Monday, 26 December 2016

Kipindupindu chaua watu 7 Dodoma


MGANGA Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Charles Kiologwe amewataka wananchi wa mkoa wa Dodoma kuchukua tahadhari, kutokana na kuibuka kwa ugonjwa wa kipindupindu ambapo mpaka sasa watu 329 wameugua na kusababisha vifo vya watu saba. Alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari juu ya kuendeshwa kwa kampeni ya ‘Ondoa kipindupindu mkoa wa Dodoma’ ambayo imeonesha mafanikio makubwa.



 Alisema ugonjwa wa kipindupindu katika mkoa wa Dodoma ulianza Oktoba 24 mwaka huu ambapo wilaya nne kati ya saba za mkoa zilikuwa na wagonjwa. Aliitaja wilaya ya Mpwapwa ndio iliyoongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi ambapo ilikuwa na wagonjwa 208 kati ya wagonjwa 329 waliokuwepo mkoa wa Dodoma, huku wagonjwa wengine wakitoka wilaya ya Kongwa, Chamwino na Manispaa ya Dodoma na kukiwa na vifo saba mkoa mzima. “Wananchi wanatakiwa kuchukua tahadhari mbalimbali na kumeanzishwa kampeni ya kutokomeza kipindupindu mkoa wa Dodoma,” alisema. Alisema kampeni hiyo itaendeshwa kuanzia ngazi ya kijiji ambapo msimamizi atakuwa mwenyekiti wa kijiji na katika ngazi ya kata msimamizi atakuwa ni diwani. “Kwenye kaya atakuwa mkuu wa kaya na kwenye wilaya ni mkuu wa wilaya, lengo ni kuondoa ugonjwa wa kipindupindu na kuzuia ugonjwa huo,” alisema. Dk Kiologwe alisema hali ya uchafu katika minada mingi imekuwa ikichochea kuibuka na kuenea kwa ugonjwa huo. “Minada inazuiwa ili kuimarisha usafi maeneo ya biashara hata upikaji na unywaji wa pombe za kienyeji umekuwa hauzingatii kanuni za usafi. Katika baadhi ya maeneo upatikanaji wa maji safi na salama umekuwa ni shida kubwa,” alisema. Alisema jukumu kubwa la serikali kwenye kata ni kutengeneza kamati ambayo itaratibu shughuli zote. “Ifikapo Januari mwakani tunataka kusiwepo kwa mgonjwa hata mmoja wa kipindupindu, kuna wakati kulikuwa na wagonjwa 10 hadi 14 kwa siku lakini baada ya kampeni ya kutokomeza kipindupindu kuanza kwa siku kuna wagonjwa wawili au hakuna kabisa,” alisema. Alisema awali ilibainika zaidi ya asilimia 60 ya wagonjwa wanatoka maeneo ya Kilosa lakini hilo likadhibitiwa na sasa wagonjwa wengi wakaonekana kutoka eneo la Pwaga Wilaya ya Mpwapwa. Akizungumza hivi karibuni, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Christina Mndeme alisema watu wawili wamefariki dunia wiki iliyopita huku wengine wanane wakiwa wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kutokana na kuugua ugonjwa huo. Aliwataka wananchi kuhakikisha chakula wanachokula kinakuwa safi, kuacha kutupa taka ovyo, mji kuwa safi na watu wote wanaouza chakula wahakikishe wanakiuza katika mazingira ambayo ni safi, kunawa mikono kabla ya kula na wakati wa kuandaa chakula.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!