Tuesday, 25 April 2017

HEROINI MIL 206/- YAWASILISHWA KORTINI

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Moshi imepokea gramu 3,406.84 za dawa za kulevya aina ya heroini za thamani ya Sh milioni 206.4, kama sehemu ya ushahidi katika kesi ya kukutwa na dawa hizo inayomkabili raia wa Nigeria, John Chibuzo.


Kielelezo hicho kilipokewa juzi mbele ya Jaji Aishaeli Sumari baada ya shahidi wa kwanza wa upande wa Jamhuri, Sajenti Hashim kuomba zipokelewe kama sehemu ya ushahidi wake. Mbali na dawa hizo, Sajenti Hashim ambaye ni mtunza vielelezo wa Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro, aliwasilisha sanduku lililotumika kubeba dawa hizo, likiwa na vitu mbalimbali zikiwemo nguo, hati ya kusafiria, simu mbili tiketi za Shirika la Ndege la Ethiopia pamoja na fedha, pia aliwasilisha kitabu cha kumbukumbu ya kuhifadhi vielelezo.
Kabla ya kuwasilisha vielelezo hivyo, Jaji Aishaeli, shahidi pamoja na maofisa wa mahakama walivaa vifaa vya kufunika pua na mdomo, kisha shahidi huyo akafungua sanduku na kutoa mzigo uliofungwa na karatasi za kaki, akaufungua na kutoa dawa hizo kuionesha mahakama. Aidha alieleza jinsi mshitakiwa alivyokuwa ameficha dawa hizo kwenye sanduku na kutoa vitu vyote vilivyokuwepo ndani na kuionesha mahakama.
Awali akiongozwa na Wakili wa Serikali, Abdallah Chavula kutoa ushahidi, Sajenti Hashim alidai kuwa Novemba 23, 2013, mshtakiwa alikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) akisafirisha dawa hizo kutoka Tanzania kwenda Roma, Italia. Alidai kuwa Novemba 24, 2013 alipokea sanduku la mshitakiwa huyo na kuanza kufanya upelelezi kwa kuandika barua kwa Mkemia Mkuu wa Serikali na Desemba 2, 2013 alimfikisha mshitakiwa mahakamani kwa ajili ya kusomewa mashitaka yake.
Alidai kuwa Januari 28, 2014, alipokea taarifa ya uchunguzi kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali iliyothibitisha kuwa dawa hizo ni aina ya heroini za uzito wa gramu 3406.84, kisha akaandika barua kwenda Tume ya Dawa za Kulevya akiambatanisha barua ya Mkemia Mkuu wa Serikali. Alidai kuwa Septemba 29, 2014 alipokea hati ya thamani kutoka Tume ya Dawa za Kulevya ikionesha thamani halisi ya dawa hizo ni Sh 206,410,400.
Katika kesi hiyo, Wakili Chavula alikuwa akisaidiana na Wakili wa Serikali Verediana Mleuza, huku mshitakiwa akitetewa na mawakili Ibrahimu Komu na Diana Solomoni. Hata hivyo, vielelezo hivyo viliwekwa chini ya uangalizi wa Jeshi la Polisi kwa kuwa mashahidi wengine katika kesi hiyo watavitumia katika ushahidi wao. Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa leo.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!