Wednesday 26 April 2017

UKATILI KIJINSIA ‘MISUMARI YA MOTO’ WANAYOTWISHWA WANAWAKE

UKATILI wa kijinsia ni kitendo kinachoweza kusababisha madhara, maumivu, kulazimisha, kunyima uhuru, bila kujali vimefanyika kisiri ama kwenye kadamnasi.

Kwa kiasi kikubwa, ukatili wa kijinsia huhusishwa wanawake na watoto kwa kuwa wao ndio waathirika zaidi wa vitendo hivyo wanaoumizwa kama waliotwishwa misumari ya moto.
UKATILI UNAOZUNGUMZWA
Happiness Bagambi, Ofisa Habari wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) kwa nyakati tofauti anasema aina za ukatili wa kijinsia wa kiutamaduni na mila kandamizi. Bagambi anasema ukatili huu unahusisha ndoa za utotoni, utakasaji na kurithi wajane, ukeketaji na mauaji ya vikongwe na vipigo kwa wanawake.
Mfano wa ukatili huu, ni ule aliofanyiwa Neema Mwita maarufu kama “Mgonjwa wa Magufuli” aliyeruhusiwa kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) hivi karibuni baada ya kupata matibabu kutokana na kupata majeraha yaliyotokana na kuunguzwa na maji ya moto kifuani, shingoni na mkononi.
Neema alikuwa akipatiwa matibabu katika hospitali hiyo kwa msaada wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli baada ya kuguswa na taarifa za mgonjwa. Vyanzo mbalimbali vinautaja ukatili mwingine kuwa ni ule wa kingono unaohusisha ubakaji, kulawiti, biashara na usafirishwaji wa binadamu (wanawake na watoto) na kushikwa au kutomaswa bila ya ridhaa.
Katika moja ya mikutano ya kitaifa kuhusu ukatili uliofanyika Sinza, Dar es Salaam yalipo makao makuu ya Tamwa, Bagambi anautaja ukatili mwingine kuwa ni ule wa kiuchumi. “Ukatili wa kiuchumi unahusisha mama na watoto kunyimwa mahitaji muhimu na fedha za kujikimu, kunyimwa umiliki wa mali na kuzuiwa kufanya kazi,” anasema.
WANAOFANYA UKATILI NA WAATHIRIKA
Boniphace Benezeth, Ofisa Ustawi wa jamii wa Wilaya ya Ngorongoro anasema, ukatili wa kijinsia hufanywa na ndugu wa karibu wakiwamo baba, mama, mke, shemeji, baba mkwe, mama mkwe, shangazi, mjomba, dada, kaka, majirani na hata baadhi ya walezi kama walimu, madaktari au wauguzi, askari polisi na viongozi wa dini wasio waadilifu.
Akaongeza, “awali, suala la mama kupigwa au kufukuzwa nyumbani lilionekana ni jambo dogo na la kawaida, lakini sasa Tamwa, taasisi nyingine na hata kitendo cha kuanzishwa kwa madawati ya jinsia katika Jeshi la Polisi, kimesaidia umma kujua kuwa waathirika hao wanakuwa.”
Anayataja baadhi ya madhara ya ukatili wa kijinsia mara nyingi hutoka kwa wazazi waliopata migogoro na kusambaa hadi kuwafikia watoto.
“Kunakuwa na madhara ikiwa ni pamoja na yale ya kimwili, kusababisha vifo, watoto kukosa huduma muhimu kama chakula, elimu, huduma za afya na malezi ya wazazi. Huu sasa unakuwa ni ukatili kwa watoto japo ulikuwa ugomvi wa mke na mume,” anasema.
MCHAKATO WA KISHERIA UNACHANGIA
Mratibu Mafunzo wa Tamwa, Gladness Munuo anasema katika mkutano na wadau wa upingaji wa ukatili wa kijinsia kutoka Zanzibar na Tanzania Bara kuwa, uelewa mdogo kuhusu matakwa ya kisheria dhidi ya vitendo vya ubakaji huchangia kupotea ushahidi hali inayowafanya waathirika wengi kukosa haki zao.
