watoto magerezani maamuzi kuhusu kuwatoa wafungwa mapema kabla ya kumaliza vifungo vyao ama kwa masharti au bila masharti yatoe upendeleo maalum kwa wanawake wenye watoto magerezani,” inasema.
Mkataba wa Haki ya Mtoto unanukuu utangulizi wa Tamko la Haki za Mtoto unaosema hivi; “mtoto, kutokana na kutokukomaa kimwili na kiakili, anahitaji ulinzi maalum na matunzo, ikiwa ni pamoja na ulinzi wa kisheria, kabla na baada ya kuzaliwa.”
Mkataba wa Mtoto pia unataka kuwa mtoto hatakiwi kutenganishwa na wazazi wake isipokuwa tu katika mazingira maalum (ibara ya 9). Kanuni za Viwango vya Chini kuhusu Matunzo ya Wafungwa za mwaka, 1955 (Kanuni za Mandela) zimeeleza kwa jumla mambo gani yanakubalika kama kanuni nzuri za utendaji katika utunzaji wa wafungwa na uendeshaji wa magereza.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!