WATU watatu wamehukumiwa kifungo cha maisha jela katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, baada ya kupatikana na hatia ya makosa matatu, ikiwemo ubakaji wa wasichana wawili na unyang’anyi wa kutumia silaha.
Washitakiwa hao ni Jackson Saimon (24), Kirapu Mgendi (41) na Marwa Mninko (44). Walihukumiwa kifungo hicho jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Juma Hassan, wakati shauri hilo lilipopelekwa kwa ajili ya hukumu.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Hassan alisema upande wa Jamhuri ulipeleka mashahidi tisa kwa ajili ya kuthibitisha mashitaka hayo ambapo hawakuacha shaka yoyote. Hakimu Hassan alisema katika kosa la kwanza la unyang’anyi wa kutumia silaha ni kwenda jela miaka 30, kosa la pili miaka 30 na tatu ambalo ni kubaka kwa nguvu kifungo cha maisha.
Alisema washitakiwa walikuwa wanakabiliwa na mashitaka matatu ambayo ni unyang’anyi wa kutumia silaha na kuwabaka wasichana wawili kwa zamu.
“Nimeridhishwa na ushahidi uliotolewa mahakamani hapa hivyo washitakiwa ninawatia hatiani washitakiwa wote kwa mashitaka yote matatu kama walivyoshitakiwa,” alisema Hakimu Hassan.
Akisoma baadhi ya ushahidi uliotolewa mahakamani hapo, alisema washitakiwa hao walivamia watu wanne nyumbani kwa Asungwile Mwakisole usiku akiwa amelala wakitaka fedha.
Alisema watu hao walimfunga Mwakisole kitambaa usoni, kamba mkononi na miguu huku wakimpiga na ubapa wa panga usoni ambapo alianza kupiga kelele.
Alieleza kuwa wakati anaendelea kupiga kelele walimpiga na kitu kama nondo kichwani wakidai atulie hapo alipo huku wakitaka awaonyeshe silaha iliko kwani alidai hana.
“Akiwa anaendelea kupekuliwa alisikia sauti ya watoto ambao ni mabinti watatu anaoishi nao wakiwa karibu na chumbani kwake wakilalamika kuwa wanaumizwa kumbe walikuwa wanawabaka kwa zamu,” alisema Hakimu Hassan.
Aliongeza kuwa wasichana wawili ndio walibakwa kwa zamu na watu watatu na baada ya tukio hilo washitakiwa waliondoka ambapo wasichana hao walikwenda kumfungua baba yao na kumueleza walivyobakwa.
Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, Wakili wa Serikali Grace Mwanga aliomba mahakama iwape adhabu kali ili iwe fundisho kwao na wengine wenye tabia kama hiyo.
Mshitakiwa Saimon, aliomba mahakama imwachie huru kwani hajafanya kitu chochote wakati mshitakiwa wa pili alidai anaweka nia ya kukata rufani na watatu alibaki kimya.
Inadaiwa washitakiwa hao walitenda kosa hilo Julai 27, 2015 eneo la Kipunguni wilayani Ilala.
Inadaiwa washitakiwa waliiba simu tatu televisheni mbili na begi la shule, mali ya Mwakisole na baada ya wizi huo walimtishia kwa panga na kisu pamoja na kipande cha chuma ili kufanikisha wizi huo. Pia washitakiwa waliingia chumbani kwa mabinti wa mlalamikaji na kuwabaka kwa zamu.
No comments:
Post a Comment