Kwa mujibu wa Munuo katika kipindi cha mwaka 2014 hadi 2015 Tamwa imebaini kuwa, kesi 63 za ubakaji na ulawiti zilishindwa kutolewa hukumu au uamuzi wa Mahakama katika Jiji la Dar es Salaam na hiyo inatokana na upotoshwaji wa ushahidi wa kesi hizo.
Kimsingi, zipo sura nyingi ambazo ni sawa na taji la miiba wanalovikwa wanawake na watoto kiasi kwamba Tamwa na taasisi nyingine watetezi wa haki na usawa wa binadamu imejikita kuhakikisha kunakuwa na haki za binadamu na usawa wa kijinsia kwa wote.
Ukatili ambao umekuwa ukiwatesa wanawake na watoto kwa kiasi kikubwa ni pamoja na hasa vipigo, vitendo vya ubakaji na ndoa za utotoni zinazozidi kuwa tishio.
MCHANGO WA MADAKTARI
Katika mazungumzo, Munuo alisema Tamwa inalaani vitendo vya baadhi ya madaktari kujaza fomu za PF3 umri wa uongo na majina ya walalamikaji ambayo si ya kweli. Akasema katika ukosefu wa uadilifu, baadhi ya madaktari wamekuwa wakiandika taarifa tofauti hususan umri na hata majina ya watoto wanaoathiriwa na ukatili wa kubakwa kwa kuongeza umri wa mwathirika, ili kuwalinda wahalifu.
Munuo anasema, “Suala kama hilo linapofika kwa mwanasheria wa Serikali, huishia kutupwa nje kwa kuwa anayedaiwa kubakwa anaonekana mtoto, labda miaka 9, 10 au hata 12, lakini fomu inaonesha umri wa miaka 19.”
Akasema, “Tunawategemea na kuwaomba wanasheria wa serikali muangalie uwezekano uliopo ili kesi za ukatili wa kijinsia zichukuliwe na kuendeshwa kwa namna ya kipekee.”
Akiwa Mkuu wa Dawati la Jinsia katika Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Mrakibu wa Polisi (SP) Leah Mbunda Sindano, aliwahi kusema, ingawa kuna mwamko mkubwa wa kuripoti matukio ya ukatili wa kijinsia katika vituo vya polisi, bado tatizo lipo kwamba wengi wanaripoti ili wapate fomu za polisi (PF3) ili waathirika wa ubakaji au shambulio watibiwe kasha wamalize suala hilo kienyeji.
Uchunguzi wa makala haya umebaini kuwa, mara nyingi mfumo dume katika jamii ni kichecheo cha ukatili wa kijinsia kwa baba ndiye anayetegemewa, hivyo anapofanya ukatili, wanafamilia wanasita kumchukulia hatua za kisheria katika vyombo vya dola, familia itakosa mahitaji hivyo, wengi wanaripoti ili kupata PF3.
Anasema, “Ndiyo maana unaweza kuona wanaoripoti ni wengi, lakini kesi zinazoendelea mahakamani ni chache sana. Kingine kinachochea ukatili huo ni mila na desturi; wengine wanasema mila zetu haziruhusu kumpeleka mwanaume polisi.”
Hali hii kwa mujibu wa uchunguzi, inawafanya hata baadhi ya wanaume kufanya vitendo vya ukatili ukiwamo ubakaji kwa ndugu zao, lakini wake zao wakata kufanya siri.
Kwa kuwa Tanzania imeridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa inayopinga ukatili wa kijinsia, hapana budi itungwe sheria inayozuia aina zote za ukatili wa kijinsia ukiwemo ukatili wa kutumia nguvu, ngono, saikolojia na uchumi.
Kadhalika wajumbe hao walipendekeza kuwapo vituo vyenye huduma zote (one stop center) yaani ushauri, matibabu, PF3 na msaada wa kisheria kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia hasa ubakaji, ulawiti na unajisi.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!