Tukio la mwanamke mmoja mkoani Mara kucharazwa viboko 50 na wanaume wanaodaiwa ni wa kutoka kwenye baraza la kimila, ndilo lililofunga mwaka 2016 na kuufungua mwaka mpya wa 2017, lakini Uwazilimekuwa gazeti la kwanza kuzungumza na mwanamke huyo ana kwa ana ambaye amesimulia mazito juu ya nini kilitokea, kubwa zaidi ni ujauzito wake kuharibika kwa sababu ya kipigo.
TUJIKUMBUSHE KWANZA
Januari 9, mwaka huu, video inayomwonesha mwanamke huyo akiwa anacharazwa viboko na wanaume wasiopungua wanne ilisambaa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kiasi cha kuzua taharuki katika jamii.
Wengi walilaani tukio hilo huku habari zikisema kuwa, Polisi Makao Makuu jijini hapa walitoa agizo kwa makamanda wote wa polisi wa mikoa nchini kufuatilia kwa kina tukio hilo la kinyama ili kubaini lilitokea wapi baada ya video hiyo kutotoa ushirikiano wa sehemu husika.
JANUARI 12, 2017
Januari 12, vyombo vya habari vikaripoti kuwa, tukio hilo lilitokea wilayani Rorya, Mkoa wa Mara ambapo watu kumi walikamatwa wakihusishwa na tukio hilo lililotafsiriwa kuwa ni la kudhalilisha na kuondoa utu wake.
UWAZI LAFUATILIA KWA KINA
Kwa kawaida, kukamatwa kwa watu hao kumi na kufikishwa kwenye Kituo cha Polisi cha Rorya ilikuwa ndiyo hitimisho la tukio hilo licha ya kwamba, Watanzania walio wengi walikuwa na kiu ya kujua kisa cha tukio na mhusika anasemaje na nini kinandelea? Ndipo Gazeti la Uwazi, kama kawaida yake ya ufuatiliaji wa matukio hata ndanindani, lilijivika jukumu la kufuatilia.
JANUARI 14, 2017
Januari 14, mwaka huu katika Kitongoji cha Kwitonyi, Kijiji cha Kinesi, Kata ya Nyamuga, Wilaya ya Rorya mkoani hapa, Uwazi lilikutana ana kwa ana na Ghati Chacha Makori (32) ambaye alikiri kuwa, yeye ndiye yule mwanamke anayeonekana kwenye video akicharazwa viboko.
UWAZI LAMKUTA AMEKAA UPANDEUPANDE
Nje ya nyumba yake ya matofali ya kuchoma, Ghati alikuwa amekaa upandeupande na alipoulizwa alisema kuwa, mpaka siku hiyo ya Jumamosi alikuwa anasikia maumivu makali sana yaliyotokana na kupigwa viboko hivyo hakuwa anaweza kukaa kwa makalio.
HII HAPA SIMULIZI YAKE
Akizungumza na Uwazi nyumbani hapo, Ghati, mama wa watoto wanne, alisema:
“Ilikuwa Desemba 23, 2016, majira ya kama saa 2:00 hivi asubuhi, mimi nikiwa hapa nyumbani kwangu na familia yangu, walifika vijana wawili, pia ni wakazi wa kijiji hiki, wakaniambia naitwa na wazee wa kimila wa kijiji.
“Mimi niliwaambia wale vijana kwamba, sitaweza kwenda huko kwa sababu naumwa, na kweli naumwa hata sasa. Lakini cha ajabu, wale vijana waligoma kuondoka kupeleka majibu, wakaamua kunibeba kwa nguvu kwenye baiskeli hadi kwa wazee wa kimila ambao niliwakuta wamekusanyika kwenye mkutano chini ya mti.
WAZEE WAMHUKUMU
“Baada ya kufikishwa kwenye mkutano huo wa kimila, wale wazee wa kimila walinihukumu kwa kuamuru nichapwe viboko hamsini (50) bila kunieleza kosa langu ni nini! Wala hawakunipa nafasi ya kujieleza kwenye mkutano huo uliokuwa ukiongozwa na wazee 12.
UJAUZITO WA MIEZI MITATU WAHARIBIKA
“Nikiwa nashangaa sasa, ghafla walianza kunicharaza viboko kwenye makalio huku wakiwa wamenilaza chini na kunikanyaga shingoni ili nisitapetape.
