Wednesday, 1 March 2017

Museveni: Rais mchapakazi aliyesoma Dar

RAIS Yoweri Museveni wa Uganda anayetajwa kuwa mmoja wa marais wachapakazi Afrika, huwezi kukamilisha historia yake bila kutaja Tanzania ambako ni ‘nyumbani’ kwake.


Mbali na kusoma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Museveni pia aliishia Tanzania akiwa katika harakati za kupambana na utawala dhalimu wa Dikteta Iddi Amin Dada na baadaye Rais Milton Obote.
Anazungumza Kiswahili kwa ufasaha. Museveni alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1967 ambako alisomea Siasa na Uchumi.
Akiwa mwanafunzi wa chuo kikuu hicho, Museveni alianza kujidhihirisha kama kiongozi wa baadaye pale alipojitosa katika uanaharakati wa masuala ya siasa akipiga vita siasa za kibepari na ukoloni mamboleo.
Wakati huo, Ujamaa ulionekana kama mkombozi wa mwafrika.
Alianzisha hapo chama kilichoitwa ‘University Students’ African Revolutionary Front’, kilichokuwa na lengo la kuwaamsha wanafunzi wa vyuo vikuu kuwa tayari katika kupambana na siasa za kibeberu, yeye akiwa kiongozi wa wanaharakati hao.
Museveni aliongoza ujumbe wa wanafunzi kwenda Msumbiji kwa nia ya kujenga uhusiano wa karibu na chama cha FRELIMO ambacho wakati huo kilikuwa chama cha ukombozi, kikilenga kuwafukuza wakoloni wa Kireno ili wananchi wawe huru.
Yoweri Museveni anatajwa kuwa mwanafunzi makini na mfuasi wa karibu wa mwalimu wake, Mwanaharakati Walter Rodney, aliyekuwa akipinga mfumo kandamizi iliyokuwa ikiinyonya Afrika.
Rodney ni mwandishi wa kitabu maarufu cha ‘How Europe Underdeveloped Africa’ (Jinsi Ulaya ilivyoididimiza Afrika kimaendeleo). Mwaka 1970, Museveni alijiunga na ofisi ya Usalama wa Taifa nchini Uganda.
Wakati Idi Amin alipopindua nchi huku Rais Milton Obote akihudhuria mkutano wa viongozi wa Afrika, Adis Ababa, Ethiopia, Yoweri Museveni alikimbilia Tanzania kwa ajili ya usalama wake akiwa na wafuasi kadhaa wa Obote.
Kati ya mwaka 1972-1980 Museveni na wenzake waliokuwa ukimbizini Tanzania na wale ambao walikuwa hawamtii Idi Amin waliendelea kujiimarisha juu ya namna ya kuikomboa Uganda dhidi ya nduli na baadaye dhidi ya vita vya wenyewe kwa wenyewe ili kuijenga Uganda mpya.
Mwaka 1972 alijitenga na makundi ya wapinzani na kuanzisha kikundi chake alichokiita ‘Front for National Salivation’. Huu ni mwaka ambao pia alifunga pingu za maisha na Janet Kataha.
Kipindi cha kati ya mwaka 1981- 1986, alikitumia akiwa msituni. Wakati huo makundi mbalimbali yalikuwa yakipigana kiasi kwamba hapakuwa na amani katika nchi ya Uganda, hivyo akadhamiria kuikomboa Uganda na kurejesha amani kama ilivyo leo.
Marafiki wa karibu wa Museveni wamekuwa wakisema mkuu wao huyo akiamua jambo hafanyi mzaha. Uamuzi wake wa kurejea Uganda aliutekeleza akiwa na wafuasi wake na kikosi kilichoitwa ‘Popular Resistance Army’ na mara moja kuanza kupanga mbinu za kuuondoa madarakani utawala wa Milton Obote ambao ulikuwa ukinyooshewa vidole na nchi za nje ukidaiwa kuua watu zaidi ya 300,000.
Vikosi vya Museveni vilianza mapambano ya kumuondoa Obote kwa kuibomoa ngome yake na kisha kuungana na vikosi vya aliyekuwa rais wa zamani Yusufu Lule pamoja na kundi la Uganda Freedom Fighters kisha kuunda National Resistance Army (NRA) na National Resistance Movement (NRM). Baada ya kumwangusha Obote, mwaka 1986 Yoweri Museveni alianza kuijenga Uganda mpya kama inavyoonekana leo.
Aliandaa mpango mkakati wa kuhakikisha kuwa Uganda inakuwa na uchumi wenye nguvu chini ya utawala wake kama ifuatavyo:
• Kuhakikisha demokrasia ya kweli inajengwa
• Kuhakikisha usalama wa nchi na watu wake unalindwa
• Kurudisha umoja ambao ulisambaratika kwa muda mrefu na
• Kulinda uhuru wa nchi. Mikakati mingine ilikuwa ni kujenga uchumi kwa njia ya kujitegemea, kuinua hali na maisha ya wananchi wa Uganda, kupambana na rushwa na utumiaji mbaya wa madaraka, kuhakikisha usawa unakuwepo miongoni mwa wananchi na kujenga na kuimarisha uhusiano na nchi nyingine za Afrika.
Kutokana na mikakati mbalimbali aliyoiweka, utawala wake uliungwa mkono na nchi nzima pamoja na nchi za nje ambazo ziliimwagia misaada nchi hiyo.
