Friday, 6 January 2017

WAFUKUA KABURI LA ALBINO ALIYEKUFA MWAKA 2008!

Yela Pambo, mmoja wa majahili waliokuwa wakichimbua kaburi ambaye aliuawa na wananchi wenye hasira kali. Wananchi walimkuta akiwa ndani ya kaburi na kumshushia kipigo hadi mauti.
Na Daniel Mbega

JANUARI 3, 2017 majira ya saa 3:00 usiku katika Kitongoji cha Songambele, Kijiji cha Mumba, Kata ya Masoko katika Wilaya ya Mbeya Vijijini mkoani Mbeya, wakati wananchi wengine wakiwa wameanza kupitiwa na usingizi, kundi la watu watano lilikuwa makaburini.
Hawakuwa wakizika maiti, bali watu hao walikuwa na kazi kubwa ya kuchimbua kaburi alimozikwa Bi. Sisala Simwali, dada aliyekuwa na ulemavu wa ngozi (albino).

Marehemu Sisala alifariki dunia Februari 28, 2008 baada ya kuugua na kuzikwa Februari 29, 2008 katika makaburi ya familia.
Kishindo cha kuchimbua kaburi kikawaamsha wananchi, ambao licha ya kupiga simu polisi katika Wilaya ya Kipolisi ya Mbalizi, walianza kupambana na watu hao na wakafanikiwa kuwakamata wawili huku mmoja akiuawa na wananchi wenye hasira na wengine kukimbia.
Lengo la watu hao, kwa mujibu wa mahojiano ya awali kati ya polisi na watuhumiwa, lilikuwa kupata mifupa ya albino ambayo walikuwa wameelekezwa na mganga wa jadi kwamba wakiipeleka basi watatengenezewa dawa ya utajiri.
Tukio hilo ni la kwanza kwa mwaka 2017 likihusisha matukio ya albino ambayo kwa miaka kadhaa sasa yametamalaki nchini Tanzania na kuwafanya watu wenye albinism kuishi kwa mashaka katika nchi yao wenyewe.
Na limeleta hofu kubwa kwa jamii kuona kwamba badala ya kuwateka, kuwakata viungo na hata kuwaua albino, sasa majahili wameanza kuyasaka makaburi walimozikwa albino na kuyafukua ili wachukue mifupa na kupeleka kwa waganga kwa imani za kishirikina.
Itakumbukwa kwamba, mpaka sasa mtoto Pendo Emmanuel Nundi (6) wa Kijiji cha Ndamhi wilayani Kwimba mkoani Mwanza hajapatikana tangu alipotekwa nyara Desemba 27, 2014.
Kilio cha Chama cha Albino Tanzania (TAS) kinachotolewa kila siku kinadhihirisha kwamba tatizo la usalama wa albino nchini Tanzania ni sugu na limeibuka tena baada ya kupoa kwa muda.
Zamani zile za giza tukiwa tunatoka kupata Uhuru, watu walikuwa wakihangaika kutafuta mbuzi, kondoo ama ng’ombe ambao ama wameibwa au wameliwa na wanyama wakali, lakini kwa zama hizi kitendo cha binadamu kutoweka kwa sababu tu ya ulemavu alionao kinaonyesha bayana hali ya usalama si shwari.
Kwa takriban miaka 10 matukio ya kutoweka ama kushambuliwa kwa albino yamekuwa yakiripotiwa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, lakini sasa yamevuka mipaka na kuenea nchi nzima ambapo kwa Mkuranga tukio la Said ni la pili katika kipindi kisichozidi miezi mitano.
Itakumbukwa kwamba, mwezi Oktoba, 2015, siku chache kabla ya uchaguzi mkuu, Mohammed Said (35), mkazi wa Mkuranga, alivamiwa na watu wasiojulikana na kushambuliwa kwa kumkata panga kichwani.
