HATIMAYE Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limeanza kufanyia kazi maagizo ya Rais John Magufuli ya kulitaka kuachana na umeme wa majenereta unaozalishwa kwa bei ya juu na kutilia mkazo umeme wa maji na gesi ambao ni wa bei nafuu ili kuwapunguzia mzigo wananchi.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad kufichua katika ripoti ya hivi karibuni kuwa kamwe Tanesco haiwezi kupata faida kwa vile inatumia gharama kubwa kununua umeme ukilinganisha na bei inayouza kwa wananchi.
CAG katika ripoti hiyo ya mwaka 2015/2016 aliyowasilisha kwa Rais Magufuli na baadaye Bungeni hivi karibuni, amesema Tanesco inanunua umeme kutoka kwa wazalishaji kwa wastani wa Sh 544.65 kwa uniti moja na kuuza kwa walaji (watumiaji) kwa wastani wa Sh 279.35. Kwa hesabu hizo za CAG ni wazi kuwa Tanesco imekuwa inapata hasara ya Sh 265 kwa kila uniti moja ya umeme inayouza.
Kutokana na agizo la Rais Magufuli na baadaye ripoti ya CAG, gazeti hili limebaini shirika hilo kuzinduka na kuanza kuchukua hatua za kuanza kutegemea maji na gesi kama vyanzo muhimu vya kuzalishia umeme wa bei nafuu. Mkakati wa wazi ni ule wa uongozi wa Tanesco kuamua kuivalia njuga kampeni iliyoasisiwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuokoa mfumo wa ikolojia katika bonde la mto Ruaha Mkuu ambao ni tegemeo kwa mabwawa muhimu ya kuzalishia umeme ya Mtera na Kidatu.
Samia hivi karibuni akiwa mkoani Iringa, alizindua Kikosi Kazi Maalumu kwa ajili ya kuokoa mfumo wa ikolojia katika bonde la mto Ruaha Mkuu ambalo lipo katika hatari ya kutoweka kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira unaoendelea kwenye bonde hilo kutokana na shughuli za kibinadamu.
Kaimu Meneja wa Mawasiliano wa Tanesco Leila Mhaji aliithibitishia HabariLeo Jumapili kuwa uongozi wa Tanesco umeamua kuitumia kampeni ya Makamu wa Rais ya kuokoa ikolojia ya Bonde la Mto Ruaha ili kuboresha mabwawa ya Mtera na Kidatu. “Hivi tunavyozungumza leo (jana) tupo Mbeya katika kamati maalumu ya Makamu wa Rais kuhusu Ikolojia ya Bonde la Mto Ruaha ambapo Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco (Dk Tito Mwinuka) ni mjumbe.
“Lengo letu ni kuhakikisha tunatumia mwanya huu kushirikiana na wadau wote muhimu ili kuhakikisha kuwa mtiririko wa maji kuelekea mabwawa yetu ya Mtera na Kidatu ambayo ni tegemeo kubwa kwa uzalishaji wa umeme unaimarika na kuwa bora.
“Tanesco tunazingatia maagizo yote yaliyotolewa kwetu katika kuhakikisha kuwa tunazalisha umeme wa maji ambao kimsingi ndio umeme wa bei nafuu zaidi na ambao utatuwezesha kuwauzia wananchi kwa bei ya chini,” alisema Mhaji.
Mhaji alisema ni wazi kuwa pamoja na kampeni hiyo kusaidia katika uhifadhi wa mazingira lakini itasaidia kwa kiwango kikubwa kukabili tatizo la upungufu wa maji katika mabwawa ya Mtera na Kidatu ambalo limekuwa linaathiri kwa kiwango kikubwa uzalishaji wa umeme wa maji na kulifanya shirika hilo kutafuta vyanzo vingine vya umeme ambavyo ni gharama.
Ushauri wa CAG Katika ushauri wake juu ya Tanesco, Profesa Assad alisema juhudi za makusudi zinatakiwa kufanyika ili kulinusuru shirika la Tanesco ambalo alisema lipo hoi kutokana na malimbikizo makubwa ya madeni. Alisema malimbikizo hayo yanatokana na shirika hilo kununua umeme kwa bei ya juu kutoka kwa watengenezaji huru wa nishati hiyo (IPPs) na watengenezaji wa dharura wa nishati hiyo (EPPs).
“Jitihada zaidi zinahitajika kuliokoa shirika katika hali liliyopo kwa kutafuta vyanzo mbalada vya umeme vyenye bei nafuu. “Tanesco inapata hasara ya Sh 265.3 kutokana na kununua umeme kwa bei ya wastani wa Sh 544.65 kutoka kwa IPPs/EPPs na kuuza kwa wastani wa Sh 279.35 kwa uniti,” alisema CAG.
Alisema kutokana kupata hasara hiyo, shirika limeendelea kuwa katika hali mbaya na kujiendesha kwa hasara, na kwamba njia pekee ya kulinusuru ni kuzalisha umeme unaotokana na maji na gesi na kuachana na wazalishaji binafsi wanaotumia mafuta.
Aliishauri serikali kutafuta fedha na kuwekeza kwenye miradi ya maji ambayo itazalisha umeme wenye bei nafuu zaidi ukilinganishwa na umeme unaotumiwa baada ya kuzalishwa na kampuni binafsi.
Alisema miongoni mwa miradi inayoweza kusaidia kuzalisha umeme wa bei nafuu ni mradi wa korongo la Stiegler`s ambao ulikuwa katika mpango mkakati wa maendeleo ya sekta ya umeme katika mwaka 2012.
Gharama kamili ya ujenzi wa mradi huo ni dola za Marekani bilioni 2.4 na mapitio ya taarifa yanaonesha kuwa mradi huo ukikamilika utakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 2,100. Mpango mkakati wa sekta ya umeme huo unaonesha kwamba mradi unatakiwa kujengwa kwa awamu tatu.
Katika awamu ya kwanza Stiegler`s I megawati 300 ungekamilika 2024, ya pili megawati 600 na ungekamilika 2026 na awamu ya tatu megawati 300 ungekamilika 2028. Alisema mradi huo ulipangwa kuendeshwa na Mamlaka ya Kuendeleza Bonde la Mto Rufiji (RUBADA), lakini katika mapitio ya taarifa wamebaini kwamba, mamlaka hiyo inakabiliwa na changamoto za kifedha hivyo haiwezi kuendeleza mradi huo
No comments:
Post a Comment