Friday, 12 May 2017

Muhongo afariji waliofukiwa na kifusi

WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amezuru eneo la machimbo ya madini, kulikotokea maafa ya wachimbaji saba kupoteza maisha kwa kufukiwa na kifusi na mwingine kukosa hewa, Aprili 20, mwaka huu wilayani Sikonge mkoani Tabora.


Ziara ya Profesa Muhongo katika machimbo yaliyopo wilayani Sikonge, ilifanyika Mei 8, mwaka huu, ambayo ililenga kuwafariji wananchi, kuzungumza na wamiliki wa migodi pamoja na wachimbaji na kutoa mwongozo wa serikali kuhusu hatua za kufuatwa ili kuhakikisha shughuli za uchimbaji wa madini zinafanyika kwa usalama.
Akizungumza na wananchi baada ya kukagua eneo yalipotokea maafa, Profesa Muhongo alitoa muda wa siku tatu kwa Mkaguzi Mkuu wa Migodi nchini, Ally Samaje kwa kushirikiana na Ofisi ya Madini Kanda ya Kati-Magharibi, Ofisi ya Ofisa Madini Mkazi Tabora pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa husika ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Aggrey Mwanri, kufanya ukaguzi na kuchukua hatua zitakazohakikisha shughuli za uchimbaji mahala hapo zinafanyika kwa usalama.
Akifafanua zaidi kuhusu mambo muhimu yanayopaswa kuzingatiwa na timu hiyo ya ukaguzi, alisema ni lazima ipatikane orodha kamili ya wananchi walio tayari kufanya kazi katika migodi husika ili wajulikane, kukagua kwa kina eneo lote la migodi ili kujionea hali halisi pamoja na kutoa mwongozo/ushauri kwa wamiliki wa leseni husika kuhusu namna bora ya kuendesha shughuli za uchimbaji wa madini kwa njia salama.
Akizungumza hilo, Samaje, kwa niaba ya timu iliyoagizwa na waziri kushughulikia hatua za kiusalama, alisema tayari wamekamilisha kazi waliyopewa na kwamba wamewapatia mwongozo wa utendaji kazi wamiliki wa leseni husika.
Alitaja baadhi ya mambo muhimu ambayo timu hiyo imeshughulikia kuwa ni pamoja na kutoa maagizo katika eneo la mgodi wenye leseni ya uchimbaji mdogo wa madini namba 002211 CWZ, inayomilikiwa na kikundi cha WINIMA, na ambalo ndilo lilihusisha vifo vya watu sita kwa kufukiwa na kifusi, kuwa na mashimo ya uchimbaji 16 tu badala ya 200 yaliyokuwepo awali.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!