BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limetoa rambirambi ya Sh milioni 100 kwa familia za wafiwa wanafunzi na wafanyakazi wa Shule ya Msingi ya Lucky Vincent waliopoteza maisha katika ajali ya gari iliyotokea eneo la Rhotia Marera wilayani Karatu mkoani Arusha.
Kati ya fedha hizo, Sh milioni 86 zimetokana na posho ya kikao cha siku moja cha wabunge na Sh milioni 14 zimetolewa na Ofisi ya Spika. Akielezea utaratibu huo baada ya wabunge kusimama kwa dakika moja kuwakumbuka wanafunzi hao, walimu wawili na dereva waliopoteza maisha katika ajali hiyo wakati wakienda kufanya mtihani wa ujirani mwema, Spika wa Bunge hilo Job Ndugai alisema uamuzi wa kutoa posho wamekubaliana wabunge wote, CCM na Upinzani.
“Nimeshauriwa na pande zote za wabunge (Upinzani na CCM) tutoe posho ya siku moja kama rambirambi yetu na fedha hizo zigawiwe sawa kwa wafiwa yaani wazazi na ndugu wa marehemu, je, mnaridhia?,” alisema Spika Ndugai na wabunge wakajibu wameridhia. Bunge lina jumla ya wabunge 392 kati ya nafasi 393 zinazopaswa kuwepo na kwa siku posho ya kikao ni Sh 220,000.
“Tumekubaliana kwa kauli moja humu bungeni tutoe posho ya siku moja kama rambirambi yetu, posho hiyo tutaipeleka mara moja kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha na itagawiwa sawa sawa kwa wafiwa wote,” alieleza Ndugai. Kampuni mbalimbali za binafsi jijini Arusha nazo zimechangia mamilioni ya fedha kwa ajili ya msiba huo mkubwa uliotikisha nchi ikiwemo Kampuni ya uchimbaji madini ya tanzanite ya TanzaniteOne iliyotoa zaidi ya Sh milioni 10.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, alisema taasisi za kifedha za mifuko ya kijamii pamoja na Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro (NCAA) na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), wamechangia zaidi ya Sh milioni 100 kufanikisha usafiri, ununuzi wa majeneza na gharama nyingine za njiani kwa wanaokwenda mbali.
Gambo alisema kampuni ya binafsi ya utalii ya Kibo Gued imetoa magari yake 10 aina ya Toyota Landcruiser kwa ajili ya kusafirisha miili ya wafiwa wanaoenda mikoa ya Mbali. Pia alisema Mamlaka ya Maji Safi na Mazingira (AWSA) nayo imeguswa na msiba huo kwani imechangia Sh milioni moja ili kufanikisha shughuli hiyo.
Alibainisha kuwa matumizi yaliyotumika mpaka jana kwa ajili ya shughuli nzima yalikuwa ni zaidi ya Sh milioni 80.3 ikiwamo kila familia kupewa Sh milioni moja nje ya gharama ya usafiri na majeneza. “Mheshimiwa Makamu wa Rais, Serikali ya Mkoa wa Arusha imegharamia shughuli yote ya msiba huu ikiwa ni pamoja na kila familia kugharamiwa usafiri, majeneza na mazishi na kupewa shilingi milioni moja kila familia iliyofiwa,” alieleza Gambo na kuongeza kuwa michango inaendelea kupokelewa
No comments:
Post a Comment