Thursday, 6 April 2017

Raha na karaha za kusoma nje ya nchi


Pamoja na jitihada za Serikali kuboresha elimu nchini, wazazi wengi wanapenda kuwapeleka watoto wao nje ya nchi kusoma wakiamini kuwa huko kuna elimu bora zaidi.



Ripoti mbalimbali za kitaaluma zinaonyesha kuwa wazazi na walezi wengi wanaamini kuwa ili mtu aweze kupata kipato kikubwa kitakachomwezesha kuishi maisha mazuri ni lazima apate elimu bora.
Hata hivyo, mwanataaluma raia wa Marekani, John Dewey ana mawazo tofauti kuhusu elimu, anasema: “Elimu siyo maandalizi ya maisha, bali elimu ni maisha yenyewe.”
Anasema kuwa mwanafunzi anaanza maisha siku ya kwanza anapoingia darasani, siyo baada ya kuhitimu masomo yake.
Katika kuhakikisha kuwa watoto wanapata elimu bora nje ya nchi, baadhi ya wazazi wamesahau kuwa kumpeleka mtoto mbali ya faida, pia zipo changamoto ambazo mwanafunzi hukutana nazo ikiwa ni pamoja na kujiingiza katika magenge ya kihalifu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Global Education Link (GEL), Abdulmalik Mollel ambaye kampuni yake imekuwa ikiwasaidia wanafunzi wanaotaka kwenda nje kusoma, anataja faida na harasa za kwenda kusoma ‘ngambo’.
Anasema wapo baadhi ya wanafunzi wanaolazimika kwenda nje kusoma kwa sababu kozi wanazozipenda hazipo nchini.
Anatoa mfano kuwa tangu kuongezeka kwa mchakato wa ugunduzi wa mafuta na gesi nchini, wanafunzi wengi wanaopenda kusomea sekta hiyo wamekuwa wakitafuta vyuo vinavyotoa kozi hizo nje ya nchi.
“Sisemi kuwa hapa nchini hakuna vyuo vinavyotoa kozi ya gesi na mafuta, lakini wanafunzi wanakwenda katika nchi ambazo zimekuwa zikifundisha kozi hizo kwa muda mrefu zaidi,” anasema.
Pia, imebainika kuwa kuna baadhi ya wanafunzi wanaokwenda kusoma nje ya nchi kukwepa gharama kubwa za kusoma katika baadhi ya vyuo hapa nchini.
Kuhusu hili anasema: “Kuna baadhi ya vyuo nchini, kusomea shahada ya sayansi ya tiba ni zaidi ya Sh10milioni, huku nchini Ukraine kuna vyuo vinatoza kati ya Sh5milioni hadi Sh7milioni kwa mwaka.
Anaongeza: “ Baadhi ya Watanzania wanakimbilia nchini China kusomea kozi hiyo, huko ada ni Sh4 milioni na hosteli ni kati ya Sh1 milioni hadi Sh2.2 milioni, hivyo jumla yake kuwa sio zaidi ya Sh6 milioni kwa mwaka.”
Sababu nyingine inayowafanya watu kwenda kusoma nje ni kutaka kupata elimu bora hasa katika baadhi ya masomo ya sayansi. Kuna wanafunzi wanaoamini kuwa elimu bora ni ile ambayo kila mwanafunzi anapata nafasi ya kutumia kifaa au mashine yake wakati wa mazoezi ya vitendo.
Mhadhiri Mwandamizi katika Shule ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Kitila Mkumbo, anasema vyuo vikuu nchini vinatoa elimu nzuri na kwamba wanaokwenda nje ya nchi wanafanya hivyo si kwa kuwa elimu inayotolewa nchini ina viwango duni.
“Vyuo vikuu vinafanya vizuri hasa vya umma, ndiyo maana wanafunzi wetu wakienda kusoma huko wanafanya vizuri katika masomo,” anasema.
Pia, anataja sababu nyingine inayowavutia wanafunzi kwenda kusoma Ulaya na Marekani kuwa ni kutaka kuboresha Kiingereza kwa kuwa hapa kwetu lugha hiyo siyo imara.

Changamoto za kusoma nje ya nchi
Baadhi ya wazazi na walezi hujuta na kushindwa kuamini kilichotokea baada ya watoto wao waliowapeleka nje ya nchi kusoma kwa gharama kubwa wakirudi nyumbani wakiwa na tabia tofauti baada ya kuangukia kwenye mikono isiyo salama.
Mollel anasema baadhi ya vyuo barani Asia vina utaratibu wa kuwaruhusu wanafunzi kuishi kwenye mabwalo, mahala wanamokutana na watu wenye tabia tofauti yakiwemo magenge ya kihalifu. Baadhi ya wanafunzi kutoka Tanzania wamejiunga na makundi hayo na kukatisha masomo.
Pia, baadhi ya wazazi hao wamepoteza fedha zao baada ya kutapeliwa na mawakala feki wanaodai wanavijua vyuo vizuri na wanaweza kuwasaidia kupata usajili kwenye vyuo hivyo.
“Kuna mawakala wa vyuo vya nje ya nchi wamekuwa wakiwalaghai wazazi na walezi kuwa watoto wao wana sifa za kwenda kusoma katika vyuo hivyo, lakini baadae wanakuja kugundua kuwa walitapeliwa,” anasema Mollel.
Anabainisha kuwa tatizo hilo limechangiwa pia na wanafunzi wanaotaka kwenda nje kusoma kozi ambazo awali walisoma masomo tofauti.
“-Mwanafunzi anataka kwenda kusoma sayansi wakati hakuwahi kusoma masomo yoyote ya kozi hiyo. Jambo hilo linawashawishi matapeli kutengeneza mazingira ya kuwahadaa watu wanaolipa ada,’’ anasema.
Iko changamoto nyingine ya wahitimu wa vyuo vya nje kutotambuliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) wanaporejea nchini.
Kimsingi sheria inatamka kuwa TCU ndiyo mamlaka ya kisheria yenye jukumu la kusimamia ubora wa viwango vya elimu na mifumo inayotumiwa na vyuo vikuu katika kukidhi viwango vya ubora wa elimu ya juu.
Ndiyo inayosimamia udhibiti na kuhakiki uhalali viwango vya kitaaluma vya tuzo za shahada na stashahada zinazotolewa na taasisi za elimu ya juu ndani na nje ya nchi.
Kwa mujibu wa TCU, tuzo hizo pia zinajumuisha shahada za heshima zinazotolewa na taasisi za elimu ya juu kwa watu waliotoa mchango mkubwa katika taaluma au ustawi wa jamii.

MWANANCHI:

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!