Watu wanne wamefariki dunia na wengine 15 kujeruhiwa baada ya basi la kampuni ya Taqwa lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Lubumbashi nchini Congo kugongana uso kwa uso na lori aina ya fuso na kisha kuparamia lori lingine la mizigo wilayani Mbarali.
Ajali hiyo imetokea katika eneo la Kongoro Mswiswi wilayani Mbarali wakati lori aina ya fuso likiwa na shehena ya ndizi na likitokea wilayani Rungwe kwenda jijini Dar es Salaam, kujaribu kulipita lori lingine aina ya Scania na ndipo likagongana uso kwa uso na basi la kampuni ya Taqwa lenye namba za usajili T 321 DAK lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Lubumbashi nchini Kongo DRC.
Muuguzi wa zamu katika hospitali ya rufaa ya Mbeya, Kizito Ally Belinado amethibitisha kupokea miili miwili ya watu waliopoteza maisha katika eneo la ajali pamoja na majeruhi 15, lakini akasema majeruhi wawili wamepoteza maisha wakati wakipewa matibabu hospitalini hapo.
Taarifa ambayo imetolewa na jeshi la polisi kwa vyombo vya habari kupitia kwa kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya, Emmanuel Lukula inasema kuwa uchunguzi wa chanzo cha ajali hiyo unaendelea.
No comments:
Post a Comment