Tuesday, 7 March 2017

Mzazi aomba msaada kutibu watoto 4 walemavu wa akili

MKAZI wa Frelimo mjini Iringa, Lucy Amanyisye anaomba msaada wa hali na mali kutoka kwa wasamaria wema ili watoto wake wanne wenye ulemavu, waweze kupata matibabu na mahitaji yao mengine ya msingi.


Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni mjini hapa, Amanyasye aliwataja watoto hao kuwa ni Judith Luwanda (29), Cosmas Luwanda (25), Revocatus Luwanda (17) na Rosemary Luwanda (14). Alisema watoto wake hao wana tatizo la akili ambalo halijaeleweka chanzo chake ni nini.
“Watoto wangu hawa wanne, wamesoma elimu ya msingi, lakini hawajui kusoma, kuhesabu wala kuandika chochote kile ikiwa ni pamoja na majina yao,” alisema mama huyo huku akibubujikwa na machozi.
Alisema hali ya maisha imekuwa ngumu kwa familia yake inayomhusisha pia mumewe, Mwalimu mstaafu wa Shule ya Sekondari Mkwawa ya mjini Iringa, Evod Luwanda.
Kwa mujibu wa mama huyo anayejihusisha na ujasiriamali wa kuuza dawa za kusafishia choo, mumewe hana kipato cha uhakika kwa sasa kwani alishastaafu na kutumia kiinua mgongo kuitunza familia.
Anasema kutokana na mazingira magumu ya kuwatunza watoto hao, wamejikuta wakishindwa kufanya shughuli yoyote ya maendeleo, kwani nguvu kubwa walikuwa wakiielekeza kwenye matunzo ya watoto, hali iliyoifanya familia mpaka sasa iishi kwenye nyumba ya kupanga.
Akizungumzia hali ya watoto, alisema mara nyingi wanashindwa kutofautisha vitu, akitolea mfano kwamba hawana uwezo wa kutofautisha thamani ya fedha (noti na sarafu), akisema kila fedha wanayoiona wanaiita Sh 200.
Kwa miaka 29 tangu amzae mtoto wake wa kwanza, Judith na wengine watatu baadaye, alisema maisha yake yaligeuka na kuwa ya kuwahangaikia watoto hao ili wapate matibabu ambayo pamoja na huduma za maombezi ya kiroho, hakuna mabadiliko yoyote waliyopata.
Alisema watoto hao wamekuwa wakishinda ndani, hawawezi kutumwa na wala kufanya shughuli yoyote kwa umakini unaotakiwa.
Alisema watoto hao wameifanya familia yao kuwa masikini, kwa sababu sehemu kubwa ya fedha wanazopata zinaishia kuwahudumia watoto hao ambao hata hivyo wanasikia na wanaweza kujibu baadhi ya mambo.
“Tuna maisha magumu, hata hivi unavyotuona hatuna hata kiwanja, si kwamba hatukuwa na malengo bali kipaumbele kilikuwa kwa hawa watoto…kila tulichopata kilikwenda kwenda matunzo tukiamini mambo yatakwenda sawa, lakini mpaka mzee anastaafu hakukuwa na unafuu na fedha yake imeishia huko…,” anasema mama huyo na kuongeza kuwa kipato chao kwa sasa hakitoshelezi mahitaji yao.
Watoto hao walipoombwa na mwandishi wa habari hii kila mmoja aandike jina lake kwenye karatasi walilopewa, wote walishindwa na walipooneshwa noti ya Sh 10,000 na kuulizwa mmoja mmoja thamani yake, majibu yao yalikuwa Sh 200 na Sh 500.
“Naomba serikali na Watanzania wanisaidie, bado naamini watoto wangu hawa wanaweza kufanyiwa uchunguzi mkubwa, wakapatiwa matibabu na kisha wakawa sawa na watu wengine,” alisema mama huyo.
Alisema kwa yeyote atakayeguswa na tatizo la watoto hao anaweza kuwasiliana naye kwa simu 0754 776 229 na 0754 778 975 au atume msaada wowote kupitia akaunti yake yenye jina Lucy Amanyisye Malindo, namba 010-0025911 iliyopo Benki ya Posta.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!