Monday, 17 April 2017

Utekaji watikisa mahubiri Pasaka


Rais John Magufuli akisalimiana na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, baada ya misa ya Pasaka katika Kanisa la Mtakatifu Petro jijini Dar es Salaam jana

HOFU iliyoanza kujijenga katika jamii kutokana na kuwapo kwa vitendo vya utekaji watu na pia kuibuka kwa vitendo vya mauaji yakiwamo ya polisi wanane wilayani Kibiti Alhamisi iliyopita
ni miongoni mwa mambo yaliyotikisa katika mahubiri baada ya ibada ya Sikukuu ya Pasaka katika makanisa mbalimbali nchini, jana.

Aidha, licha ya kulaani mauaji ya polisi wasio na hatia wilayani Kibiti, Pwani na kutaka waliohusika na unyama huo kusakwa popote walipo ili wafikishwe kwenye mkono wa sheria, maaskofu na viongozi wengine walitumia mahubiri hayo ya Pasaka kuwahimiza Watanzania wazidishe upendo na mshikamano kwa nia ya kumridhisha Mungu kwa matendo hayo mema.

Hivi karibuni kumetokea matukio kadhaa ya utekaji yaliyozua gumzo kubwa kuhusiana na hofu ya kutetereka kwa hali ya usalama nchini, yakiwamo ya Ben Sanaane ambaye ni kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) aliyetoweka kwa zaidi ya miezi minne sasa. Mwingine aliyetekwa na watu wasiojulikana kabla ya kupatikana siku tatu baadaye ni nyota wa bongofleva, Roma Mkatoliki.
Aidha, matukio ya ujambazi na mauaji dhidi ya watu wasio na hatia yaliongeza hofu nyingine Alhamisi iliyopita baada ya askari Polisi wanane waliokuwa kazini kushambuliwa kwa risasi wakiwa kwenye gari na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi katika eneo la Mkengeni, Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani. Katika tukio hilo, askari mwingine alijeruhiwa na kisha wauaji kutwaa bunduki walizokuwa nazo askari na kutokomea nazo kusikojulikana.
Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi, Mhashamu Isaac Amani; Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu wa Katoliki Tanzania (Tec), Padri Raymond Saba; Askofu wa Kanisa la Anglikana Zanzibar, Michael Hafidh; Padri Fabian Muhoja wa parokia ya Bujora, Mwanza na Askofu Josephat Gwajima wa Kanisa la Ufufuo na Uzima jijini Dar es Salaam ni miongoni mwa wale waliotoa mahubiri yaliyozungumzia hali ya amani na umuhimu wa jamii kuzidisha upendo.
Wengine waliotoa mahubiri ya kuhimiza upendo ni pamoja na Askofu Mkuu wa Jimbo la Arusha, Josephat Lebulu; Askofu wa Kanisa la Morovian (MRCT), Emmaus Mwamakula; Mkuu wa Dinari ya Pwani Jimbo la Tanga, Moses Shemweta; Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika (DCT), Dk. Dickson Chilongani na Mchungaji wa Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ushirika wa Mwanakwerekwe Zanzibar, Shukuru Steven Maloda.
“Tunalaani maovu yote yanayoliingiza taifa letu katika kaburi la hofu. Hatima ya Tanzania ipo mikononi mwetu. Tuombe Mungu atufungue vifungo hivi kwa sababu matukio ya utekaji, utesaji, mauaji ya vikongwe, biashara ya viungo kwa watu wenye ulemavu wa ngozi na kupotea watoto si mambo ya kushangilia,”’alisema Askofu Amani katika sehemu ya mahubiri yake kwenye Kanisa la Kiaskofu la Parokia ya Kristo Mfalme mjini Moshi, jana.
Askofu Amani alisema matukio ya utekaji na utesaji wa raia yaliyojitokeza hivi karibuni, yanaweka giza katika amani iliyopo na hivyo, jambo hilo halipaswi kuachwa liendelee.
Akieleza zaidi, Askofu Amani alisema baadhi ya Watanzania wamejiingiza katika ujambazi kwa kuufanya uhalifu kuwa ajira, bila kujali na kuthamini utu wa mwanadamu.
Akionyesha kuchukizwa na taarifa za kuwapo kwa baadhi ya watu kushangilia mauaji ya askari wanane wa Jeshi la Polisi wilayani Kibiti, Askofu Amani alisema jambo hilo ni baya na hivyo kuna kila sababu kwa kila Mtanzania kusaidia msako dhidi ya wahusika wake popote pale walipo ili hatimaye sheria itwae mkondo wake.
PADRI SABA JIMBO KUU DAR
Wakati akisoma tafakari ya neno katika ibada ya mkesha wa sikukuu ya Pasaka juzi usiku, kwenye Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph, Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Padri Saba alisema utekaji na mauaji ya watu wasio na hatia ni matukio yanayowakosesha watu amani na upendo na hivyo yanapaswa kulaaniwa na kila mmoja kuyapiga vita kwa nguvu zote.
Aliongeza kuwa vitendo aina hiyo, pamoja na ufisadi na uzembe katika jamii, vinaashiria kuwa bado kuna watu hawajafufuka, hali ambayo ni kinyume cha sikukuu ya Pasaka.
“Wanaotenda matendo hayo wakati mwingine ni sisi ambao tunafanya ibada na kujitanabahisha kuwa ni Wakristo. Pasaka itufanye na sisi tufufuke na Yesu Kristo kwa kuishi katika maisha na imani mpya, na kuepuka matendo yanayoeneza chuki baina yetu,” alisema Padri Saba.
Paroko wa Kanisa la Kristo Mfalme Parokia ya Tabata jijini Dar es Salaam, Padri Peter Shao, akiongoza ibada ya mkesha wa sikukuu hiyo, alisema katika dunia ya leo vitendo vya ukatili vimekithiri ambavyo haijulikani wananchi wamevitoa wapi na hivyo, kila mmoja ajiepushe na mambo hayo yanayomchukiza Mungu.
.
"Huu ukatili tumeutoa wapi? Hivi vitendo vya kutekana nyara, kuuana, kuchukiana tumevitoa wapi? Pasaka hii itubadilishe na tuishi katika imani ya Mungu,” alisema Padri Shao.

