Kumekuwepo na wimbi kubwa la matukio ya moto katika maeneo mbalimbali ya nchi. Hii inatokana na wananchi wengi kutokuwa na uelewa juu ya kinga na tahadhari ya majanga ya moto na pia kutokulijua vyema Jeshi la Zimamoto na uokoaji pamoja na majukumu yatolewayo na jeshi hilo.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Tanzania limeanzishwa kwa sheria namba 14 ya mwaka 2007 na kwa mujibu wa sheria tajwa, jeshi hili linao wajibu wa kuzima moto, kuokoa maisha na mali na kushughulikia dharura zote zisizokua za kihalifu. Katika kufanikisha jukumu lake, Jeshi linashirikiana na wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na wananchi kutekeleza kazi zake. Ili kufanikisha dhima ya jeshi kuzuia majanga ya moto, elimu ni muhimu ili kuwawezesha watu kukabiliana pale unapotokea.
Moto ni muwako unaotoa joto na mwanga ambao hadi utokee unahitaji vitu vitatu (pembe tatu za moto) ambavyo ni Oksijeni, Joto (kiwashio) na fueli (kinachowaka). Oksijeni husaidia moto kuwaka, Joto (kiwashio) hupandisha kiwango cha joto cha kitu kinachoweza kuwaka ili kiweze kuwaka na fueli ni kitu chochote kinachoweza kuwaka. Fueli hupatikana katika hali tatu ambazo ni yabisi (ugumu), vimiminika na gesi.
Moto umegawanyika katika makundi saba ambayo ni kundi A linalohusisha karatasi, nguo, nyasi na mbao (jamii ya mimea) na huzimwa kwa kutumia maji au mchanga mkavu. Kundi B ni moto wa petroli, dizeli, mafuta ya taa na mafuta ya kupikia na huu huzimwa kwa kutumia povu. Kundi C ni moto wa butani, propane, methane na asetilini na huu huzimwa kwa kutumia poda kavu na hewa ya ukaa.
Kundi D ni moto wa sodium, magnesiamu, chuma na shaba na huzimwa kwa kutumia poda kavu maalumu au mchanga mkavu. Kundi F ni moto wa mafuta ya kupikia ambao huzimwa kwa kutumia hewa ya ukaa. Kundi la mwisho ni moto unaosababishwa na umeme ambao unaweza kuzimwa na poda kavu, hewa ya ukaa au mchanga mkavu. Kuna sababu mbalimbali ambazo zinaweza kusababisha moto.
Sababu hizo ni uvutaji sigara na utupaji ovyo vipande vya sigara, uchomeleaji vyuma bila ya uangalifu, hitilafu za umeme, radi, kuacha chakula jikoni kikichemka bila uangalizi na watoto kuchezea viberiti Visababishi vingine ni msuguano kutokana na kukosekana kwa vilainishi, kuchoma makusudi, kuchoma taka bila uangalifu, kuchoma nyasi wakati wa utayarishaji mashamba na kutotumia kwa uangalifu mishumaa, viberiti, majiko yanayotumia mafuta ya taa au gesi.
Kuna hatua mbalimbali ambazo zikifuatwa zinaweza kuzuia au kupunguza matukio ya moto. Hatua zenyewe ni kuzuia uvutaji wa sigara katika maeneo yasiyofaa na matumizi ya vifaa vya umeme vilivyoidhinishwa na taasisi zinazotambuliwa kitaifa au kimataifa kama Shirika la Vipo (TBS), Hatua nyingine ni kuwa na matumizi mazuri ya mioto iliyo wazi kama vile mishumaa na majiko.
Ni muhimu pia kutengeneza barabara au njia za kuzuia moto kuzunguka mashamba na misitu na hatua ya mwisho ni majengo kuwekewa vifaa vya kinga dhidi ya radi na vizimia moto vya awali. Endapo utagundua kuwa kuna moto mahali ulipo kuna vitu muhimu vya kufuata ili uweze kuokoa maisha pamoja na mali na sio kuchanganyikiwa hadi kufikia hatua ya kuhatarisha maisha yako.
Mambo muhimu ya kufuata ni kupiga king’ora, kengele au mayowe, kuita Jeshi la Zimamoto na uokoaji haraka kwa kutumia namba ya simu 114. Jaribu kuzima moto kwa kutumia vizimia moto vya awali bila kuhatarisha usalama wako na watu wengine wanaokuzunguka.
Kwa sehemu za kazi watumishi wasiohusika na uzimaji moto wakusanyike sehemu maalumu ya kukusanyikia na wakishakusanyika waitwe majina ili kujua nani hayupo, askari wa Jeshi la Zimamoto au polisi waelezwe kama kuna mtu haonekani, swichi kuu ya umeme izimwe na unapozima moto hakikisha mlango upo nyuma yako.
Iwapo umezingirwa na moshi, tambaa kwa kutumia magoti na mikono na mwisho hairuhusiwi kurudi ndani ya jengo linalowaka moto hadi itakapokuwa salama kufanya hivyo au utakaporuhusiwa na ofisa wa Zimamoto. Kuna vifaa mbalimbali vinavyotumika kuzimia moto hususani mioto ya awali.
Vifaa hivyo vimegawanyika katika makundi makuu mawili yani vifaa visivyobebeka (hose reel, rising main, ring main, automatic fire alarm system na automatic sprinklers system); na vifaa vinavyobebeka (portable fire appliances) kama vile mitungi ya kuzimia moto, blanketi maalumu la kuzimia moto na kifaa kiitwacho fire beater. Mitungi ya kuzimia moto ipo ya aina tano ambayo ni pamoja na mtungi wa maji ambao hufaa sana kuzimia mioto ya kundi A hapo juu.
Hairuhusiwi kuzimia moto uliosababishwa na hitilafu ya umeme kabla ya kuzima swichi kuu ya umeme. Wa pili ni mtungi wenye kemikali ya povu ambao hufaa kuzimia mioto ya kundi B. Mitungi yenye poda kavu hufaa kuzimia mioto ya kundi A, B, C. Mitungi yenye hewa ya ukaa hufaa kuzimia mioto ya kundi B na mitungi yenye kemikali inafaa kuzimia moto wa kundi F. Hii hufaa sana kuzimia mioto ya mafuta ya kupikia ambayo joto lake hufikia au kuzidi nyuzijoto 360.
Mitungi hii ina hatua zake za kufuata ili kutumia, ambapo hatua ya kwanza ni kuondoa pini ya usalama, hatua ya pili ni kulenga kwenye kitako cha moto (fire base), hatua ya tatu ni kuminya au kukamua mikono ya mtungi ili kuruhusu kizima moto. Mwandishi wa makala haya ni ofisa wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.
No comments:
Post a Comment