Tuesday, 13 December 2016

Wanaozimia viwanjani kumbe siyo bure


By Fredrick Nwaka

Mtandao wa Healthline.com, unaeleza, kuzimia ni tendo linalotokea, wakati mwingine bila kutarajia. Mara nyingi husababishwa na ubongo kukosa oksijeni ya kutosha na kufanya mtu kupoteza fahamu. Pia presha ya kushuka inatajwa kuwa chanzo.


Kitaalamu, inaelezwa kuwa upungufu wa mtiririko wa damu kwenye ubongo husababisha kuzimia. Aina za watu kuzimia zimeainishwa kitaalamu kuwa ni; vasovagal, carotid sinus syncope na situational syncope.
Mtandao huo umeainisha kuwa vasovagal imekuwa ikitokea mara nyingi, hasa kwa watoto na wakati mwingine vijana. Aina hii ya kuzimia inatokana na mshtuko, msongo wa mawazo, mwelekeo wa damu, na wakati mwingine hutokea kwa mtu kusimama muda mrefu.
Kama mtu ana historia ya kuzimia, anatakiwa kujichunga kuzuia jambo fulani ili isimtokee hata kuzimia. Ikitokea hivyo, inatakiwa kukaa ama kulala. Wengine huzimia wanapopata matibabu, wakati mwingine mwambie daktari hali yako. Daktari anaweza kukushauri cha kufanya kuepuka hali hiyo.
Kuhisi kizunguzungu pamoja na kuishiwa nguvu, inatakiwa kuinamisha kichwa kwenye magoti ili damu iweze kutiririka kwenye ubongo kwa urahisi au lala ili usiumie endapo itatokea kudondoka. Usisimame hadi utakapojihisi nafuu.
Nini cha kufanya kwa aliyezimia
Kama itatokea mtu uliyenaye anaishiwa nguvu hata kuzimia, mwambie alale na unyanyue miguu yake juu ili kusaidia damu kuelekea kwenye ubongo kwa urahisi.
Mfungue vifungo vya shati kama wmkanda na nguo nyingine zilizombana. Mwache mgonjwa alale dakika 10 hadi 15 akipata upepo. Ukimya utawale na kumweka sehemu yenye utulivu ni vizuri zaidi. Akinywa maji baridi, pia inaweza kumsaidia.
Mashabiki Simba na Yanga
Hapa Tanzania, unapokaribia mchezo baina ya wapinzani wa jadi Simba na Yanga mashabiki na wapenzi wa timu hizo huwa ‘matumbo joto’ kila mmoja akiomba timu yake ipate ushindi.
Wengi wao wakitawaliwa na hisia na mapenzi yaliyopitiliza kwa klabu wanazoshabikia. Hata Ulaya na America Kusini, visa vya mashabiki kuzimia viwanjani vimejitokeza mara kadhaa na kuzua mijadala ulimwenguni kote.
Miaka minne iliyopita katika mchezo wa Ligi Kuu baina ya timu hizo uliomalizika kwa Simba kuichakaza Yanga mabao 5-0, mashabiki wa timu zote mbili walijikuta wakizimia ama kwa furaha au kwa huzuni.
Vimekuwa kama vitendo vya fasheni hasa katika mchezo wa Simba na Yanga. Pambano la msimu wa mwaka juzi uliomalizika kwa sare ya 3-3, hali ilikuwa hiyo na hata mechi ya iliyomalizika kwa Simba kusawazisha dakika 87, baadhi ya mashabiki walizirai.
Spoti Mikiki imefanya mahojiano na mashabiki wa soka, madaktari na wanasaikolojia juu ya suala hili ambalo pia huwaacha hoi wapenzi wa soka.
Msalaba Mwekundu
Watoa huduma ya kwanza wa Chama cha Msalaba Mwekundu, ndiyo waliopewa jukumu la kukabiliana na hali za mashabiki uwanjani.
Ofisa Habari na Mawasiliano wa Red Cross Tanzania, Kamar Yusuph anasema jukumu kubwa la shirika hilo kunapotokea matukio ya mashabiki kuzimia viwanjani ni kuhakikisha wanapata huduma ya kwanza kabla ya taratibu nyingine kufuata.
“Tuna kitengo kinaitwa volunteers (watu wa kujitolea) ambao wanapewa mafunzo ya namna ya kutoa huduma ya kwanza kabla ya viwanjani na katika maeneo mengine yenye mikusanyiko ya watu.
“Kazi yetu ni kuhakikisha mgonjwa anapata huduma ya kwanza na kisha kumuwahisha hospitali kwa taratibu nyingine,” anasema.

