Tuesday, 30 May 2017

IGP Sirro ala kiapo, kuanza na Kibiti

MKUU mpya wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro amesema kwamba kazi yake ya kwanza atakayoanza nayo katika wadhifa wake mpya ni kupambana na uhalifu hasa nchini uhalifu, unaoendelea katika wilaya za Kibiti, Mkuranga na Rufiji mkoani Pwani.


Akizungumza baada ya kuapishwa na Rais John Magufuli, Ikulu jijini Dar es Salaam jana, Sirro ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa ni Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, alisema kwa matatizo ya Rufiji, kinachohitajika zaidi ni ushirikiano kutoka kwa wananchi. Alisema bila wananchi kushiriki kikamilifu katika kutoa taarifa, mapambano dhidi ya uhalifu yatakuwa magumu.
Alisema wananchi wanatakiwa kutoa ushirikiano mkubwa kwa jeshi lao la polisi ili wahalifu wanaoendesha uhalifu katika maeneo hayo waweze kukamatwa. “Najua tuna changamoto ya Ikwiriri na Kibiti, lakini niwahakikishie wakazi wa Pwani kuwa tuko vizuri tutaenda huko kufanya kazi, tunachoomba kutoka kwa wananchi ni ushirikiano,” alisema IGP Sirro.
Sirro alisisitiza kuwa katika kushughulikia tatizo hilo, ataenda huko Rufiji, Mkuranga na Kibiti kuangalia mazingira yalivyo na namna ambavyo polisi imejipanga kupambana na tatizo hilo.
“Kipaumbele changu ni uhalifu na kazi ya Polisi ni kuzuia na kupambana na uhalifu, tunataka Watanzania waishi kwa amani na hata wana Pwani nao waishi kwa amani,” alisema na kuongeza kuwa kingine anachotegemea katika kufanikisha kazi yake ni ushirikiano kutoka kwa watendaji wa Polisi wanaotakiwa kuwa na nidhamu ya hali ya juu.
“Kwa umoja wetu tutapunguza uhalifu kwa kiasi kikubwa kama ambavyo tumefanikiwa katika Mkoa wa Dar es Salaam,” alisema IGP Sirro na kusisitiza wananchi waendelee kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi katika kutokomeza uhalifu nchini.
Mangu: Atafanya kazi nzuri Kwa upande wake, IGP Ernest Mangu ambaye ameondolewa madarakani juzi na Rais Magufuli, alitoa mwito kwa wananchi kumpa ushirikiano wa kutosha mkuu mpya wa Jeshi la Polisi kama ambavyo walikuwa wanampatia yeye ili afanye kazi zake kwa ufanisi.
“Bahati nzuri IGP sio mgeni polisi, anazifahamu changamoto zote za Jeshi la Polisi, nina hakika atafanya vizuri,” alisema Mangu. Mangu alisema kwa sasa kuna uhalifu mkubwa huko Rufiji ambao alisema Watanzania hawakuwahi kuushuhudia na akaongeza kuwa anaamini kwamba IGP mpya ataendeleza mapambano ambayo yeye alishayaanza.
Sirro aliteuliwa juzi na Rais Magufuli kushika wadhifa huo kuchukua nafasi ya Mangu aliyeteuliwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete, Desemba 30, 2013 kuchukua nafasi ya Said Mwema ambaye alistaafu kwa mujibu wa sheria.
Mangu aliapishwa Desemba 31, 2013 na kuanza kazi Januari mosi, 2014. Mangu (58) kabla ya uteuzi wake wa kuwa IGP, alikuwa Mkurugenzi wa Intelijensia ya Jinai katika Jeshi hilo la Polisi.
Hakuna ambaye alikuwa tayari kutaja sababu ya Mangu kuondolewa katika wadhifa wake huo. Licha ya kuwa baadhi ya wadadisi wa mambo wamekuwa wanaeleza kuwa kuna uwezekano sababu kubwa iliyosababisha kung’olewa kwa IGP huyo ni uhalifu unaoendelea wilayani Kibiti na Rufiji.
Watu takribani 32 wameshauwa katika maeneo hayo wengi wao wakiwa Polisi na viongozi wa Chama cha Mapinduzi jambo ambalo lilifanya chama hicho tawala kutoa tamko la kulaani mauaji hayo na kuhoji iweje wanaouawa wawe viongozi wa chama hicho peke yake.
Katika tamko lake alilolitoa hivi karibuni, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha vinaelekeza akili, nguvu zao katika wilaya hizo kwa kuwa mauaji hayo yanasababisha kuzorota kwa shughuli za maendeleo.
Mtweve ampongeza
Baadhi ya wakazi wa Jiji la Mwanza, viongozi wa madhehebu ya dini na watu waliosoma na kufanya kazi kwa karibu na IGP Sirro, wamempongeza kwa uteuzi wake na kwamba matarajio yao ni kuona Jeshi la Polisi linafanya kazi kwa kuzingatia maadili katika kudhibiti matukio ya uhalifu yaliyopo nchini.
