Mtoto mwenye ulemavu wa viungo, Abubakar Amir (12) amekuwa na kilio cha muda mrefu cha kwenda shule ili kupata elimu, kama ilivyo kwa watoto wengine wasio na matatizo ya kimaumbile au kiakili.
Hata hivyo, kilio chake hakijapata mtu wa kukituliza kwa kuwa mama yake mzazi ambaye ndiye anayeishi naye ameshindwa kumpeleka shule kutokana na kutokuwa na uwezo wa kifedha, huku baba yake mzazi, Amir Habib anadaiwa hana mpango wa kukidhi kiu ya mtoto huyo ya kupata elimu.
Abubakar anakabiliwa na tatizo la mwili kukakamaa, huku viungo vyake vikiwa havina nguvu hivyo kushindwa kusimama, kushika kitu wala kukaa mwenyewe. Amekuwa ni mtu wa kulala muda wote. Pia, hawezi kutamka vizuri baadhi ya maneno.
Mbali na hayo, mtoto huyo ana tatizo la ugonjwa wa ngiri ambao humsababishia maumivu makali.
Mama yake Abubakar, Sophia Rashid mkazi wa Segerea wilayani Ilala Mkoa wa Dar es Salaam anasema kumekuwa na taarifa za kupingana kutoka kwa madaktari; wapo wanaosema ana matatizo kwenye ubongo na wengine wakidai hana tatizo hilo.
Kutoka na matatizo yanayomkabili mtoto huyo, baba yake mzazi anadaiwa kupuuza kilio cha mtoto huyo cha kupata elimu kwa madai kwamba kulingana na hali yake hataweza chochote, hivyo hakuna haja ya kumpeleka shule.
Hata hivyo, mama na mwanaye wanapinga madai ya baba. Sophia anasema mbali na kuwa na matatizo kidogo katika kuzungumza, ana ufahamu mzuri na uwezo wa kuelewa akifundishwa.
Kutokana na kuzidiwa na kilio cha mwanaye, Sophia anaomba msaada kutoka kwa yeyote atakayeguswa amsaidie mtoto huyo kutimiza ndoto yake ya kupata elimu sawa na watoto wengine.
Sophia anabainisha kuwa msaada anaohitaji ni wa chombo cha usafiri, hasa pikipiki ya magurudumu matatu maarufu bajaji itakayomsaidia kumpeleka shuleni na kumrudisha nyumbani.
Akizungumza na Mwananchi kwa simu, baba wa mtoto huyo, Habib anasema hajakataa kumsomesha mtoto huyo. Anadai hajawahi kuelezwa kuhusu suala hilo, licha ya kwamba wanawasiliana na mama yake.
Habib anasema yuko tayari kumsomesha mwanaye isipokuwa tatizo ni kukosa fedha. “Kwa suala la shule kutokana na jinsi alivyo ni lazima awepo mtu wa kuwa karibu naye, hivyo hapo kwenye gharama ndiyo matatizo.
“Sina uwezo wa kununua bajaji ambayo inagharimu takriban Sh7.5 milioni, kiasi hicho ni kikubwa kwa maisha yangu ya kubangaiza. Hata fedha ya matumizi wakati mwingine huwa namwambia mama yake asubiri kidogo na huwa ananielewa,” anasema.
Habib pia anasema kwa hali ya mtoto wake hadhani kama anaweza kusoma. “Kwa hali ilivyo sidhani kama kuna mwelekeo kwa sababu hata kuongea kwake ni tatizo,” anasema.
Abubakar alonga
Mbali na maelezo ya mama, Mwananchi lilifanya mahojiano na Abubakar ambaye licha ya baadhi ya maneno kushindwa kuyatamka kwa ufasaha, lakini yanaeleweka na ana ufahamu mzuri kuhusu mambo mbalimbali. Kwa mfano, aliweza kutamka herufi a, e, i, o, u.
Ingawa viungo vyake vimekakamaa na havina nguvu ya kushika kitu, mtoto huyo anasema atakuwa anaandika kwa kutumia mdomo, kauli inayodhihirisha kiu yake ya kupata elimu.
Uwezo wa kifedha
Sophia anasema mzazi mwenzake huyo anayeishi Kitunda ana uwezo mzuri kifedha kutokana na shughuli zake za biashara.
Anasema kila anapomweleza suala la kumpeleka mtoto shule amekuwa akikataa kwa madai kuwa hataweza kujifunza.
“Mwanangu anapenda shule, hivyo naomba Watanzania wenzangu wanisaidie angalau nipate bajaji itakayoniwezesha kumpeleka shule naye apate elimu,” anasema Sophia.
