Wednesday, 29 March 2017

Bajeti ya serikali 2017/2018 kuwa Trillion 31.6


Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania inatarajia kuwa na bajeti ya shilingi trillion 31.6 katika mwaka Mpya wa bajeti 2017/2018.

Ambapo fedha za maendeleo zimeongezeka kutoka trillion 11.8 mwaka 2016/2017 mpaka kufikia shilingi trillion 11.9 kwa mwaka huu Mpya wa bajeti 2017/2018 ambapo ni sawa na wastani wa 38% ya bajeti yote tarajiwa.

Nini maoni yako kwa bajeti hii inyotarajiwa ukilinganisha na bajeti iliyopita .

Je maeneo yapi yanajitaji kutiliwa mkazo katika bajeti hii Mpya.

Habari zaidi.....

Serikali imewasilisha mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa na kiwango cha ukomo wa bajeti ya mwaka wa fedha 2017/18 huku ikionyesha ukomo wa kufikia shilingi trilioni 31.6 kutoka trilioni 22 za mwaka wa fedha unaoisha Juni 30, mwaka huu

Katika bajeti hiyo, fedha za maendeleo zimeongezeka kutoka trilioni 11.8 mwaka 2016/17 hadi trilioni 11.9 mwaka 2017/18 sawa asilimia 38 ya bajeti yote.

Mapendekezo hayo yamewasilishwa hii leo bungeni mjini Dodoma ikiwa ni siku chache kabla ya kuanza kwa vikao vya bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

VIPAUMBELE
Kwa mujibu wa Dk. Mpango, maeneo ya kipaumbele kwa mwaka wa fedha 2017/2018 ni pamoja na miradi ya kielelezo ya maendeleo ambayo inayolenga kufanikisha utekelezaji wa Malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 inayohusisha mradi wa Makaa ya Mawe Mchuchuma, Mchuchuma Liganga, ujenzi wa reli ya kati kutoka Dar es Salaam, Tabora hadi Kigoma yenye urefu wa Km 1,251 kwa kiwango cha standard gauge na matawi yake ya Tabora kupitia Isaka hadi Mwanza yenye urefu wa Km 379, Isaka hadi Rusumo Km 371, Kaliua kupitia Mapanda hadi Karema Km 321, Keza hadi Ruvuma Km 36 na Uvinza hadi Kelelema kuelekea Musongati yenye urefu wa Km 203.

Miradi mingine ya kielelezo ni uboreshaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), ujenzi wa mitambo ya kusindika gesi mkoani Lindi, uanzishwaji wa Kanda Maalum za Kiuchumi mkoani Tanga, Bagamoyo, Kigoma, Ruvuma, uanzishwaji wa kituo cha biashara cha Kurasini, bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Bandari ya Tanga na kusomesha vijana katika stadi za mafuta na gesi, uhandisi na huduma za afya.

Maeneo mengine ya kipaumbele ni viwanda vya kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa kukuza uchumi wa viwanda, kufungamanisha maendeleo ya uchumi na maendeleo ya watu, mazingira ya wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji, kuhamisha shughuli za Makao Makuu ya serikali Dodoma, ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi pamoja na maeneo mengine muhimu kwa ukuaji wa uchumi na ustawi wa taifa.

Kwa mujibu wa Dk. Mpango, shabaha ya uandaaji wa mpango wa bajeti ya mwaka 2017/18 unaongoza serikali kusimamia mambo ya uchumi kwa ujumla ikiwamo kuongeza kasi ya ukuaji wa pato halisi la taifa kufikia asilimia 7.5 kwa mwaka 2017, asilimia 7.9 mwaka 2018 na asilimia 8.2 mwaka 2019, kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kuhakikisha kuwa unabaki kwenye wigo wa tarakimu moja kufikia asilimia 5.0 katika kipindi cha muda wakati, kuwa na pato ghafi la taifa la Sh. trilioni 123.9 kwa mwaka 2017/18, Sh. trilioni 139.7 kwa mwaka 2018/19 na Sh. trilioni 165.4 mwaka 2019/20 pamoja na mapato ya kodi kufikia asilimia 14.6 ya pato la taifa mwaka 2017/18, asilimia 15.5 mwaka 2018/19 na asilimia 15.8 mwaka 2019/20.

