Friday, 2 December 2016

Msituchonganishe na Dangote - Mwijage

SERIKALI imesema kumekuwa na taarifa zisizo sahihi zinazosambaa kuhusu Kampuni ya Saruji ya Dangote na kubainisha kuwa haipo tayari kumuachia mwekezaji yeyote aondoke nchini, lakini haiwezi kutoa kila kitu bure au kumpa mwekezaji nishati bure badala yake wameweka vivutio vitakavyowawezesha kuwekeza.


Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam alipozungumzia masuala ya uwekezaji nchini, na kufafanua kuwa suala la Dangote limekuzwa na watu wasio na taarifa za uthibitisho kutoka kwa vyanzo sahihi.
“Mpaka sasa nataka kuwathibitishia kwamba hakuna tatizo katika viwanda vyote vya saruji, ninaweza kumuita Dangote kama ‘Game Changer’ yaani ameleta mabadiliko kwa wazalishaji wengine waliokuwa wamelala waamke,” alieleza Mwijage.
Alisema Serikali imejiwekea mikakati ya kuhamasisha uwekezaji na wamepewa maelekezo kuhakikisha wanawavutia wawekezaji ili washiriki kwenye ujenzi wa uchumi na kujenga uchumi wa viwanda.
“Sisi tunawalenga wawekezaji wa ndani na nje katika kufanya kazi hizo, tunafuata maandiko matakatifu hivyo hatutakubali hata mmoja apotee tutawaacha 99 tushughulike kumtafuta mmoja,” alisema na kuongeza kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja cha Serikali ya Awamu ya Tano, takwimu zinaonesha kwamba hali ni nzuri na kumekuwepo na ongezeko la uwekezaji kutoka nje katika sekta ya nishati, ujenzi wa majengo, viwanda vya kuchakata, kilimo, usafirishaji, mawasiliano, maliasili na sekta ya huduma.
Alisema wanaolalamika waende katika wizara yake kwani katika suala la Dangote wameibuka watu wanamsemea ilhali kampuni hiyo ilitoa taarifa kwa maandishi wizarani kwamba uzalishaji umesimamishwa kwa sababu za kiufundi.
Alisema serikali haijabadilisha vivutio vilivyowekwa, isipokuwa sheria inayosimamiwa ni ya mwaka 2014 iliyohusisha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) baada ya kutokea malalamiko kwamba kila kitu kinatolewa bure.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Kapulya Msomba alisema bei elekezi ya gesi inayopendekezwa na TPDC lazima ipitishwe na Mamlaka ya ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na bei ambayo inauzia gesi hiyo ni dola 5.14 huku Dangote akitaka kuuziwa kwa Dola 4.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!