ASKOFU HAFIDH - ZANZIBAR
Askofu Hafidh alisema taarifa za matukio ya utekaji katika jamii na matendo mengine aina hiyo huwafanya wabunge na wananchi kupoteza furaha na amani, hivyo kila mmoja anapaswa kujiweka mbali nayo na kutenda mambo yaliyo mema.
Askofu Hafidh aliyasema hayo wakati akiongoza ibada ya Pasaka iliyofanyika katika Kanisa la Mkunazini, Zanzibar.
“Huwezi kuwa na amani bila ya kuwa na furaha ndani ya moyo. Wabunge na wananchi wamekuwa na wasiwasi wa maisha yao kutokana na kupoteza furaha moyoni,” alisema Askofu Hafidh.
Aliongeza kuwa wakati umefika kwa viongozi kurejesha furaha kwa wananchi wao ili kuendeleza misingi ya amani, utulivu na umoja wa kitaifa, huku pia akilaani mauaji ya askari polisi wasio na hatia wilayani Kibiti.
PADRI MUHOJA - MWANZA
Padri Muhoja wa Parokia ya Bujora wakati akiongoza misa ya mkesha wa sikukuu ya Pasaka kwenye Kanisa Katoliki la Sub-Parish ya Ihayabuyaga Jimbo kuu la Mwanza, alihimiza amani na upendo na kutaka Pasaka iwe chanzo cha kukumbuka wajibu huo kwa kila mmoja.
Aidha, katika adhimisho la ibada ya Pasaka, Katekista Bonephase Kadogosa alisema ukweli wa imani unadhihirisha Yesu Kristo amafufuka kwa kuishi maisha ya kumwabudu Mwenyezi Mungu na kushika amri zake.
ASKOFU LEBULU - ARUSHA
Askofu Lebulu wa Jimbo la Arusha alisema iwapo Watanzania hawajui wapi wanatoka na kwenda, basi ni balaa kubwa.
Katika mahubiri yake ya sikukuu ya Pasaka yaliyofanyika Kanisa la Kiaskofu la Mtakatifu Theresa jijini Arusha jana, Askofu Lebulu alisema ufufuko wa Yesu Kristo umeondoa giza mioyoni mwa waumini na kuwaletea mwanga.
“Tumshukuru Mungu kwa uhai aliotupatia na mwanga…kama hakuna mwanga kuna giza na hali hiyo ndiyo tunasema ni kukosa maarifa,” alisema.
Mchungaji kiongozi wa Usharika wa Njiro na Kijenge wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Francis Letara, akihubiri katika ibada ya Pasaka iliyofanyika Mtaa wa Sayuni Njiro, aliwataka Wakristo kufanya matendo mema yanayompendeza Mungu.
ASKOFU MWAMAKULA - DAR
Askofu Mwamakula aliwataka Watanzania kuzingatia matendo mema (ikiwamo kuacha matendo ya kikatili) na pia kuacha kutumia vibaya mitandao ya kijamii kunakoendelea hivi sasa na kwamba, kuendelea kufanya hivyo kunaweza kuharibu amani ya nchi.
Alisema hayo katika ibada ya Kongamano la Sikukuu ya Pasaka la Umoja wa Wanafunzi wa Kikristo Tanzania (Ukwata).
“Utamaduni wa kuvumiliana katika nchi yetu umeanza kupotea taratibu na hali hii imeanza kuonekana tangu Januari mwaka huu, wapo baadhi ya watu wanaandaa ‘skendo’ kwa ajili ya watu wengine.
“Si kwa wabunge, wanasiasa, wananchi wa kawaida na makundi mbalimbali hii sio dalili njema kwa amani ya nchi yetu. Tuikemee,” alisema Mwamakula.
ASKOFU CHILONGANI - DODOMA
Askofu Chilongani aliwaasa Watanzania kuwaamini viongozi wao kwa kuwa wanaweza kuibadili Tanzania kiuchumi.
Aliyasema hayo wakati alipokuwa akihubiri katika ibada ya sikukuu ya Pasaka katika Kuu la Anglikana Mjini Dodoma, jana.
Aidha, aliwataka Watanzania kuamini maono ya viongozi wao kwa kuwa wasipofanya hivyo ni dhambi kubwa itakayowaangusha.
Katika hatua nyingine, Paroko Onesmo Wisi wa Kanisa Kuu Katoliki la Paulo wa Msalaba Jimbo Kuu lililopo mkoani Dodoma amewataka wakristo nchini kuendeleza matendo mema waliyokuwa wakifanya wakati wa kipindi cha Kwaresma ili waweze kudumisha amani kupitia neno la Mungu.
Pia aliwataka Watanzania kufanya kazi kwa bidii badala ya kupoteza muda kujadili mambo yasiyo na tija.
MCHUNGAJI MALODA - ZANZIBAR
Mchungaji Maloda alilaani mauaji ya polisi wanane Kibiti na kutaka wote waliotenda unyama huo watafutwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Alisema tukio hilo ni la kusikitisha na linapaswa kulaaniwa kwa nguvu zote kwakuwa ni jambo la kuondoa uhai wa mtu na kamwe halimpendezi Mungu.
Aidha, alisema ni vyema kufuatilia matukio ya mauaji yanayotokea nchini ili kujua kitu gani kimetokea kabla hali haijawa mbaya zaidi, hasa kutokana na taarifa za mfululizo wa matukio ya utekaji, uvamizi na sasa mauaji ya askari wasio na hatia.
“Tuamke kama wanawake waliyokwenda kaburini hawakuogopa na walifuatilia ili kujua kama ni kweli Yesu alifufuka na walirejea kuuambia ulimwengu ukweli kuwa Yesu amefufuka,” alisema Mchungaji huyo, akihimiza wajibu wa kila mmoja kushirikiana na vyombo vya dola kuzuia maovu nchini.
Aliwataka Watanzania kuishi katika umoja, udugu na mshikamano kwa sababu kufanya hivyo ndiyo usalama wao utaimarika dhidi ya wahalifu ambao watajulikana kirahisi katika jamii na kudhibitiwa kabla hawajaleta madhara.
Mchungaji wa Kanisa la TAG Kariakoo - Zanzibar, Joachim Bigambwa, aliwataka Watanzania kuisherehekea kwa amani sikukuu ya Pasaka pasipo kujihusisha na vurugu.
Alizungumzia pia matukio ya mauaji na utekaji, akiwataka Watanzania wote kushiriki kadri kila mmoja kwa nafasi yake kuzuia kushamiri kwa vitendo hivyo.