MWONGOZO KUANDAA BAJETI
Mwongozo wa kuandaa mpango na bajeti ya serikali kwa mwaka 2017/2018, unawataka maofisa maduuli kuzingatia masuala muhimu wakati wa uandaaji wa mipango na bajeti za mafungu yao ili kutekeleza Sheria ya Bajeti Na. 11 ya mwaka 2015.

Baadhi ya maelekezo yaliyomo kwenye mwongozo huo ni mapato yote kuingizwa katika Mfuko Mkuu wa Serikali na hivyo kufuta utaratibu wa ‘Retention’, kutumia mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato na kudai stakabadhi kwa bidhaa na huduma zilizotolewa; ukusanyaji wa kodi ya majengo kusimamiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kutumia Taasisi za Umma katika huduma za bima, usafirishaji wa barua, mizigo na vifurushi (courier) na usimamizi wa matangazo na usafiri.

Mengine ni kuhakiki watumishi wote ili kuondokana na watumishi wanaolipwa bila kustahili, ununuzi wa bidhaa na huduma kwa pamoja/wingi (in bulk) kutoka kwa wazalishaji au watengenezaji ili kupata nafuu ya bei, kutenga bajeti na kulipa michango ya serikali katika mashirika ya kimataifa na kikanda kupitia hazina, kufanya marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma na kugharamia uendeshaji wa elimu msingi bila malipo kuanzia Januari 2016.

SURA YA BAJETI
Kwa mujibu wa Dk. Mpango, bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2017/18 inatarajiwa kuwa jumla ya Sh. trilioni 32 zitakazokusanywa na kutumika katika kipindi hicho.

Waziri huyo anaeleza kuwa mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa Sh. trilioni 20.872 sawa na asilimia 63 ya mahitaji yote. Kati ya mapato hayo, serikali inalenga kukusanya mapato ya kodi ya jumla ya Sh. trilioni 18.097 sawa na asilimia 87 ya mapato ya ndani.

Mapato yasiyo ya kodi Sh. trilioni 2.022 na mapato kutoka vyanzo vya Halmashauri yanatarajiwa kuwa Sh. bilioni 753.3.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, serikali inategemea kukopa kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 900 (Sh. Sh. trilioni 2.080 kutoka vyanzo vya nje vyenye masharti ya kibiashara na Sh. trilioni 4.434 zinazotarajiwa kupatikana kutokana na mikopo ya ndani kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za serikali zinazoiva.

Kwa mujibu wa waziri huyo, Sh. trilioni 1.859, sawa na asilimia 1.5 ya Pato la Taifa ni mikopo mipya ya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Pia washirika wa maendeleo wanatarajiwa kuchangia Sh. trilioni 3.7. Kati yake, Sh. bilioni 496.3 ni misaada na mikopo nafuu ya kibajeti (GBS), Sh. trilioni 2.821 ni misaada na mikopo kwa ajili ya miradi ya maendeleo na Sh. bilioni 382.4 ni misaada na mikopo nafuu ya mifuko ya pamoja ya kisekta.

MATUMIZI
Kwa mujibu wa Dk. Mpango, katika mwaka 2017/18, serikali inapanga kutumia jumla ya Sh. trilioni 32.946 kwa matumizi ya kawaida na maendeleo. Kati yake, Sh. trilioni 19.782 zitatengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida, ambapo Sh. trilioni 7.206 ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa serikali na taasisi za umma na Sh. trilioni 9.723 ni kwa ajili ya kulipia Deni la Taifa lililoiva.

Aidha, matumizi ya maendeleo yatakuwa Sh. trilioni 13.164, sawa na asilimia 40 ya bajeti yote, ambapo fedha za ndani ni Sh. trilioni 9.960, sawa na asilimia 76.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!