Saturday 29 April 2017

Babu atiwa mbaroni kwa kumtia mimba mjukuu wake

No automatic alt text available.

Jeshi la Polisi Jijini Mwanza linamshikilia Mzee wa miaka 66 kwa tuhuma za kumpa ujauzito mjukuu wake wa miaka 16.
- Inadaiwa kuwa amekuwa akimuingilia kinguvu tangu mwaka 2011.

Mzee Kala Machange(66) Mkazi wa Nyasaka Ilemela Jijini Mwanza, anashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kumtia ujauzito mjukuu wake wa miaka 16.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema mtoto aliyetiwa mimba ni mwanafunzi wa kidato cha pili, shule ya Sekondari Nyasaka.

Kwa mujibu wa Kamanda Msangi, mtuhumiwa huyo alikuwa akiishi na mjukuu wake huyo tangu mwaka 2011 akitokea Musoma Vijijini na kwamba alianza kumuingilia kwa nguvu na kumtisha asiseme kwa mtu na endapo atasema atamuachisha shule kisha kumrudisha kijijini , jambo lililomfanya mtoto huyo kuvumilia udhalilishaji huo kwa miaka sita.

Kwa mujibu wa Kamanda Msangi, mtoto huyo aliendelea kuvumilia hali hiyo bila kumwambia mtu yeyote hadi Aprili 25 mwaka huu walimu walipotilia shaka afya ya mwanafunzi huyo na kumpeleka hospitali.

"Baada ya uchunguzi binti aligundulika kuwa mjamzito wa miezi minne . Alipohojiwa alidai amepewa na Babu yake." Alisema Kamanda Msangi.

" Walimu walitoa taarifa polisi na askari wetu walifuatilia na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa" alisema huku akisisitiza kwamba mtuhumiwa huyo anaendelea kuhojiwa na uchunguzi unaendelea.

Kamanda Msangi aliwaonya watu wazima wenye tabia ya kuwarubuni watoto kisha kuwafanyia vitendo vya ngono kuacha tabia hiyo.


Chanzo: Tanzania Daima

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!