Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga (Kushoto-waliokaa) na Mwakilishi kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, anayeshughulikia Mfuko wa Maendeleo wa Ulaya (EDF), Goodlove Stephen (Kulia-waliokaa), wakitiliana saini Mkataba wa Msaada wa Euro milioni 6.5 kutoka Umoja wa Ulaya (EU) na Euro milioni 1.5 kutoka Serikali ya Tanzania, kusaidia Mfuko wa uendelezaji miradi ya Umeme Vijijini. Wanaoshuhudia ni viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Fedha na Mipango na REA. Hafla hiyo ilifanyika hivi karibuni Makao Makuu ya Wizara, mjini Dodoma.
Na Veronica Simba – Dodoma
Umoja wa Ulaya (EU) umetoa Euro milioni 6.5 ambazo ni sawa na takriban shilingi bilioni 15.3 za Tanzania kwa ajili ya kusaidia Mfuko wa uendelezaji miradi ya umeme vijijini. Aidha, Serikali ya Tanzania imechangia Euro milioni 1.5, sawa na takribani shilingi za Tanzania bilioni 3.5 hivyo kuwezesha kufikia jumla ya Euro milioni 8 ambazo ni zaidi ya shilingi bilioni 18 za Tanzania.
Mkataba wa msaada huo, ulisainiwa hivi karibuni baina ya mwakilishi wa EU na Serikali ya Tanzania, Makao Makuu ya Wizara ya Nishati na Madini, mjini Dodoma. Akizungumza katika hafla ya utilianaji saini mkataba huo, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani alieleza kuwa, fedha hizo zitatumika kujenga Kituo cha kupoza umeme wa kilovolti 220/33 wilayani Kilombero Mkoa wa Morogoro pamoja na miundombinu ya kusambazia umeme katika Wilaya za Kilombero na Ulanga.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (katikati), akizungumza na Ujumbe kutoka Umoja wa Ulaya (Kulia) pamoja na baadhi ya viongozi kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Fedha na Mipango na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) (Kushoto), katika hafla ya kutiliana saini Mkataba wa jumla ya Euro milioni 8, ambazo kati yake, Euro milioni 6.5 zimetolewa na EU na Euro milioni 1.5 zimetolewa na Serikali ya Tanzania, kwa ajili ya kusaidia Mfuko wa uendelezaji miradi ya Umeme Vijijini. Hafla hiyo ilifanyika hivi karibuni Makao Makuu ya Wizara, mjini Dodoma.
Naibu Waziri alifafanua kuwa, msaada huo uliotolewa ni kutoka Mfuko wa Maendeleo wa Ulaya (European Development Fund – EDF) ambao unalenga kusaidia Ukanda wa Kilimo wa Kusini wa Tanzania. “Nia hasa ni kuwezesha mazingira ya mapinduzi ya kilimo endelevu kwa Ukanda huo.”
Dk Kalemani alieleza zaidi kuwa, Mradi huo utawasaidia wananchi wanaojishughulisha na kilimo hususan katika Wilaya za Ifakara, Kilombero na Ulanga kutokana na upatikanaji wa umeme wa uhakika katika maeneo yao na hivyo kuwa kichocheo kikubwa kwa uchumi wa viwanda.
“Nawahamasisha wananchi wa maeneo hayo wajiandae kuupokea Mradi husika kwa manufaa yao na Taifa kwa ujumla,” alisisitiza.
Alisema kuwa, Mradi huo utakaochukua kipindi cha miezi 36 kukamilika, utaanzia maeneo yaliyotajwa lakini lengo ni kufikia maeneo mbalimbali nchini. Kwa upande wake, Mkuu wa Mahusiano kutoka EU, Jose Correia Nunes alisisitiza kuwa, upatikanaji wa umeme ni moja ya sifa muhimu za kuwawezesha wananchi kiuchumi. “Ni kwa sababu hiyo, Umoja wa Ulaya kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania, tunalenga kuhakikisha kuwa wananchi wanapata umeme wa uhakika na wa bei nafuu ili waweze kukabiliana na changamoto ya kuondoa umaskini.”
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (Kulia) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani), mara baada ya hafla ya kutiliana saini Mkataba wa jumla ya Euro milioni 8, ambapo Euro milioni 6.5 zimetolewa na EU na Euro milioni 1.5 zimetolewa na Serikali ya Tanzania, kwa ajili ya kusaidia Mfuko wa uendelezaji miradi ya Umeme Vijijini. Kutoka kushoto ni Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Nishati, Dkt Juliana Pallangyo na Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Madini, Profesa James Mdoe.
Naye mwakilishi kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Goodlove Stephen alisisitiza kuwa, Tanzania inao mkakati wa muda mrefu wenye lengo la kutosheleza mahitaji ya ongezeko la idadi ya watu inayokua kwa kasi ili kuiondoa nchi katika umaskini. “Inakadiriwa kuwa, usambazaji wa umeme unatakiwa kuongezeka na kufikia megawati 10,000 ili kuendana na ukuaji wa uchumi unaotakiwa kuibadilisha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Msaada huu kutoka Umoja wa Ulaya utasaidia kuharakisha mipango husika, ikiwemo lengo la kuongeza uunganishaji umeme kufikia asilimia 75 ifikapo mwaka 2025.”
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga, alibainisha kuwa Mpango-Mkakati wa miaka mitano wa REA (2016/17 – 2020/21) unalenga kuwezesha azma ya Serikali kuhakikisha vijiji 7,873 nchini, ambavyo havijapata umeme, vinapatiwa huduma hiyo kufikia mwaka 2021
No comments:
Post a Comment