Wiki iliyopita tulianza kuzungumzia mambo ambayo yanaweza kumsaidia mwanamke anayefanya kazi kujipanga ili kuzimudu vyema kazi za nyumbani na kazini. Leo tunaendelea kueleza mambo hayo.
Kuamka mapema asubuhi
Kama anapotoka usingizini huwa anachelewa kuchangamka, usiku kabla ya kulala afanye baadhi ya mambo ambayo huwa akilazimika kuyafanya asubuhi.
Mambo hayo ni kama vile kuandaa nguo watakazovaa asubuhi yeye na watoto; kuandaa meza kwa ajili ya kustaftahi na kuweka katika mkoba nyaraka na vitu atakavyoondoka navyo asubuhi. Muhimu zaidi ni kuandika mambo yote anayokusudia kuyafanya siku inayofuata.
Ni lazima awe na utaratibu wa kufanya mazoezi walau kwa dakika chache ili kufanya damu itembee vyema mwilini.
Kukamilisha jambo aliloanza kulifanya
Watu wengine huwa na maisha ya shughuli nyingi ambazo wanazianza na kuziacha hazijakamilika. Hali hii huwafanya wajikute wana viporo vya kazi nyingi na hata kuweza kupata msongo wa mawazo. Usiwe unaacha viporo vya kazi kwani kila kazi unayoikamilisha hukuletea faraja. Kila unapowatangazia wanafamilia kazi uliyoikamilisha utajiongezea furaha na juhudi. Tumia tabia hiyo kwa kusema kama vile. “Nimekamilisha kazi ya kusafisha stoo ambayo nilikuwa nimekusudia kuifanya siku nyingi bila mafanikio” au “Nimewasilisha mpango wangu wa kazi wa mwaka mzima kwa bosi wangu.”
Kugawa kazi kwa watu wengine
Kanuni nyingine muhimu ni ya kugawa kazi kwa watu wengine nyumbani au kazini. Usijilimbikizie kazi zote hata zile ambazo zinaweza kufanywa na watu wengine vizuri na kwa muda mfupi. Kwanza amua kwa makini ni kazi ipi ambayo unaona huwezi kuifanya peke yako au unayoweza kumpatia mtu mwingine akusaidie. Pili tafuta mtu unayeamini anaweza kuifanya kwa usahihi. Tatu toa maelekezo sahihi ya jinsi inavyotakiwa ifanyike. Jambo la nne ni kufuatilia utekelezaji ili kuhakikisha inatekelezwa jinsi inavyostahili.
Kufanya maamuzi sahihi
Kuna uamuzi unaohusiana na kazi ambayo huwa tunayafanya kila siku nyumbani au kazini. Tukifanya uamuzi wa busara kila siku tutafanya utekelezaji wetu wa kazi usiwe wa dharura au wenye uchovu. Ni muhimu kuzingatia mambo yafuatayo.
•Amua kazi gani ifanyike wakati gani?
Licha ya kutekeleza kazi kwa kuzingatia vipaumbele, zitambue kazi zinazoweza kuunganishwa katika safari mmoja. Kwa mfano mama anapokuwa akielekea kulipa bili ya maji anaweza kutumia safari hiyo hiyo kupita sokoni kununa mahitaji ya nyumbani na hata kupita hospitali kumuona mgonjwa. Vilevile ni muhimu mwanamke achunguze ni nyakati zipi katika siku anakuwa na uwezo zaidi wa kufanya kazi na kuutumia wakati huo kwa kufanya kazi zinazohitaji uwezo na makini zaidi.
•Kwa jasiri kuweza kusema hapana
Inapotokea kuwa kuna ndugu au jamaa anayetaka kukuona au anataka umfanyie kazi fulani na wewe una kazi nyingine uwe jasiri kusema hapana na kumpangia siku au wakati ambao hautaathiri ratiba yako ya kazi.
•Jifunze kuacha kufanya kazi unapochoka
Wakati wowote mtu anapojisikia yuko hoi na hawezi kufanyakazi yoyote vizuri kama ipasavyo ni vizuri apumzike, baada ya kupumzika na kujisikia uchovu umetoka aendelea na kazi.
•Jitume mwenyewe
Kufanya kazi ni suala linalotaka moyo wa kujituma. Inabidi mwanamke ajitume mwenyewe. Kila kazi anayofanya aifanye kwa kasi inayostahili ili kuepuka kupoteza muda.
Fanya sasa usingoje baadaye
Adui mkuu wa kazi ni kuahirisha kazi kwa kusema “Nitaifanya kesho au baadaye. Zifuatazo ni mbinu zitakazomsaidia mwanamke kuepuka tabia ya kuahirisha utendaji wa kazi.
•Unapopanga kazi weka malengo yanayotekelezeka na epuka kuweka malengo kwa jazba ambayo yanaweza kuwa kama ndoto zisizo na uhalisia.
Unapoweka lengo na ukafanikiwa kulitekeleza ni fahari kwako. Itenge kazi kubwa katika hatua au awamu. Unapokuwa na wasiwasi kuwa kazi fulani ni kubwa sana na hutaweza kuimaliza mara moja, itenge katika hatua kadhaa za kuitekeleza.
•Kadria muda wa kuikamilisha kazi. Jiambie wewe mwenyewe katika nafsi yako kuwa kazi fulani utaimaliza katika muda fulani. Kwa mfano sema “Kazi hii nitaimaliza katiika saa moja.” Baada ya muda huo jiulize kama umeitekeleza
•Tenga muda maridhawa wa kutekeleza kazi zako. Unapopanga muda wa kufanya kila kazi hakikisha kila moja unaiwekea karibu mara mbili ya muda halisi unaohitajika kuitekeleza. Hii itakusaidia wakati wa utekelezaji usijione kama umechelewa na uko nyuma ya wakati.
•Iwekee utaratibu wa kujizawadia
Unapokamilisha kazi fulani, hasa ile ambayo ilikuwa mgumu jipongeze mwenyewe na ujipe zawadi. Zawadi inaweza kuwa hata kitu kidogo tu kama vile kujinunulia kitamaa cha mkononi ambacho umekuwa una hamu sana ya kuwa nacho au hata kwenda saluni kujiremba na mengine mengi. Lengo likiwa kujifurahisha kwa kufaulu kutekeleza kazi fulani.
•Anza kwanza kutekeleza kazi ngumu
Unapopanga kutekeleza kazi anza na zile zilizo ngumu na zisizovutia. Ili usikate tama, wakati wote utakapokuwa ukitekeleza vuta hisia uwaze jinsi itakavyovutia itakapokamilika au furaha utakayokuwa nayo utakapoikamilisha.
No comments:
Post a Comment