WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali itaanza kusambaza kiasi cha tani milioni 1.5 za chakula zilizobaki msimu uliopita katika maeneo yenye uhitaji mkubwa ili kupunguza kasi ya ongezeko la bei ya vyakula nchini.
Waziri Mkuu aliwaambia waandishi wa habari jana mjini Dodoma kwamba katika msimu uliopita, kulikuwa na zaidi ya tani milioni tatu na hivyo baada ya wabunge kushinikiza serikali kuruhusu kuuza vyakula nje, kiasi cha tani milioni 1.5 kiliuzwa na hivyo kubakiwa na tani milioni 1.5.
Aidha, imefahamika kuwa hadi kufikia Januari 12, mwaka huu, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) walikuwa na akiba ya tani 88,152 za mahindi.
Waziri Mkuu Majaliwa alisema serikali ndio yenye jukumu la kutangaza hali ya chakula kama ni mbaya au nzuri.
“Tanzania bado haina tatizo la chakula, kelele zinazopigwa na baadhi ya vyombo vya habari na taarifa zinazotolewa si sahihi, serikali ndiyo yenye mamlaka ya kutangaza hali ya chakula na kwa maana hiyo basi bado tuna chakula cha kutosha,” alieleza Majaliwa na kuongeza kuwa pale serikali itakapokuwa na upungufu Watanzania watapata taarifa.
Waziri Mkuu alisema ni kweli kumekuwa na shida ya mvua, lakini sasa karibia maeneo yote mvua zimeanza kunyesha na mikoa mingine mvua zinanyesha na kutaka kutumia mvua zinazonyesha kwa kupanda mazao ya muda mfupi ili msimu ujao chakula cha kutosha kipatikane.
Pia alisema kwenye baadhi ya mazao yamepanda bei kutokana na nchi jirani za Afrika Mashariki kuwa na uhaba wa chakula.
“Kazi yetu ni kuhakikisha chakula kinakuwa kingi ili kiweze kuwa na bei nafuu,” alieleza na kuongeza kuwa tatizo hili limekuwa kama kampeni ya wafanyabiashara kuonesha nchi ina upungufu mkubwa wa chakula, jambo ambalo si sawa sawa.
Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba, alisisitiza kuwa hali ya chakula nchini inaridhisha isipokuwa zao la mahindi ambalo kwa sasa bei yake imepanda ikilinganishwa na msimu kama huu, wa mwaka jana.
Aidha, amekiri kuwa kwa sasa kumekuwa na uingiaji wa taratibu wa mazao mapya kutokana na baadhi ya maeneo kukumbwa na tatizo la uhaba wa mvua za vuli.
Aidha, ametoa onyo kwa wafanyabiashara aliowaita wenye hila wanaonunua mahindi kwa kasi na kuyafungia ndani na kusubiri bei ya zao hilo ipande zaidi ndipo wayalangue, na kuwataka wayauze mazao hayo mara moja kabla serikali haijachukua hatua za ziada dhidi yao.
Dk Tizeba alibainisha hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya chakula nchini, ikiwa ni pamoja na kutoa ufafanuzi dhidi ya madai kwamba nchi imekumbwa na baa la njaa.
“Nawahakikishia Watanzania kuwa hali ya chakula si mbaya, serikali inao utaratibu wake wa kutathmini hali ya chakula eneo kwa eneo, mkoa kwa mkoa na wilaya kwa wilaya,” alifafanua Dk Tizeba na kuongeza:
“Nafahamu kuwa kuna watu wanavumisha huko kwenye mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari kuwa kuna baa la njaa. Si kweli, serikali iko hadi kwenye ngazi ya mamlaka ya vitongoji inafahamu vyema hali halisi ya chakula ilivyo nchini,” alisisitiza.
Alisema kuanzia Oktoba mwaka jana, Tanzania ilikuwa na ziada ya chakula kilichozalishwa ya zaidi ya tani milioni tatu na hivyo kuwa na kiwango cha akiba ya chakula kwa asilimia 100.
Alisema kutokana na wingi huo wa mazao yaliyovunwa, wabunge na wananchi waliwasilisha kilio na wasiwasi wao juu ya uwezekano wa kushuka kwa bei ya mazao na kuomba waruhusiwe kuuza mazao hayo nje, ombi lililokubaliwa.
“Sasa ni takribani miezi miwili tangu turuhusu mazao hayo kuuzwa nje ambayo ni takribani tani milioni 1.5, tena tulitahadharisha wakulima kuwa makini kwa kutonogewa na bei na kujikuta wanauza kila kitu bila kuweka akiba, tulifanya hivi ili kuhakikisha usalama wa chakula nchini mwetu,” alifafanua.
