WAUMINI wa dini ya Kiislamu Tanzania, jana waliungana na Waislamu wenzao duniani, kusherehekea siku ya kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W).
Akizungumza katika Baraza la Maulid lililofanyika kitaifa kijiji cha Shelui wilayani Iramba mkoani Singida, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa pamoja na mambo mengine aliwataka Waislamu kudumisha amani, utulivu na mshikamano na waumini wa dini nyingine.
Alisema serikali itaendelea kulinda uhuru wa kila mwananchi, kuabudu kile anachoona kinafaa na kwamba itafanya kila liwezekanalo, kusimamia na kuhakikisha hakuna kikundi kinahatarisha usalama wa nchi.
Alinukuu kauli ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliyosema kuwa “Nchi haina dini, bali watu wake wana dini” na kwamba serikali itaendelea kusimamia uhuru wa kuabudu.
Tunapenda kuunga mkono kauli hiyo ya Waziri Mkuu ya kuhakikisha kwamba hakuna kikundi kinahatarisha usalama wa nchi yetu kutokana na ukweli kwamba yapo baadhi ya makundi, yana nia mbaya ya kutaka kuvuruga amani, utulivu na mshikamano wetu.
Hapa tungependa kusisitiza kwamba wananchi kwa ujumla wao, pia wana jukumu la kushirikiana na kushikamana na serikali yao katika hili, kwa maana ya kutoa taarifa katika vyombo husika, iwapo watabaini vikundi au watu, wanaotaka kutuletea zahama ya kuvuruga amani yetu.
Ieleweke kwamba katika suala zima la kulinda amani ya nchi yetu, serikali na wananchi hawana budi kuzungumza lugha moja ili pasiwepo mwanya wa maadui, kutumia ufa wa aina yoyote ile ili kulivuruga taifa letu.
Akizungumza katika sherehe hizo, Mufti wa Tanzania, Abubakar Zuberi bin Ali alisema kuzaliwa kwa Mtume Muhammad na maisha yake kwa ujumla yalilenga furaha, amani na umoja wa kuishi kindugu baina ya Waislamu, wasio Waislamu na jamii nzima.
Katika hili la kudumisha amani kwa kila hali, Mufti alitaka Waislamu wamuenzi Mtume Muhammad kwa kuacha majungu, fitina na kuishi kwa upendo. Hapa viongozi wetu hawa wa serikali na dini, wanatoa msisitizo zaidi kwetu kama Watanzania kuendelea kudumisha utamaduni wetu, uliojengeka kwa muda wa miaka mingi kabla na hata baada ya kupata uhuru wetu miaka 55 iliyopita kuwa ni watu tunaoishi kwa pamoja bila kubaguana.
Ubaguzi wa aina yoyote ile, ikiwa ni pamoja na ubaguzi wa dini, kabila, rangi na ubaguzi wa kiitikadi, hauna nafasi katika taifa letu kwa lengo moja kuu la kutaka kuleta ustawi katika maendeleo ya kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na kuimarisha mshikamano.
Taifa lolote linaloendekeza aina yoyote ya ubaguzi uliotajwa, itakuwa ni vigumu kuweza kufikia maendeleo ya kweli na ustawi kwa watu wake. Pamoja na changamoto nyingine tulizopitia kama taifa, bado nchi yetu inajivunia umoja, amani na utulivu na inaendelea kukabiliana vilivyo na vita dhidi ya maradhi, ujinga na umasikini.
Hakuna ubishi kwamba kuna kila aina ya dalili ya kuvishinda vita hivyo kadiri tunavyopambana navyo, mradi wale wanaotaka kutukwamisha katika vita hivi, wasipewe nafasi. Mungu Ibariki Tanzania.
No comments:
Post a Comment