Friday 24 March 2017

AONAVYO MDAU KATIKA MABADILIKO MADOGO YA BARAZA LA MAWAZIRI TANZANIA

Image result for baraza la mawaziri 2017

Binafsi nimeshangazwa kama ambavyo watu na Taasisi mbali mbali zimeshangazwa na Mabadiliko madogo ya baraza la mawaziri yaliyotokea kwa sababu binafsi sikutarajia na ninafikiri wengi wenu pia hamkutarajia kuwa hali hiyo ingeweza kujitokeza hasa kutokana na ukweli kuwa Mheshimiwa Nape ni mtu ambaye ameonekana kuwa muhimu sana katika kuasili mchakato wa mageuzi na Mabadiliko yanayoendelea ndani ya chama cha mapinduzi na serikali yake.


Hata hivyo pamoja na kusema hayo bado naunga mkono juhudi za serikali katika vita dhidi ya madawa ya kulevya na hasa hatua za uthubutu wa kuanzisha vita hiyo zilizochukuliwa na mheshimiwa Paul Makonda na pengine labda natofautiana naye kidogo katika njia anazopitia.Aidha suala linalohusiana na vyeti feki ni kama nilivyosema katika post yangu iliyopita kuwa suala hili ili malumbano yaishe na lihitimishwe walalamikaji ni budi wakaenda mahakamani ili mahakama ilitolee uwamuzi.Sijui kigugumizi ni cha nini?.Suala hili lingeisha haya yote yangeepukika.maana ndilo chanzo cha hili la sasa.
Pamoja na kuziunga mkono juhudi hizo pia napenda kusema nisieleweke kuwa naunga mkono kitendo cha uvamizi uliofanywa na mheshimiwa Paul Makonda dhidi ya kituo cha television na redio cha Clouds.Kimsingi sikuona sababu ya kuvamia ili hali mama muhusika aliyelalamika kuhusu Askofu Gwajima yupo.
Kitu ambacho kinachojibainisha katika matatizo yaliyojitokeza nafikiri ni muonekano wa dhahiri wa mahusiano yasiyo mazuri baina ya viongozi husika ambayo nafikiri ndio yaliyosababisha wao kutoshauriana juu ya namna gani bora ya kuchukua hatua dhidi ya masuala hayo.Nina imani kuwa kama mheshimiwa Paul Makonda angemshirikisha vyema Waziri Nape kama waziri mwenye dhamana na vyombo vya habari na waziri Mwigulu Nchemba ambaye ni Waziri Mwenye dhamana na Wizara ya mambo ya ndani pengine wangepata njia mbadala katika kushughulikia tatizo la video ya Askofu Gwajima na hali kama hii ingeepukika.Hali hii inasababisha viongozi wanaohusika katika kutoa maamuzi ya utekelezaji wa mambo mbali mbali muhimu ya nchi kuonekana kama wakurupukaji tu.
Hatua zilizochukuliwa na chama cha mapinduzi hivi karibuni cha kuwafukuza baadhi ya makada walionekana kama wakorofi,wanafiki na wasaliti huku baadhi wakionywa kwa otovu wa nidhamu ilitoa ishara njema na matumaini mapya kwa Wanachama na Watanzania kwa ujumla na kuwa mfano wa kuigwa na vyama vingine. Lakini kwa haya yanayoendelea yanafifisha ishara na matumaini hayo na ni linaonekana sasa kama doa ambalo lingeweza kuepukwa kama ushirikiano ungezingatiwa.
Viongozi wote ni kama timu kwa kuwa lengo ni moja hivyo ni budi kushirikiana.kama ushirikiano na mashauriano juu ya utelezaji wa mambo mbali mbali haupo ni dhahiri kutakuwa na migongano na hivyo kuzua tafrani kama hii. Ni budi viongozi kupendana na kuheshimiana ili kujenga nidhamu ambayo italiwezesha Taifa kufikia malengo ya kimaendeleo.
Tatizo jingine ni masuala ya mifumo ya kimamlaka ambayo inatoa Mamlaka kwa viongozi wa kisiasa na watendaji kama si kutokuweka mipaka bayana au la kutokueleweka vizuri kwa viongozi wahusika.
Kuhusu mheshimiwa Nape Nnauye kwa upande wangu sijaona kosa lake kwa kuwa alichukua hatua kama waziri mwenye dhamana ingawa hatua zake zimeeleweka vibaya na hivyo kupelekea mabadiliko ya baraza la mawaziri kutokea.
Natoa ushauri kuwa ujengwe Utamaduni kwa viongozi kushirikiana na kushauriana katika kutoa maamuzi katika masuala ambayo yana mwingiliano wa Mamlaka kisekta.
Aidha mifumo ya kimamlaka kwa viongozi itizamwe upya ili kushabihi mazingira ya sasa na pia yanayozingatia sekta ambazo zinaingiliana katika Mamlaka mbali mbali za kisiasa na utendaji.
Nampongeza mheshimiwa Nape Nnauye kwa ushujaa wake kwa kukubali kilichotokea na kwamba na nafurahi kusikia kuwa binafsi yake hana kinyongo na Rais.Huyu ni muungwana na ameonyesha ukomavu kisiasa.
Na la mwisho nawasihi tena wanahabari na wanaotumia mitandao hebu tujikite katika mambo mengine yanayohusu maendeleo badala ya kushabikia na kukuza masuala ya kisiasa yanayojitokeza ambayo kwa namna moja yanachangia kuzalisha matatizo mengine.Kushabikia nafikiri kunasababisha mihemuko kwa viongozi ambao mihemuko inawasababishia kutoa maamuzi ambayo hutafsiriwa baadae kuwa ni ya kukurupuka.
Na kwa wale ambao wanaona kuna jambo ambalo wanaliona linahitaji haki walipeleke mahakamani Kwani vyombo vya habari havihusiki katika kutoa hukumu dhidi ya watuhumiwa.Mfano kuhusu suala la Gwajima kutuhumiwa kuzaa na yule mama na video kuzagaa mitandaoni.Yule mama si yupo si angeenda mahakamani ili haki itendeke?Jamani tunatia mchanga kitumbua.


Kennedy Ernest Mchomvu-Kirashy Jr.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!