Tofauti na maelezo ya baba wa mtoto huyo kuwa hajawahi kuelezwa kuhusu elimu ya Abubakar, mtoto huyo anasema huwa anamweleza kwamba anataka kwenda shuleni.
Mama yake anasema kila anapopata fursa ya kuwasiliana na baba yake kwa simu, Abubakar amekuwa akimweleza anataka kusoma.
Anasema Habib hafiki nyumbani kwake Segerea kuwatembelea kwa kuwa alishakata mguu tangu mtoto huyo akiwa na miaka minne.
Kutokana na hilo, anasema aliwasilisha malalamiko Idara ya Ustawi wa Jamii ambao walimuamuru Habib kumpatia fedha za matumizi ya mtoto Sh8,000 kila wiki au Sh25,000 kila mwezi.
Anasema ingawa mzazi mwenzake amekuwa akitoa fedha hizo na wakati mwingine baada ya kukumbushwa mara kadhaa, bado ni kiasi kidogo ambacho hakitoshelezi mahitaji kulingana na hali halisi ya maisha.
Licha ya mzazi mwenzake kujitenga na hatimaye kukata mguu kabisa kufika nyumbani, Sophia anasema kuwa maisha yake hayakuwa mabaya sana kwani aliweza kuendelea na biashara zake ndogo za kuuza nyanya sokoni Kariakioo, kwa kuwa mtoto huyo mgonjwa alikuwa na mtu wa kumwangalia.
Akizungumzia suala hilo, Habib anasema ni kweli lilifikishwa Ustawi wa Jamii kutokana na mzazi mwenzake kushawishiwa kufanya hivyo.
Mbali ya mzazi mwenzake kujitenga na kukata mguu kufika nyumbani kwake, Sophia anasema awali alimudu maisha kwa kuwa alijishughulisha na biashara ya nyanya sokoni Kariakoo.
Anasema aliweza kufanya hivyo kwa kuwa alikuwa na mtu wa kumwachia mtoto wake, ambaye alihakikisha anampatia mahitaji yote muhimu.
Mama huyo anasema alikuwa akimwacha nyumbani na kaka yake (mtoto wake mwingine) ambaye sasa ameondoka nyumbani na kwenda kujitafutia maisha.
“Kwa hiyo nimebaki peke yangu na mwanangu. Kwa hali aliyonayo wakati mwingine nashindwa hata kwenda kwenye biashara zangu za kuuza nyanya,” anasema na kuongeza:
“Lakini ninapoishiwa fedha nalazimika kumwacha peke yake, namfungia ndani ya nyumba namwashia runinga nakwenda kutafuta riziki. Hata hivyo, ninapokuwa huko huwa sina amani maana kila mara huwa natamani kumuona.”
Anasema iwapo atapata msaada wa bajaji, licha ya kuwa itamrahisishia usafiri wa kumpeleka shuleni mwanaye, pia itakuwa ni chanzo cha mapato kwa kuwa ataikodisha kwa ajili ya biashara ili kupata fedha za kujikimu kimaisha.
Historia ya matatizo ya Abubakar
Akizungumzia historia ya matatizo ya mtoto wake, Sophia anasema yalianza tangu siku alipozaliwa, Juni 24, 2004, katika Hospitali ya Amana.
Anasema licha ya kwamba alikuwa na afya nzuri, hakulia alipozaliwa na alikuwa amenyooka tu.
Mama huyo anasema aliwekwa kwenye mashine na baadaye aliweza kupumua na kupelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambako alipatiwa matibabu.
“Baada ya wiki mbili tuliruhusiwa kurudi nyumbani na mtoto aliendelea vizuri, lakini baada ya miezi mitatu alianza kutapika na alipatwa ugonjwa kama vile degedege,” anasema Sophia.
Anasema alipotimiza miezi sita, alikuwa bado hajaweza kukaa na alionekana kama bado ni mtoto mchanga.
Kwa mujibu wa mama huyo, walipompeleka Muhimbili walielezwa kuwa ana tatizo kwenye ubongo ambalo ndilo lilisababisha asilie alipozaliwa.
“Walitushauri aendelee na mazoezi ya viungo, lakini baadaye alipofanyiwa vipimo wakasema hakuna tatizo lolote kwenye ubongo,” anasema na kuongeza:
“Daktari mwingine aliyeandika vipimo vya ‘ultra sound’ alisema kuna tatizo dogo kwenye ubongo hivyo tukapewa dawa.”
Sophia anasema waliendelea na matibabu huku akibadilishiwa vidonge lakini hali ya mtoto wake haikuwa na mabadiliko hadi sasa.
Sophia anaomba kwa yeyote atakayeguswa na tatizo la mtoto wake na anapenda kutoa msaada awasiliane naye kwa namba ya simu 0719 826 203.
No comments:
Post a Comment