MKAZI wa kijiji cha Chapakazi, Mbalizi mkoani Mbeya, Jonas John (28) anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa, baada ya kukamatwa akifukua kaburi la mtu mwenye ualbino, aliyefariki a kuzikwa kijijini Mumba mwaka 2010.
John, mkazi wa kata ya Ilembo katika wilaya ya Kipolisi ya Mbalizi, alikamatwa saa 7 usiku jana.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Mbeya, Dhahir Kidavashari, alisema John alikamatwa katika kijiji Mumba kata ya Ilembo, Tarafa ya Isangati Wilaya ya Kipolisi Mbalizi, mkoani humo.
Kijana huyo alikamatwa na askari akiwa na wenzake wawili, wakifukua kaburi la mtu aliyefahamika kwa jina la Sister Osisara, aliyekuwa mlemavu wa ngozi (albino) kwa lengo la kuchukua viungo vyake.
Alisema inadaiwa kuwa Osisara, alifariki dunia mwaka 2010 kwa ugonjwa wa homa na kuzikwa katika makaburi ya kijiji cha Mumba.
Kamanda alisema mtuhumiwa alikutwa na majembe na koleo, ambayo walikuwa wakiyatumia kufukulia kaburi hilo usiku huo, kabla ya wakazi wa maeneo ya jirani na makaburi hayo kubaini kilichokuwa kikiendelea na kutoa taarifa.
Alisema baada ya mtuhumiwa kukamatwa na kuhojiwa na polisi, aliwataja washirika wenzake wawili, ambao walikimbia baada ya kuwaona askari. Kamanda Kidavashari alisema msako unaendelea, kuwatafuta watuhumiwa wawili waliokimbia.
Aliwataka watu au mtu yeyote aliye na taarifa, juu ya walipo watu hao, kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama ili hatua zichukuliwe dhidi yao.
“Wenzie wawili walikimbia kwa kuwa ilikuwa rahisi kwao kuwaona polisi kwani walikuwa nje, huyu mwenzao aliyekamatwa akiwa ndani ya kaburi,” alisema Kamanda Kidavashari.
Taarifa zaidi kutoka kwa baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, zinaeleza kuwa mtuhumiwa alikutwa ndani ya kaburi akiwa amemaliza kazi ya kutoa udongo.
Mashuhuda walidai alikuwa amebakia kuutoa mwili wa marehemu nje ya kaburi hilo, lakini alishindwa kutimiza azma hiyo baada ya wanandugu na majirani na makaburi, kushtuka na kutoa taarifa kisha kwenda makaburini hapo, kabla ya watuhumiwa wawili kukimbilia kusikojulikana.
No comments:
Post a Comment