Uchumi wa Uganda uliokuwa taabani, chini ya Rais Museveni ulikua kwa kasi. Hatua ya Museveni kuamua kuachana na siasa za kijamaa na kugeukia uchumi huria inatajwa kuwa moja ya vitu vilivyosaidia kukuza haraka uchumi wa Uganda.
Uamuzi wake uliungwa mkono na nchi za Magharibi, Shirika la Fedha (IMF) na Benki ya Dunia kwa kuanza kumwaga fedha za kusisimua maendeleo nchini Uganda. Uganda ilianza kurekebisha uchumi wake mwaka 1987, lengo likiwa ni kuwapa hamasa wananchi kufanya kazi, kuwekeza katika vitega uchumi kwa kuwashirikisha wawekezaji kutoka ndani na nje.
Pia serikali ya Museveni iliwapa wananchi wake uhuru wa kufanya biashara kimataifa.
Akihutubia katika moja ya mikutano yake, Rais Museveni alisema ili nchi yake iendelee kukua kiuchumi, lazima kuwe na mkakati maalumu wa kuhakikisha kuwa wananchi wa Uganda wanalindwa pamoja na mali zao na wanaruhusiwa kufanya biashara mahali popote wanapotaka.
Kutimiza hayo, Rais Museveni alihakikisha nchi yake ina demokrasia ya kweli. Mei 9, 1996, aliitisha uchaguzi mkuu wa urais ambapo wananchi walipewa fursa ya kupiga kura ya kumchagua rais wanayemtaka.
Katika uchaguzi huo, Museveni aligombea pamoja na Poul Ssemogerere wa Democratic Party na kushinda kwa asilimia 75.5 na hivyo kutawazwa kuwa Rais wa Uganda kwa mara ya pili Mei 12, 1996. Uchaguzi mwingine ulifanyika mwaka 2001.
Kipindi hiki Museveni alipambana na aliyekua mtu wake wa karibu wakati wa harakati za kuikomboa Uganda, Dk Kizza Besigye na kumshinda kupata asilimia 69 ya kura zote.
Katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2010 Museveni alipambana tena na Besigye na kumshinda kwa kupata asilimia 61 ya kura wakati Besigye akipata asilimia 35 ya kura zote zilizopigwa. Feburuari mwaka jana, 2016, Museveni alichaguliwa tena kwa kupata asilimia 61.
Kwa hakika Museveni amefanikiwa kuleta amani na utulivu uliosababisha nchi ya Uganda kukua kiuchumi. Pamoja na kwamba alichukua nchi iliyokuwa na matatizo mengi yakiwemo vita vya wenyewe kwa wenyewe, Rais Museveni ameweza kuiongoza nchi hiyo na kuwezesha uchumi wake kupaa kwa kiwango kikubwa.
Shahada za udaktari Pia kwa uongozi wake uliotukuka, amekuwa mstari wa mbele kupambana na ugonjwa wa Ukimwi na nchi yake kuwa moja ya nchi zinazoongoza barani Afrika katika kutokomeza ugonjwa huu.
Juhudi zake hizi zimemuwezesha kujipatia heshima kubwa duniani kutoka kwa viongozi wenzake pamoja na wasomi. Katika urais wake, vyuo vikuu mbalimbali vimekuwa vikiona juhudi zake na kumpa tuzo nyingi. Baadhi ya tuzo hizo ni shahada kutoka vyuo vifuatavyo:
• Humphrey School of Public Affairs (Marekani) ambacho mwaka 1994 kilimtunuku Shahada ya Uzamivu ya Sheria (Doctor of Laws).
• Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Uganda (University of Science and Technology of Uganda) ambacho mwaka 2003 kilimtunuku Shahada ya Uzamivu ya Sheria (Doctor of Laws).
• Latin University of Theology (Marekani) ambacho mwaka 2003 kilimtunuku Shahada ya Uzamivu ya Elimu ya Dini (Doctor of Divinity).
• Chuo Kikuu cha Faith (Uturuki) ambacho mwaka 2010 kilimtunuku Shahada ya Heshima (Honorary Degree).
• Chuo Kikuu cha Makerere (Uganda) ambapo mwaka 2010 kilimtunuku Shahada ya Sheria (Doctor of Laws).
• Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Tanzania) ambacho mwaka 2015 kilimtunuku Shahada ya Uzamivu ya Fasihi (Doctor of Literature).
Huyu ndiye Rais Yoweri Kaguta Museveni ambaye umahiri wake na uongozi uliotukuka umetokana na matunda ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Historia yake Museveni alizaliwa Septemba 15, 1944 huko Tungamo, Uganda. Anatokea katika kabila la Banyankole. Jina lake la ‘Museveni’ lina maana ya ‘kijana mvulana wa mtu wa saba’ hii na kwa heshima ya Kombania ya saba ya kikosi cha King’s African Rifles (KAR).
Hili lilikuwa jeshi la wakoloni wa Kiingereza ambalo Waganda wengi walijiunga nalo katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia.
Alipofika umri wa kwenda shule, alipelekwa katika Shule ya Msingi ya Kyamate nchini Uganda baada ya kufanya vizuri alichaguliwa kujiunga na masomo ya sekondari, Mbarara High School na kisha Shule ya Ntare, zote za nchini Uganda.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!