Monday, 27 February 2017

WATU 10 WAFA WAKITOKA SOKONI

Image result for SOKONI
AJALI mbili tofauti zilizotokea mwishoni mwa wiki zimesababisha vifo vya watu 14, wakiwamo wachimbaji wawili wadogo maarufu wanaApolo wa madini ya tanzanite yaliyoko Mererani mkoani Manyara ambao wamekufa maji ndani ya mgodi wilayani Simanjiro.


Wakati wanaApolo hao wakifa maji ndani ya mgodi, mkoani Tanga watu 12 wamekufa, 10 papo hapo wakati wakirejea makwao kutoka sokoni katika mji wa Kitivo Jimbo la Mlalo wilayani Lushoto juzi.
Katika ajali ya Mererani, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi (ACP), Francis Massawe alisema kwa njia ya simu ya kiganjani kwamba ilitokea juzi kwenye mgodi unaomilikiwa na mfanyabiashara maarufu jijini Arusha, Lucas Roika uliopo eneo la kitalu B maarufu kwa jina la Opec.
Kamanda Massawe aliwataja waliokufa kuwa ni Amiri Matatizo (24) ambaye alikuwa mkazi wa Kijiji cha Makiba wilayani Arumeru mkoani Arusha na Mahmoud Ramadhani (27) mkazi wa kitongoji cha Kazamoyo, Kata ya Endiamtu wilayani Simanjiro.
Alisema chanzo cha vifo ni ajali iliyotokea mgodini wakati wachimbaji hao wawili wakiwa na wenzao wanane wakiendelea na kazi ya kuchoronga mgodini ghafla kulitokea maji yenye kasi kubwa kutoka kwenye mwamba na kuwaua.
“Wengine walifanikiwa kujiokoa ila hao wachimbaji wawili walifariki dunia wakati wakiendelea kujiokoa kwa kukimbia ili wasikutwe na maji hayo yaliyotokea kwenye mgodi huo,” alieleza Kamanda Massawe.
Alisema wachimbaji hao wawili, walifariki dunia baada ya kushindwa kujiokoa, ila hao wenzao walijiokoa na kisha wakapanda juu ya mgodi, wakatoa taarifa kwa viongozi wao ambao nao walitoa taarifa kwenye Kituo cha Polisi Mererani juu ya tatizo hilo.
Alisema miili ya marehemu hao imehifadhiwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru, kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi kabla ya maziko.
Alisema Jeshi la Polisi na madaktari wa hospitali hiyo wanaendelea na uchunguzi wa vifo hivyo vilivyotokea na pindi wakishaukamilisha marehemu hao watazikwa.
Mkoani Tanga, ajali iliyoua watu 10 papo hapo na wengine wawili hospitalini, ilitokea Ijumaa jioni wakati gari ndogo aina ya Canter ilipopinduka na kusababisha vifo vya watu hao waliokuwa wakitoka sokoni Kitivo katika Jimbo la Mlalo kwenda mjini Lushoto.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa ajali hiyo, watu 10 walikufa papo hapo na wengine wawili ambao hali zao zilikuwa mbaya, walifariki dunia wakiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Lushoto.
Imeandikwa na John Mhala (Arusha) na Anna Makange (Tanga).

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!