Wednesday 31 May 2017

Tuisaidie Serikali kupambana na ebola

UGONJWA wa ebola umeripotiwa kulipuka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) huku watu 43 wakiambukizwa na wanne kufa. Nchi zinazopakana na DRC ikiwemo Tanzania, zimeanza kuchukua hatua za kudhibiti ebola isienee katika maeneo yake ili kuwalinda raia.


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema Serikali imeshatumia Sh bilioni 1.5 kudhibiti ebola. Udhibiti huo unahusisha ukaguzi wa wageni wote wanaoingia nchini kutoka DRC kupitia njia za barabara, viwanja vya ndege na bandari.
Lengo la hatua hiyo ni kubaini kama wana ebola au dalili zake kwa kuwapima joto lao la mwili na hivyo kudhibiti wasiueneze na pia kujikinga. Tunaipongeza Serikali kwa kuchukua hatua za haraka kudhibiti kuenea kwa ebola kwa kupima wageni wote wanaoingia na kukinga wenyeji.
Hatua hiyo itasaidia kuwahakikishia wananchi, usalama wa afya zao unaotishiwa na ugonjwa huo na kuokoa nguvu kazi kupotea kwa vifo. Tunaomba wananchi nchini kote, waunge mkono hatua hiyo ya Serikali kudhibiti kuenea kwa ebola kwa kufuata maelekezo inayoyatoa.
Kwa mfano, Serikali imesema sanjari na kuweka vifaa vya kupima homa na dawa za tiba, itatoa elimu ya kujikinga na ugonjwa huo wa hatari. Ni vyema basi wananchi wote waishio mpakani mwa DRC na wanaopokea wageni kupitia njia za viwanja vya ndege, barabara na bandari kuchukua tahadhari ili wasiambukizwe nao.
Tunaomba wafanyakazi kwenye mipaka ya Tunduma, Namanga, viwanja vya ndege Kigoma, Songwe, Mwanza, Arusha, Kilimanjaro, Zanzibar, Julius Nyerere Dar es Salaam nao kujiandaa kushiriki kudhibiti kuenea kwa ebola.
Tukifanya hivyo, itakuwa rahisi kwa nchi kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo katika maeneo zaidi ya DRC na hivyo kuokoa watu wetu na majirani. Kama tuliweza kudhibiti kuenea kwa ebola kwa kudhibiti mipaka yetu ilipolipuka kwa mara nyingine nchi za Afrika Magharibi, hatuoni kwa nini tushindwe kuidhibiti sasa ikitokea jirani.
Kinachotakiwa ni kuweka nia ya dhati ya kutaka kuutokomeza ugonjwa huo kwa hatua mujarab za kujikinga nao na pia kutumia dawa inapobidi. Tukifanya hivyo, tutakuwa tumeliokoa Taifa na janga ambalo linaweza kusababisha hasara kubwa ya rasilimali watu, vifaa na fedha wakati huu ambao Serikali inadhibiti matumizi yake.
Haya shime Watanzania tushirikiane kudhibiti ebola kwa kuhakikisha tunatoa ripoti ya kila mgeni anayeingia na tunamhisi ana dalili au anao ugonjwa huo ili aweze kutibiwa haraka.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!