Tuesday, 21 March 2017

Asilimia 60 ya watoto wana tatizo la upungufu wa damu

TAFITI zilizofanyika nchini zinaonesha kuwa asilimia 60 ya watoto chini ya umri wa miaka mitano wana tatizo la upungufu wa damu na kwamba mkoa wa Shinyanga ndio unaoongoza kwa tatizo hilo.


Aidha, tafiti zilizofanywa kwa wanawake zinaonesha kuwa karibu nusu ya wanawake wote wana upungufu wa damu, hasa Kaskazini Pemba, ambapo asilimia 72 ya wanawake katika kisiwa hicho wana upungufu wa damu.
Daktari Bingwa wa magonjwa ya damu, Dk Clara Chamba, alisema hayo alipokuwa akizungumza na HabariLeo kuhusu tatizo la upungufu wa damu lililopo nchini.
Dk Chamba aliongeza kuwa, takwimu hizo pia zinaonesha kuwa takriban asilimia 25 ya watu duniani wana upungufu wa damu, makundi yaliyoathirika zaidi kwa upungufu wa damu ni watoto wenye umri chini ya miaka mitano na wanawake walioko kwenye umri wa kuzaa.
Kwa mujibu wa Dk Chamba, upungufu wa damu ni ishara kuwa mtu ana ugonjwa fulani ingawa sababu ni nyingi zinagawanywa katika makundi matatu ikiwemo upungufu wa damu unaotokana na kuvuja damu na upungufu wa damu unaotokana na uboho kushindwa kuzalisha damu au kuzalisha damu kwa uhafifu.
Pia, alisema kuwa upungufu wa damu unaotokana na uharibifu au kuvunjwa vunjwa seli nyekundu za damu.
“Miongoni mwa mambo yote haya yanayosababisha upungufu wa damu, upungufu wa madini ya chuma una mchango mkubwa katika upungufu wa damu. Asilimia kubwa ya watu wenye upungufu wa damu mara nyingi hukutwa na upungufu wa madini chuma...,”. “Upungufu wa madini chuma hutokana na lishe hafifu, matumizi makubwa ya madini chuma ndani ya mwili (wamama wajawazito, watoto), na kuvuja damu muda mrefu (hedhi zisizo za kawaida, vidonda vya tumbo),” alisema.
Dk Chamba alisema ili kuepuka kuwa na upungufu wa damu alishauri ni muhimu kuhakikisha unakula mlo uliokamilika, endapo mtu ana dalili zozote za upungufu wa damu anashauriwa kwenda hospitali kwa ajili ya uchunguzi.
Alisema upungufu wa damu ni hali itokanayo na seli nyekundu za damu kuwa chini ya kiwango cha kawaida. Seli hizi zina protini iitwayo hemoglobin ambayo hutumika kubeba oksijeni kutoka kwenye mapafu na kuisambaza katika viungo mbali mbali vya mwili.
Alisema katika hali hiyo, viungo vya mwili havipati oksijeni ya kutosha na husababisha muathirika kujisikia uchovu usio wa kawaida, kuishiwa pumzi, kizunguzungu, kichwa kuuma au kuongezeka kwa kasi ya mapigo ya moyo.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!