“Hali ile ilinisababishia maumivu makali sana. Kwa kweli maumivu yalikuwa makali sana. Mbaya zaidi wakawa wanaitana kuja kunicharaza viboko. Kila mmoja alichapa idadi yake.
“Nilikuja kushtuka nikiwa navuja damu nyingi. Nilikuwa na ujauzito wa miezi mitatu nao ukachoropoka.
AELEZWA KISA CHA KUCHARAZWA VIBOKO
“Baada ya kuchapwa viboko hivyo, wale wazee walimuita mbele yangu mama yangu mzazi, anaitwa Anna na kisha wazee hao wakanieleza mbele ya mama kwamba, wamenicharaza viboko kwa sababu mama yangu aliwapelekea malalamiko kwamba, nimemtukana na kumuita mchawi na kumkana kuwa yeye si mama yangu mzazi na kwamba nitamuua kwa sumu kwa vile amekatalia nisiuze matofali yangu.”
MADAI YANA UKWELI?
“Ni kweli yule ni mama yangu aliyenizaa, lakini namkataa kabisa kuwa si mama yangu kwa sababu alinifanyia unyama mkubwa bila kujali kuwa mimi ni mtoto wake wa kwanza wa kuzaa na kwa sasa nina mji (makazi) wangu.
“Kisa kiko hivi, nilifyatua matofali 5,800 nyumbani kwetu anapoishi mama, nikayachoma ili niyauze, nilipe mkopo wa watu, lakini mama aliyakatalia matofali hayo nisiyauze, hivyo mimi sioni sababu ya kumuita mama yangu. Mimi najua alipoona nakazania kuuza matofali yangu akaamua kunisemea kwa wazee wa kimila ili nichapwe viboko kama njia ya kunitisha,” alisema Ghati kwa sauti ya kujiamini.
MAMA WA GHATI ANASEMAJE?
Baada ya kusikia maelezo ya Ghati, Uwazi lilimfuata mama yake, Anna Chacha Makori (53), ambaye katika utetezi wake wa kwa nini alimfikisha bintiye kwa wazee wa kimila, alisema:
“Mimi niliamua kumpeleka Ghati kwa wazee wa kimila ili apigwe viboko kwa sababu ananidharau na kuanza kunitukana kuwa mimi ni mchawi mkubwa na kwamba ataniua. Pia amenikana kwamba mimi sijamzaa.”
BARAZA LA WAZEE WA KIMILA LAFUTWA
Matiku Wambura Iramba ni Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Kinesi, yeye akizungumzia tukio hilo alisema:
“Ofisi yangu imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kuchapwa viboko kwa Ghati kwani baraza hilo la kimila lilikuwa likifanya shughuli zake kinyume cha sheria bila ofisi yangu kuelewa. Desemba 21, 2016 (siku mbili kabla ya tukio la Ghati) ofisi yangu ililiandikia baraza hilo barua rasmi ya kulifuta baada ya kulalamikiwa na wananchi juu ya utendaji kazi wake unaokiuka haki za binadamu.
“Kwa hiyo ninachoweza kusema ni kwamba, tayari baraza hilo nimelifuta. Sijui tena wazee hao walikaa na kuendesha vikao vyao kwa kibali cha nani, nasubiri huyo mwathirika wa tukio alete barua za hospitali ili niwachukulie hatua kali wale wote walioendesha zoezi hilo la kinyama.”
SHUGHULI ZA GHATI
Ghati alisema amekuwa akipata riziki yake ya kila siku kwa kufanya shughuli za kilimo cha bustani ya mbogamboga lakini kwa sasa hawezi kwenda bustanini na hivyo kutegemea msaada wa watoto wake wadogo.
KAULI YA KAMANDA WA POLISI KANDA MAALUMU akizungumza na gazeti hili Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Tarime, Rorya ACP Sweetybert Njewike alisema wamemtafuta Ghati lakini wameshindwa kumpata kwa kuwa wazee wa Kimila wamemficha.
Kama kuna uwezekano wa kumleta hapa kituoni mleteni wale wazee wamemficha baada ya kumfanyia ukatili ule”, alisema na kuongezakwamba tabia ile ya kimila haifai na inapaswa kupigwa vita na kila Mtanzania.
No comments:
Post a Comment