Hali ya kuongezeka kwa matukio hayo ndiyo inawafanya wananchi wahoji kwamba zile jitihada zilizoonyeshwa na Jeshi la Polisi pamoja na vyombo vingine vya usalama kwa kipindi cha takriban miezi nane mwaka 2015 zimepotelea wapi?
Watanzania wanakumbuka matukio takriban manne yanayohusisha albino, ambapo polisi wakishirikiana na vyombo vingine vya usalama, walifanikiwa kupambana na kuwatia mbaroni baadhi ya watuhumiwa, huku pia wakikamata viungo vya albino.
Tukio la mtoto Yohana Bahati (1) wa Kitongoji cha Ilyamchele, Buseresere wilayani Chato lililotokea Februari 2015 lilivuta hisia za watu wengi, ikiwemo jumuiya ya kimataifa, baada ya majahili kuvamia nyumbani kwa Bahati Songoloka na kumkata mapanga mama wa mtoto kabla ya kumnyang’anya na kutoweka naye.
Jitihada za vyombo vya usalama zikasaidia kupatikana kwa kiwiliwili cha mtoto huyo kikiwa kimefukiwa shambani, lakini tayari majahili hao wakiwa wameondoka na mikono na miguu, viungo ambavyo mpaka leo bado havijapatikana ingawa baadhi ya watuhumiwa wametiwa mbaroni.
Mara baada ya tukio hilo, likafuata tukio la mtoto Baraka Cosmas (4) wa Kijiji cha Kikonde wilayani Sumbawanga ambaye alikatwa kitanga cha mkono wa kulia, lakini jitihada za wanausalama zikafanikisha, siyo tu kuwakamata watuhumiwa wote akiwemo tajiri aliyetoa tenda, bali hata kiganja chenyewe ambacho inaelezwa kwamba tajiri huyo alikihifadhi nyumbani kwake.
Tukio la kukamatwa kwa Mwalimu wa shule ya msingi huko Kahama mkoani Shinyanga, akiwa na mifupa inayodhaniwa kuwa ya binadamu akiambatana na waganga wa jadi nalo lilivuta hisia kubwa na likafanikiwa kufichua mambo mengi ikiwemo mitandao ya mauaji dhidi ya watu wenye albinism.
Taarifa zinaeleza kwamba, kazi kubwa ambayo inastahili pongezi kwa jeshi hilo ni ile ya kuubomoa ‘mnada’ wa albino mkoani Tabora hasa baada ya kumkamata mtu mmoja akiwa katika harakati za kumuuza binti mwenye albinism wilayani Nzega.
Kukamatwa kwa Masanja Mwinamila (44), mkazi wa Kitongoji cha Kona Nne, Kijiji cha Ugembe II, Kata ya Mwakashanhala, Tarafa ya Puge wilayani Nzega katika Mkoa wa Tabora akitaka kumuuza hai binti wa dada yake kwa mamilioni ya fedha kunadhihirisha kwamba matukio mengi ya kuuawa au kujeruhiwa kwa watu wenye albinism yanapangwa na kufanikishwa na wanandugu wenyewe kwa sababu ya mawazo potofu ya kutafuta utajiri kwa njia za mkato.
Tukio hilo lilitokea baada ya wanausalama kuwakamata watuhumiwa sita Mei 21, 2015 huko Kahama wakiwa katika harakati za kuuza mifupa inayodhaniwa kuwa ni ya watu wenye albinism kwa mamilioni ya fedha.
Kama alivyoeleza Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, ACP. Juma Bwire, mtuhumiwa Masanja Mwinamila alithubutu kwenda kumnyakua mtoto huyo Margret Hamisi (6) majira ya saa 3 usiku na kukimbia naye gizani akiwa na lengo la kumuuza ajipatie utajiri.
