Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli amewaapisha mabalozi sita watakaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali duniani huku akiwaambia mabalozi hao kuwa litakuwa jambo la fedheha kwa taifa endapo mabalozi hao watashindwa kufanya jambo la kukumbukwa katika taifa katika kipindi chao cha uwakilishi.
Rais Dkt John Pombe Magufuli ameyasema hayo Ikulu jijini Dar es Salaam mara baada ya kuawaapisha mabalozi sita watakaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali duniani ambapo mbali na kuwataka kudumisha mahusiano baina ya Tanzania na nchi hizo ameongeza kuwa itakuwa ni fedheha endapo katika kipindi chao chote cha uwakilishi patakosekana matunda ya kukumbukwa katika taifa.
Pia Dkt Magufuli amewaeleza mabalozi hao kuwa yeye pamoja na taifa la watanzania kwa ujumla wanategemea uwakilishi uliotukuka kutoka kwa mabalozi hao.
Wakizungumza mara baada ya kuapishwa mabalozi hao akiwemo Dkt Emmanuel Nchimbi anayeiwakilisha Tanzania nchini Brazil wamesema watatumia fursa zilizopo katika mataifa wanayokwenda ili kuiwezesha Tanzania kufikia azma ya kuwa Tanzania ya viwanda kama ilivyo Azma ya serikali ya awamu ya tano hususani katika sekta za viwanda, gesi na mafuta.
Mabalozi walioapishwa hii leo katika hafla iliyohudhuriwa pia na makamu wa rais Mama Samia Suluhu Hassani pamoja na nchi wanazokwenda kuziwakilisha ni pamoja na balozi Dkt James Msekela, balozi wa Geneva katika umoja wa mataifa, balozi Mbelwa Kairuki balozi wa China, balozi George Madafa, balozi wa Italia, balozi Emmanuel Nchimbi, balozi wa Brazil,balozi Fatma Rajab balozi wa Qatar na Profesa Elizabeth Kiondo, balozi anayeikilisha Tanzania nchini Uturuki.
No comments:
Post a Comment