Jeshi la Polisi limesema limeanza kufanyia kazi maagizo waliyopatiwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, kumsaka mtu aliyemtolea bastola aliyekuwa Waziriri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye.
Hayo yalisemwa jana na Msemaji wa Jeshi hilo, Advera Senso. Awali, Mwananchi lilimtafuta Mkuu wa Jeshi hilo, IGP Ernest Mangu, lakini simu yake ilipokelewa na msaidizi wake aliyemtaka mwandishi amtafute Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso ili atoe ufafanuzi kuhusu utekelezaji wa agizo la Waziri Nchemba.
Alipopigiwa simu, Senso alijibu kwa ufupi kuwa wameanza kufanyia kazi agizo la Waziri Nchemba.
“Sisi tumepokea maelezo ya waziri na tayari tumeanza kuyafanyia kazi, hilo ndilo ninaloweza kukwambia,” alisema.
Hali hiyo imekuja ikiwa ni siku moja baada ya polisi aliyevalia kiraia kumtishia bastola, Nape ambaye pia ni Mbunge wa Mtama (CCM).
Waziri Nchemba alilaani kitendo hicho na kumuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi kuchukua hatua “Mheshimiwa Nape sio jambazi, hana rekodi za uhalifu. Kitendo cha kutolewa bastola si cha Kitanzania na si cha kiaskari na sio cha Kimungu,” ameandika Mwigulu katika ukurasa wake wa facebook.
“Kama mtu ameweza kutoa bastola mbele ya kamera, nawaza mbali, ingekuwa kwenye uchochoro angefanya nini. Nimemuagiza IGP achukue hatua.
“Nahusika na usalama wa raia wote wa Tanzania. Nimemwelekeza IGP atumie picha kumsaka mtu yule aliyeinua kufanya kitu cha kihalifu kwa kofia ya uaskari. Na kama ni askari, basi sheria zinazoongoza taasisi husika zichukue mkondo wake.”
Credit - Mwananchi
No comments:
Post a Comment