Mashabiki wadai mahaba yamezidi.
Pastory Mwakyagi aliyejitambulisha kuwa ni shabiki wa Simba anasema mashabiki wengi wana mapenzi yaliyozidi kwa klabu zao na ndiyo maana lolote linalotokea, wanakuwa waathirika wa kwanza.
“Mashabiki wa soka wana mahaba yaliyopindukia na wanashindwa kuzuia hisia zao na kujikuta wanazimia, ukizingatia watanzania wengi ni maskini, wanakwenda viwanjani kutafuta faraja nako wanajikuta wanaumizwa, ndiyo inafikia hatua wanajiuzulu,” anasema.
Mhimitimu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino, Aloyce Mchunga anasema sababu kubwa inayopelekea mashabiki kuzimia ni kwa kuwa wanakwenda viwanjani na matokeo mifukoni.
“Matokeo yanapokuja tofauti, wanapatwa na mshtuko wa akili na moyo na matokeo yake wanazimia.”
Bali Lucas Samba anasema mashabiki wanazimia kwa sababu ya presha inayotokana na kuwa na imani kubwa na wachezaji na timu zao. “Mashabiki hasa wa Simba na Yanga wanazimia kwa sababu wachezaji wanaoamini watawapa matokeo inakuwa tofauti.”
Mkubwa Kambi ambaye ni shabiki wa Simba anasema kuna mashabiki wanazimia kwa furaha na wengine kwa huzuni na kulihusisha suala hilo na hisia na mahaba ya timu zao.
“Kama unakwenda uwanjani ukiwa na hisia za kawaida huwezi kujikuta katika katika hali hiyo (kuzimia), tatizo ni hisia. Ilitokea katika mechi ya Simba na Yanga, Yanga ilipoongoza kwa magoli matatu mashabiki wa Simba walizimia kwa huzuni na waliposawazisha mashabiki walizimia kwa furaha, kwa hiyo ni suala la hisia kwa ujumla.
Shabiki mwingine wa soka Obadia Mwidete anasema suala la mashabiki wa soka kuzimia viwanjani si jambo geni duniani kote.
“Mambo haya yanatokea duniani kote na ni kutokana na mashabiki wanataka timu zao zifanye vizuri lakini inakuwa ndivyo sivyo. Wanajikuta wanashindwa kuzuia mihemko yao,” anasema.
Madaktari wa michezo
Daktari wa Simba, Yassin Gembe anasema tatizo la mashabiki kuzimia viwanjani linasababishwa na mshtuko unaotokana na kutokujua hali za afya zao.
“Soka kama ilivyo michezo mingine ni mchezo unaotawaliwa na hisia lakini mashabiki wengi wanakwenda viwanjani pasipo kujua afya zao.
“Watazamaji ni mchanganyiko wa watu tofauti na wana matatizo yao kiafya kama presha au maradhi ya mshtuko. “Ni muhimu kujua afya yako na kuhakikisha unakwenda uwanjani ume-relax (umetulia),” anasema Gembe na kuongeza kuwa jukumu la madaktari wanapokuwepo viwanjani ni kutoa huduma ya kwanza kabla ya utaratibu mwingine kufanywa.”
Naibu katibu mkuu wa chama cha madaktari wa tiba za michezo Tanzania, Dk Sheikhy Mngazija anasema sababu kubwa ni mashabiki kuingia na matokeo uwanjani na ikiwa kinyume hali hiyo huwatokea.
“Kitaalamu mshtuko unatokea pale shabiki anapoingia uwanjani na kukutana na jambo ambalo hakulitarajia, mwishowe mapokeo ya mwili na akili yanakuwa tofauti na ndipo anapata mshtuko na kuzimia.
Daktari wa timu ya Yanga Nassoro Matuzya mbali na kuamini suala hili ni la kisaikolojia, anasema zimiazimia ya mashabiki viwanjani inatokana na mwambata wa maradhi yanayoleta msisimko wa mwili yanapotokea ghafla.
“Suala hili ni mwambata wa maradhi, unakuta shabiki anakwenda uwanjani akiwa na ugonjwa kama presha au magonjwa ya mshtuko. Inapotokea jambo la furaha au huzuni humpa msisimko unaosababisha mwili kupoteza fahamu ghafla. Ni vizuri mashabiki wapunguze hisia na mapenzi yaliyopitiliza,” anasema.
Wanasaikolojia wana mtazamo upi?
Mhadhiri wa saikolojia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Chris Mauki anasema kisaikolojia wanadamu wanatofautiana katika mapokeo ya tukio fulani na kuongeza kuwa utendaji wa moyo hupokea hisia juu ya jambo husika.
“Furaha na maumivu ya mwanadamu yametenganishwa na mstari mdogo sana. Utendaji wa moyo ndio unapokea hisia na ndiyo unakuta mtu akiumia au kuwa na furaha iliyochanganywa na presha ya jambo husika inatokea mtu kuzimia.
“Kingine unakuta mtu amepania mechi au mchezo fulani na kuweka dau kwamba timu yake itashinda, matokeo yakiwa tofauti anajikuta anapoteza fahamu na kuzimia, kwahiyo ili suala ni la kiasili zaidi,” anasema Dk Mauki.
Mhadhiri wa saikolojia katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino, Padri Leons Maziku anasema kuna uhusiano wa karibu kati ya mwili na akili unaoitwa psychical-somatic relationship na kuongeza kuwa soka ni furaha na unahusisha mawazo hivyo unaathiri mzunguko wa damu na mapigo ya moyo.
“Katika furaha au hasira kuna homoni inayoitwa adrenaline, hii ina uthubutu na ujasiri. Kwenye mechi shabiki anakuwa na mategemeo makubwa ilia pate furaha hivyo anakwenda mpirani na mchanganyiko wa furaha, woga na msongo wa mawazo.”
“Matokeo yakiwa kinyume, anapata mshtuko unaotokana na damu kwa nguvu na haraka kwenda kwenye ubongo na kujikuta mtu anapoteza fahamu,” anasema.

MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!