Monday, 24 April 2017

Mrema aja na siri ya kufichua wauaji

MWENYEKITI wa Bodi ya Parole, Augustine Mrema amemwomba Rais John Magufuli amruhusu atoe wafungwa wenye sifa ya kupata msamaha kutoka bodi hiyo ili wamsaidie kufichua majambazi wanaopora na kuua askari polisi kwani anaamini majambazi na watu wanaoendesha mauaji yakiwamo dhidi ya polisi, wengi wametokea magerezani au wana uhusiano na wafungwa walioko gerezani.


Mrema aliyasema hayo jana alipohudhuria msiba wa ndugu yake kijijini Kiraracha Marangu mkoani Kilimanjaro, aliposema ipo kampeni mbaya ya kumchafua Rais Magufuli katika utawala wake inayofanywa na watu wasioukubali utawala wa Awamu ya Tano.
“Kwa uzoefu nilionao, kuna kampeni chafu ya kumchafua Rais Magufuli ili nchi isitawalike kwamba hata majambazi wanaweza kuua askari hivyo kuna kila haja ya kuwashirikisha wafungwa katika tukio hili ili wasaidie kufichua,” alisema Mrema aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi katika Serikali ya Awamu ya Pili.
Alisema watu wabaya wasioridhika na uongozi wa Rais Magufuli wanafanya kila mbinu kumchafua, ikiwemo kufadhili vikundi vya uhalifu vinavyohatarisha amani ya nchi. Mrema alisema ili kukomesha matukio hayo, ni vema Rais akaruhusu Bodi yake iwakamate na kuwapunguza wafungwa walio gerezani hasa wale wenye makosa ya kushindwa kulipa faini ili watumike kuwafichua wanaohusika na uhalifu huo.
Alimtaka Rais kudhibiti watu wanaoleta chokochoko za maneno dhidi yake na wachukuliwe hatua kwani wameonesha dhahiri hawapendezwi na utawala wake na kwamba, anaamini kwa kiasi kikubwa kuwa wamekuwa wakifadhili matukio hayo ya kihalifu. Alimpongeza Rais Magufuli kwa kumchagua kuwa Mwenyekiti wa Bodi hiyo, kwani amejipanga kumsaidia kwa nguvu zote bila kujali maslahi binafsi.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!