Wamesema Rais Magufuli hajakosea kumteua Sirro kwa madai kuwa rekodi yake ya utendaji ndani ya Jeshi la Polisi inafahamika na ni mchapakazi.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza ambaye pia aliwahi kuwa Kamishina wa Fedha na Lojistiki wa Polisi nchini, Clodwig Mtweve alimshukuru Rais Magufuli kwa kumteua Sirro kushika wadhifa huo, kwani ni sehemu ya majukumu yake kama Amiri Jeshi Mkuu kupanga majeshi yake.
“Amemteua Sirro baada ya kujiridhisha kuwa atatekeleza majukumu yake ndani ya jeshi hilo, binafsi nampongeza kwa uteuzi wake huo na nina imani ataliunganisha jeshi kuleta ufanisi wa kazi,” alifafanua Mtweve.
RPC Msangi anena
Naye Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi amempongeza IGP Sirro, na kueleza kuwa ni mtu aliyefahamiana naye siku nyingi tangu walipokutana Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Kilimanjaro, yeye (Sirro) akiwa amehamia kutoka Shule ya Sekondari ya Seminari ya Maua kati ya mwaka 1985-1986.
Alisema amemfahamu Sirro tangu alipokuwa shuleni, alikuwa ni mtu ambaye anafikiri kwa haraka na kwamba dalili za uongozi alizianza tangu akiwa shuleni na amefanya kazi naye tangu akiwa Chuo cha Polisi, Mkuu wa Makosa ya Upelelezi ya Jinai Magomeni, Kamanda wa Polisi mikoa ya Tanga, Shinyanga, Mwanza na Kanda Maalumu Dar es Salaam.
“Ni mtu ambaye ana uzoefu wa kutosha wa masuala ya kijeshi kwani aliweza kudhibiti mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi, wazee na vikongwe kwa mikoa ya Shinyanga na Mwanza halikadhalika ameendelea kudhibiti matukio ya uhalifu kwa mkoa wa Dar es Salaam hadi kuteuliwa kwake,” alieleza Kamanda Msangi.
Msangi alisema kuwa IGP Sirro anayafahamu vyema majukumu ya Jeshi la Polisi na kwamba matarajio yake ni kuona ufanisi na uongozi bora kwa watu anaowaongoza ili wampatie ushirikiano wa kutekeleza majukumu yake.
“Natumaini hatojiangusha baada ya kuaminiwa na Mheshimiwa Rais kukabidhiwa kijiti hicho cha uongozi ili kuhakikisha kuwa Jeshi la Polisi linatoa huduma bora kama inavyotarajiwa na wananchi wa kada zote bila ya kumuonea wala kumpendelea mtu kwa kuhakikisha sheria za nchi zinafuatwa,” alifafanua.
Askofu, Shekhe wamkubali
Kwa upande wake, Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani Mkoa wa Mwanza, Shehe Hassan Kabeke alisema amefanya kazi kwa karibu na IGP Sirro wakati alipokuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, na kwamba ni mtendaji mzuri na mfuatiliaji wa mambo na anajua anachokifanya.
“Matarajio yangu ni kuona mwendelezo wa kazi nzuri ya jeshi la polisi nchini katika kudhibiti uhalifu,” alieleza. Naye Askofu Mkuu wa Kanisa la Gethsemane Assemblies of God la jijini Mwanza, Steven Gonga alisema baada ya kusikia uteuzi wa IGP Sirro juzi akitokea kanisani, alipofika nyumbani kwake alipiga magoti na kumuombea kwa Mungu.
“Namfahamu Kamanda Sirro tangu akiwa hapa Mwanza na Dar es Salaam kama Kamishina wa Kanda Maalumu, ni mmoja wa makamanda wa polisi wanaofanya kazi kwa weledi wa hali ya juu, lakini pia uwajibikaji ni jambo analolipa kipaumbele,” alisema Askofu Gonga.
Meneja Mahusiano na Habari wa Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi Tanzania, Josephat Torner alisema uteuzi wa Sirro haujakosewa kutokana na kuwa na rekodi nzuri ya utendaji iliyotukuka.
“Bila kuficha nimeufurahia uteuzi aliofanya Rais Magufuli kwa kumteua Sirro kuwa IGP, nimefanya naye kazi kwa karibu wakati akiwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, ni mchapakazi na msikivu, habagui dini, kabila wala rangi ya mtu,” alieleza na kuongeza kuwa ni matumaini yake sasa wimbi la mauaji ya wenye ualbino litakomeshwa

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!