WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imetangaza ahueni kwa wananchi kumiliki ardhi, ambapo kuanzia Julai Mosi, mwaka huu, itapunguza tozo ya mbele ya thamani ya ardhi kutoka asilimia 7.5 hadi 2.5.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alisema hayo Bungeni Dodoma jana wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2017/18. Lukuvi alisema punguzo hilo ni sawa na asilimia 67 ya tozo hiyo, hali itakayowasaidia wananchi kumiliki mashamba na viwanja vilivyopimwa.
Alisema lengo la kufuta tozo hizo ni kuwezesha wengi kumiliki maeneo yao kwa gharama nafuu na kupanua wigo wa walipa pango la ardhi. “Ada hii hutozwa mara moja wakati wa umilikishwaji ardhi kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999. Kupunguzwa kwake kutavutia wananchi wenye maeneo ya ardhi kujitokeza kwa wigi zaidi kupimiwa viwanja na kumilikishwa ardhi yao,” alisema.
Alisema pia kupunguzwa kwa tozo hiyo kutapunguza gharama kubwa za sasa za viwanja na kufanya wengi kumudu kumiliki viwanja vilivyopimwa. Pamoja na hayo, alisema wizara inatarajia kuongeza viwango vya pango la ardhi kutoka Sh 400 hadi Sh 1,000 kwa ekari kuanzia Julai, mwaka huu, kwa mashamba ya biashara yaliyopimwa na kumilikishwa nje ya miji.
“Mashamba hayo yanatozwa kiwango cha shilingi mia nne kwa ekari moja, kiwango hiki bado ni kidogo ikilinganishwa na thamani pamoja na uwezo wa uzalishaji wa ardhi husika,” alisema na kutahadharisha kuwa ongezeko hilo la pango la ardhi, halihusishi wale wote wenye hati za kimila ambao wao kwa sasa hawatozwi kiasi chochote kwa mujibu wa sheria.
Aliwataka wamiliki wote wa ardhi nchini ambao mpaka sasa hawajalipa kodi ya pango kuhakikisha wanalipa kodi hiyo kabla ya Juni 30, mwaka huu. Alisema serikali haitasita kuwachukulia hatua wasiolipa kodi hiyo kwa kuwafikisha mahakamani, kukamata na kuuza mali zao na kuwafutia miliki. Alisema wanakamilisha mipango kabambe ya majiji ya Dar es Salaam na Tanga, Singida, Ifakara, Mahenge, Malinyi, Bariadi, Kibaha na Korogwe.
Akitoa maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mjumbe wake, Silafu Maufi aliishauri serikali kuhakikisha inapanga matumizi ya ardhi kwa kuzingatia ongezeko la wananchi. “Hakuna uwiano wa ongezeko la watu na ardhi iliyopo, ardhi ni rasilimali muhimu ambayo shughuli zote za kijamii, kiuchumi na kimaendeleo zinafanyika. Hii ni rasilimali adimu ambayo hushindaniwa,”alisema.
Lukuvi pia alizungumzia Mamlaka ya Ustawishaji wa Mji wa Kigamboni (KDA) alisema ana maombi ya Halmashauri ya Kigamboni na Mbunge wa jimbo hilo, Dk Faustine Ndugulile kuhamishia shughuli hizo halmashauri.
No comments:
Post a Comment