ASKOFU GWAJIMA- DAR
Katika mahubiri yake, Askofu Gwajima alisema Watanzania wanapaswa kuliombea taifa ili kuliepusha na mambo mabaya, ikiwamo kuhakikisha majambazi yaliyoua askari nane wa Jeshi la polisi yanapatikana mara moja.
Askofu Gwajima alitoa kauli hiyo jana wakati akihubiri katika ibada ya Sikukuu ya Pasaka katika Kanisa hilo lililopo Ubungo jijini Dar es Salaam.
Alisema kuuawa kwa askari hao ni jambo la kuhuzunisha na baya kwa taifa kwa kuwa polisi ndiyo walinzi wa usalama wa raia na mali zao.
“Ni jambo la kuhuzunisha kuuawa askari… anapouawa askari anayelinda nyumba yako, na mali yako wewe unakosa ulinzi. Hivyo jambo hilo lazima lilaaniwe na kila mtu na tunafanya maombi waliofanya hivyo wasakwe kama kumbikumbi na wapatikane,” alisema
Askofu Gwajima alimpa pole Rais John Magufuli, Waziri wa Mambo ya Ndani na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) kwa kupatwa na tukio hilo zito.
“Tunaliombea taifa Mungu aliepushe na mambo mengine mabaya yanayoambatana na hayo ya kuuawa askari, wanapouawa hivyo askari wengine lazima watiwe woga, na wanapotiwa uwoga, majambazi yanatawala, kwa hiyo lazima tuyakemee,” alisema Askofu Gwajima.
MCHUNGAJI MKUU WA DINARI PWANI
Mkuu wa Dinari ya Pwani Jimbo la Tanga, Mchungaji Shemweta, alihimiza amani na kulaani matukio ya utekaji.

Aidha, alisema vijana wengi wanatekwa kwa sababu ya ukosefu wa maadili na hali hiyo inaweza kusababisha taifa kungia katika hali mbaya ya vurugu na machafuko.
Mchungaji huyo wa Kanisa la KKT Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Dinari ya Pwani, alisema ni vyema kila mmoja akahubiri amani na kujiepusha na vurugu.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!