Thursday, 22 December 2016

Miili 7 iliyookotwa Mto Ruvu bado utata

KITENDAWILI cha vifo vya watu saba ambao miili yao ilikutwa kwenye mifuko ya sandarusi katika kingo za Mto Ruvu wilayani Bagamoyo, Pwani, hakijateguliwa kwa kuwa Polisi bado inaendelea na uchunguzi.


Wakati Polisi ikichunguza miili hiyo, baba mzazi wa Mkuu wa Idara ya Utafiti na Sera wa Chadema aliyetoweka katika mazingira ya kutatanisha, Ben Saanane, Fokasi Saanane ameiomba serikali kuonesha jitihada za dhati za kumtafuta mwanawe, ili kuiweka familia yake katika mazingira ya amani huku akieleza kutamani kusikia kauli ya Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe ambaye mwanawe alikuwa msaidizi wake.
Hata hivyo, hivi karibuni Chadema ilizungumza kuhusu Saanane na kuitaka Serikali kupitia vyombo vyake vya dola kuhakikisha mtumishi huyo wa Chadema, makao makuu, anajulikana alipo.
Saanane alitoweka Novemba 14, mwaka huu. Miili ya watu saba Kuhusu miili ya watu saba, Polisi imefafanua kuwa kabla ya miili kuzikwa, utaratibu wa uchunguzi wa awali ulifanyika, ukiwahusisha daktari na polisi kufika eneo la tukio na kukagua maiti kabla ya kuzikwa huku mwili mmoja ukipelekwa hospitali kwa uchunguzi zaidi.
Jeshi hilo bado linaendelea na jitihada za kutambua maiti hizo, ambazo hadi sasa hazijatambulika na pia kujua kilichowasibu na watu waliofanya kitendo hicho. Hayo yalielezwa na Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Robert Boazi wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Jeshi hilo, jijini Dar es Salaam.
Alisema baada ya kupata taarifa za kuonekana kwa miili hiyo, polisi pamoja na madaktari walikwenda eneo la tukio na kufanya uchunguzi wa kitaalamu na baada ya uchunguzi huo, miili sita iliamriwa izikwe hapo hapo kutokana na kuharibika sana.
Alisema maiti hiyo ilikaa katika hospitali hiyo hadi Desemba 16, mwaka huu ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, ilichukua jukumu la kuizika maiti hiyo.
“Aliyekufa maji hasa kama ni muda mrefu huwezi hata kuisogelea na ndio sababu ya msingi wale sita wakazikwa pale na ndio sababu ya msingi yule mwenye nafuu ulichukuliwa kwenda kufanyiwa uchunguzi,” alisema.
Kuhusu Saanane Kuhusu Saanane, Boazi alisema bado wanaendelea na uchunguzi wa taarifa za kupotea kwa Ben Focus, maarufu kama Saanane, ambaye taarifa zake za kupotea ziliripotiwa Desemba 5, mwaka huu na mtu aliyejitambulisha kama rafiki yake.
Boazi alisema baada ya taarifa hizo kuripotiwa, jalada la uchunguzi lilifunguliwa na taratibu zote za kiupelelezi zinazohusu mtu aliyepotea, zilifuatwa na kwamba bado upelelezi unaendelea.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Willbrod Mutafungwa, amesema uchunguzi uliofanywa kuhusu mwili uliookotwa katika eneo la Uru Ongoma, umebainika ni wa Steven Kimario (55), mkazi wa Sanya Juu wilayani Siha, na si wa Ben Saanane, kama inavyoripotiwa katika mitandao ya kijamii.
Mutafungwa alitoa taarifa hiyo jana mbele ya waandishi wa habari, ambapo alisema uchunguzi wa polisi umebaini kuwa dada wa marehemu, Anitha Kimario na mume wake aliyetambulika kwa jina moja la Rasi, wote wakazi wa kata ya Miembeni Manispaa ya Moshi, ndio wanaotuhumiwa kwa mauaji hayo ya kikatili.
Akielezea mazingira ya tukio hilo, Mutafungwa alisema watuhumiwa hao mara baada ya kutekeleza tukio hilo, walitoweka katika eneo la tukio. Kwamba mwili wa marehemu uliokotwa Desemba 15, mwaka huu eneo la Uru Ongoma Kata ya Uru Kaskazini, baada ya polisi kupata taarifa kutoka kwa raia wema.
“Uchunguzi uliofanywa kuhusu mwili uliookotwa katika eneo la Uru Ongoma si wa Ben Saanane, kama ambavyo imekuwa ikiripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari kwani uchunguzi umebaini kuwa ni mtu aitwaye Steven Kimario (55) ambaye aliuawa kwa kupigwa na dada yake kwa madai ya kufanya jaribio la kumbaka mtoto wa dada yake wa umri wa miaka tisa,” alidai Kamanda Mutafungwa.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!