Alisema nchi nyingi za jirani kama vile Msumbiji, Zambia, Malawi, Kenya na Uganda nazo hazikuzalisha kwa kiwango cha kuridhisha mazao msimu uliopita na hivyo kutegemea zaidi Tanzania.
“Kama kweli tungekuwa na uhaba wa chakula, nchi hizi nazo zingetangaza kukumbwa na balaa la njaa.”
Alisema katika taarifa inazokusanya kutoka sehemu mbalimbali nchini hali ya upatikanaji wa chakula katika masoko yaliyopo kwenye halmashauri zote inaridhisha isipokuwa bei ya mahindi iliyopanda ikilinganishwa na mwaka jana katika msimu kama huu.
Dk Tizeba alisema katika msimu wa chakula na soko kwa mwaka 2016/17 bei ya mazao imekuwa na mwelekeo wa kupanda kuanzia mwanzoni mwa Julai mwaka jana.
Alisema hadi kufikia Desemba mwaka huo, bei ya mahindi kwagunia la kilo 100 ilipanda na kufikia wastani wa Sh 84,000 ikilinganishwa na Desemba mwaka 2015 ambapo gunia la kilo hizo 100 liliuzwa kwa wastani wa Sh 65,104.
Kwa upande wa mchele na maharage, bei ina mwelekeo wa kushuka ambapo bei ya wastani kwa mwezi Desemba mwaka jana kwa gunia la kilo 100 ni Sh 151,957 wakati kwa mwaka 2015 bei ya gunia hilo liliuzwa kwa Sh 176,237 na maharage mwaka 2015 yaliuzwa kwa Sh 172,852 na hadi kufikia Desemba mwaka jana zao hilo liiuzwa kwa Sh 171.251.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa pamoja na hali hiyo hakuna hata soko moja hapa nchini ambalo limekosa bidhaa za mahindi, mchele na maharage. Alisema serikali inatambua uwepo wa tatizo la uhaba wa mvua za vuli ambazo katika baadhi ya maeneo hazikunyesha kwa kiwango kinachoridhisha hali iliyosababisha kuwepo na tatizo la uingizwaji wa mazao mapya.
“Lakini nataka ieleweke kuwa Tanzania inategemea zaidi mazao kupitia msimu wa mvua za masika na si vuli. Kutokana na hali iliyopo kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini tayari tumeanza kuona kuwa huenda pia mvua za masika zisijitosheleze katika baadhi ya maeneo,” alisema.
Alisema serikali imejipanga kupitia wakuu wa mikoa kueneza uelewa kwa wakulima kuhakikisha wanatumia mbegu zinazokomaa mapema na kupanda mazao yanayostahimili ukame.
Dk Tizeba alisema katika kuhakikisha nchi inakuwa salama Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kwa mwaka wa fedha 2016/17 ilipanga kununua jumla ya tani 100,000 za chakula, lakini hadi kufikia Januari 8, mwaka huu ilinunua tani 62,087 za mahindi sawa na asilimia 62 ya lengo iliyojiwekea.
Alisema kati ya tani hizo, tani 38,162 zilinunuliwa kupitia vituo vya ununuzi na tani 23,925 zilinunuliwa kupitia vikundi vya wakulima na hadi kufikia Januari 12, mwaka huu NFRA ina akiba ya tani 88,152 za mahindi. Waziri huyo, aliwataka viongozi wote nchini kutotumia hali ya ukame katika baadhi ya maeneo kueneza uvumi wa kuwepo kwa baa la njaa na kuwapatia taharuki wananchi.
Aidha, aliwataka wafanyabiashara wanaotumia fursa hiyo kwa lengo la kujifaisha wenyewe hapo baadaye kwa kununua mazao na kuyaficha kuacha mara moja kwani tayari serikali kupitia vyombo vyake inazo taarifa za wafanyabiashara hao na wakiendelea kukaidi watachukuliwa hatua.
Hivi karibuni, Rais John Magufuli alitoa mwito kwa wakazi wa maeneo mbalimbali nchini kutumia mvua zinazoendelea kunyesha kwa ajili ya kulima mazao yanayostahimili ukame badala ya kutegemea chakula kutoka serikalini.
Rais Magufuli alisema sasa wakati wa kulima mahindi umebadilika, na wakulima wasijilazimishe kulima mahindi ambayo yanahitaji mvua nyingi.
“Mvua zinaponyesha tulime kwani hakuna shamba la serikali,” alieleza Dk Magufuli. Imeandikwa na Sifa Lubasi, Dodoma na Halima Mlacha, Dar.
CHANZO: HABARI LEO
No comments:
Post a Comment