Lakini habari kutoka eneo la tukio zinaeleza kwamba, haikuwa kazi rahisi kwa wanausalama kumwokoa binti huyo akiwa hai na kumtia mbaroni mtuhumiwa, kwani walilazimika kujifanya ‘wanunuzi’ ili kuweka mtego wa kumkamata mtuhumiwa na kumwokoa mateka.
Taarifa za uchunguzi zinaeleza kwamba, mtuhumiwa huyo alianza mchakato wa kutafuta ‘soko’ la kumuuza mtoto wa dada yake mapema mwezi Juni 2015, lakini wasamaria wema wakawaarifu wanausalama kuhusu kinachotaka kutokea katika eneo hilo.
Ilibidi maofisa wawili wa usalama wapangiwe kazi ambapo mmoja alijifanya mnunuzi na mwingine mganga wa jadi anayeambatana na ‘tajiri’ huyo feki ambao walikutanishwa na mtuhumiwa huyo aliyewaeleza kwamba ‘dili la albino lipo’.
Bi. Joyce Mwandu Nkimbui (34), ambaye ni mama wa Margret, anasema siku tatu mfululizo kabla ya tukio, mtuhumiwa huyo ambaye ni kaka yake anayeishi jirani na hapo alikuwa akija asubuhi na jioni akijifanya kuja kusalimia na wakati mwingine hata kupikiwa chakula.
Hata hivyo, alishangaa kukuta kwamba ndiye aliyevamia nyumbani kwao usiku wa Juni 15, 2015 na kumwamuru asikimbie kabla yeye hajaingia ndani na kumkwapua mtoto.
“Walikuja usiku, sijui walikuwa wangapi, lakini wakanilazimisha ‘wewe mama tulia’, nikaogopa na kukimbilia kwenye majani, nikaanguka kwa sababu sioni vizuri usiku, nikakutana na mwenyekiti wa kitongoji, ambaye tulikwenda naye nyumbani na kukuta tayari mtoto hayupo,” Joyce alisema kwa masikitiko.
Tayari Masanja alikwishahukumiwa kifungo cha miaka 10 jela tangu Juni 19, 2015 baada ya kukiri kutenda kosa la kuteka nyara mtoto mwenye albinism kwa lengo la kutaka kwenda kumuuza.
Wakati tukio hilo linatokea, tayari watu sita walikuwa wamefikishwa mahakamani Juni 3, 2015 na wengine watatu wakisubiri kuunganishwa katika kesi mbili za kujaribu kuua kwa kumkata mkono Bi. Mungu Masaga Gedi, mkazi wa Kitongoji cha Mkuyuni, Kijiji cha Buhekela, Kata ya Igoweko wilayani Igunga, na linguine la kumkata mkono mtoto Nkamba Ezekiel kwenye Kijiji cha Mwisole, Kata ya Lutende, wilayani Uyui.
Kama jeshi hilo lilifanikiwa walau kufuatilia na kukamata watuhumiwa katika kadhia hizo zilizotajwa, ni wakati sasa wa kuhoji nini kilichotokea hata ikawa wameshindwa kupambana na matukio hayo.
Yawezekana wako kazini, lakini kazi yenyewe ina ufanisi kiasi gani ikiwa kila siku kuna matukio mapya? Ni ufinyu wa bajeti au kujisahau? Ni kupuuza janga hilo ama kusubiri matukio yatokee ndipo waanze kukimbizana?
Kuna kila sababu, tena ya msingi kabisa, ya kuhakikisha serikali kupitia vyombo vyake vya usalama, inashughulikia masuala ya mauaji ya albino, ambayo yanakwenda sambamba na mauaji ya vikongwe, ili kurudisha amani ya wananchi badala ya kuzidi hofu na mashaka.
Kama serikali iliona iko salama, basi ni wakati wa kuongeza fungu katika kazi maalum kama hizi, ikibidi kuwashirikisha na albino wenyewe katika mapambano hayo katika msingi wa kujenga uwazi na uwajibikaji.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!