Wednesday, 15 March 2017

Muhongo: Mnaopata umeme REA msidai fidia

WANANCHI wanaoishi maeneo yanayopitishwa miundombinu ya umeme vijijini wametakiwa kutodai fidia ili wafikishiwe huduma hizo kwa maendeleo yao.


Hayo yalisemwa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo wakati wa uzinduzi wa awamu ya tatu ya mradi wa umeme vijijini chini ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA) mkoani Pwani uliofanyika Mlandizi wilayani Kibaha.
Alisema fedha zilizotengwa takribani shilingi trilioni moja kwa ajili ya mradi huo, hazitakuwa sehemu ya fidia kwa ajili ya maeneo utakapopita umeme huo.
“Bajeti iliyopangwa kutumika kwenye awamu hii (REA III) kwa nchi nzima ni mara tatu ya bajeti iliyopita; lengo ni kuhakikisha Watanzania wote wanapata huduma za umeme hasa vijijini. Fedha hizo ni za ndani hivyo lazima wananchi nao wajitolee pasipo kudai fidia,” alisema.
Alisema miradi ya REA ilipoanza mwaka 2007 wananchi waliokuwa wakitumia umeme walikuwa asilimia 2 na hadi kufika Desemba 2017 itakuwa imefikia asilimia 49.5 huku gharama zikibebwa na Serikali.
Alilitaka Shirika la Umeme (Tanesco) kutoa kipaumbele kwa Mkoa wa Pwani ili wawekezaji wapate umeme wa kutosha kutokana na mkoa huo kuwa na viwanda vingi vikihitaji umeme ambao ni injini ya maendeleo.
Akielezea kuhusu mradi huo mkoani Pwani, Mkurugenzi wa REA, Gisima Nyamo-Hanga alisema, utatekelezwa katika vijiji 55. Awamu iliyopita vilifikiwa vijiji 150.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo alisema mkoa huo unakabiliwa na tatizo la wateja kuhitaji kuunganishiwa umeme, lakini vifaa kama vile nguzo, mita na nyaya ni vichache.
Aliomba mkoa huo uongezewe nguvu ya umeme kwani wanapata megawati 38 hadi 40 huku mahitaji yakiwa ni megawati 60 kwenye vituo vidogo vya Mlandizi, Chalinze na Mkuranga.
Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete alisema tathimini ilifanyika katika baadhi ya vijiji kukiwa na mahitaji kidogo lakini sasa mahitaji yameongezeka.
Naye Mbunge wa Kibaha Vijijini, Abou Jumaa alisema baadhi ya vijiji vina changamoto ya ukosefu wa umeme, hivyo kushindwa kufanya shughuli za kimaendeleo.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!