ASILIMIA 97 ya Watanzania hawajui kama wana ugonjwa wa himofilia au hawajawahi kupima. Wataalamu wa afya wanasema, kuna uwezekano wa watu wengi zaidi kupoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.
Himofilia ni ugonjwa wa kurithi, ingawa asilimia 30 ya wagonjwa wameupata bila kurithi ila kutokana na mabadiliko ya vinasaba. ugonjwa huo unasababishwa na upungufu wa protini hivyo kusababisha damu damu isigande hata mtu akipata jeraha dogo.
Daktari bingwa wa magonjwa ya damu kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Stella Rwezaura, amesema jijini Dar es Salaamkuna umuhimu watu wapime ili wafahamu kama wana ugonjwa huo au la.
Ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu himofilia.
“Serikali imekuwa ikifanya kampeni kama za tohara, sawa watu wanaweza kwenda kufanyiwa lakini kuna asilimia 97 hawajui kama wana himofilia au hawana, ni bora wangekuwa wanapimwa kabla ya kufanyiwa kuepusha vifo,” amesema.
Dk. Rwezaura amesema, kati ya Watanzania 10,000 mmoja ana ugonjwa wa himofilia na kwaTanzanaia inakadiriwa kuwa watu 5,400 wana ugonjwa huo lakini waliojiandikisha kwa ajili ya matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ni 100 tu.
Dk Rwezaura alisema kuwa tatizo jingine kwa Tanzania ni upungufu wa vifaa tiba na vipimo kwani ni hospitali tatu tu ikiwemo MNH ambazo ndizo zinaweza kubainisha kama mtu ana himofilia A au B na nyingine ni Hospitali ya Bugando na KCMC.
Takwimu za Shirika la Afya duniani za mwaka 2008 zinabainisha kwamba vifo takribani milioni 30 vilitokana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Lakini pia, kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Himofilia duniani, watu takribani 400,000 wanaishi na ugonjwa huo na kati ya hao, asilimia 25 tu ndio wanapata matibabu na asilimia 75 hawapati matibabu.
Akizungumzia dalili za ugonjwa huo, Dk Rwezaura alisema moja ya dalili za ugonjwa huo ni mtu kutokwa na damu kwa muda mrefu, na mgonjwa hupata nafuu baada ya kuongezewa damu au kuchoma sindano ya chembe sahani.
Rais wa Chama cha Himofilia nchini, Richard Minja alisema, ugonjwa huo una changamoto nyingi, kwani husababisha wanaoumwa ugonjwa huo kushindwa kufanya shughuli zao za kawaida na kwamba mwisho wake ni ulemavu au kifo.
Alisema watu wengi wamekuwa wakipata ulemavu na vifo kutokana na kwamba ugonjwa huo hautambuliki sana nchini, hivyo wameamua kuchukua jukumu la kutoa elimu maeneo yote nchini.
Mkurugenzi Msaidizi wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza kutoka wizara ya Afya, Profesa Ayoub Magimba, alisema serikali itaendelea kuhakikisha kuwa huduma za matibabu ya Himofilia zinaimarika na kusogezwa karibu na wananchi.
No comments:
Post a Comment