WIZARA ya Afya ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema hakuna sababu ya mgonjwa wa kifua kikuu kufa kwa sababu dawa za kutibu ugonjwa huo zipo na zinatolewa bure katika hospitali zote mjini na vijijini.
Naibu Waziri wa Afya, Harusi Said Suleiman alisema hayo wakati akitoa ufafanuzi kuhusu taarifa kuwa hakuna dawa za kutibu ugonjwa wa kifua kikuu pamoja na ukoma na hivyo kuwafanya wagonjwa wa aina hiyo kuhangaikia matibabu yao.
Akifafanua, alisema dawa za kutibu magonjwa hayo zipo na zinapatikana bure na hakuna mgonjwa aliyetozwa fedha kwa ajili ya kupata dawa hizo pamoja na huduma kwa ujumla.
“Hatuna upungufu wa dawa za kutibu ugonjwa wa kifua kikuu katika hospitali zetu Unguja na Pemba. Dawa hizo zinatolewa bure kwa mujibu wa masharti ya wagonjwa wa aina hiyo duniani ikiwa ni maelekezo ya Shirika la Afya Duniani (WHO),” alisema.
Aidha, alitoa onyo na kusema mtu yeyote atakayeuziwa dawa hizo anatakiwa kutoa taarifa serikalini kwa sababu dawa hizo hazitakiwi kuhifadhiwa au kuuzwa sehemu yoyote isipokuwa katika hospitali za Serikali na kutolewa kwa utaratibu maalumu unaofahamika.
Awali, Mkurugenzi wa Tiba wa Wizara ya Afya, Fadhil Abdallah alisema bado ugonjwa wa kifua kikuu ni tishio kwa afya ya binadamu ingawa hauna kiwango kikubwa cha idadi ya vifo kwa wananchi wa Zanzibar.
Alisema takwimu za hali ya ugonjwa wa kifua kikuu Zanzibar zinaonesha katika mwaka 2012 wagonjwa 600 waligundulika, mwaka 2015 wagonjwa 6,855 na mwaka 2016 wagonjwa 723 walipatiwa matibabu baada ya kubainika kuugua ugonjwa huo.
Aidha, Abdallah ameyapongeza mashirika ya afya ya kimataifa kwa misaada yao katika kutibu ugonjwa wa kifua kikuu pamoja na usambazaji wa dawa hizo.
No comments:
Post a Comment