Saturday, 10 December 2016

Kifo cha mchezaji wa Mbao kiiamshe TFF


MATUKIO ya kuanguka na kufa uwanjani kwa wanamichezo siyo geni duniani. Zipo sababu mbali mbali zimekuwa zikitolewa za kutokea kwa matukio hayo ya kusikitisha.



 Miongoni mwa wanamichezo walioanguka na kupoteza maisha uwanjani ni Marc Vivien Foe, kiungo wa timu ya taifa ya Cameroon mwaka 2003 aliyepatwa na mkasa huo alipokuwa akiichezea timu yake dhidi ya Colombia, pia Patrick Ekeng aliyefariki dunia Mei 6, 2016 aliyedondoka wakati wa mechi dhidi ya FC Viitorul Constanta, ikiwa ni dakika ya saba baada ya kuingia akitokea benchi alimbikizwa hospitali lakini alifariki muda mchache baadaye.

Kwa mujibu wa mtandao wa afya wa Healthline.com, vifo vya aina hiyo vinasababishwa na mapafu au moyo kushindwa kufanya kazi ghafla, kukosekana kwa hewa ya oksijeni kufika kwenye mapafu. Kitaalamu pia, inaelezwa upungufu wa mtiririko wa damu kwenye ubongo husababisha mtu kuzimia au kuanguka na kupoteza maisha. Mwishoni mwa wiki iliyopita, tasnia ya soka ilikumbwa na simanzi kubwa baada ya kumpoteza mchezaji wa timu ya vijana ya chini ya umri wa miaka 20 ya Mbao, Ismail Khalfan kuanguka uwanjani na kufariki dunia. Ismail amezikwa Jumatatu ya wiki hii kwenye makaburi ya Ilemela Mwanza. Tukio hilo lilitokea katika michuano ya ligi ya vijana chini ya umri wa miaka 20 (U20) ambayo fainali zake zitafanyika kesho kwenye uwanja wa Azam Complex Chamazi. Michuano hiyo ilizinduliwa rasmi Novemba 15 mwaka huu kwa mchezo maalumu kati ya Yanga na Kagera Sugar. Ligi hiyo ilikuwa na vituo viwili ambavyo ni Dar es Salaam na Bukoba ambapo kwa upande wa Dar ilishirikisha timu za JKT Ruvu, Simba, Ruvu Shooting, Ndanda, Majimaji ya Songea, Mtibwa, Mbeya City na Tanzania Prisons. Kituo cha Bukoba mkoani Kagera kulikuwa na timu za Azam, African Lyon, Mbao FC, Toto Africans, Mwadui ya Shinyanga kama ilivyo Stand United, Kagera Sugar na Yanga. Hata hivyo dosari kubwa katika michuano hiyo ni ukosefu wa huduma ya kwanza uwanjani ikiwemo gari la wagonjwa. Kwa mujibu wa kanuni za mashindano yoyote, moja ya mambo yanayotakiwa kuwepo uwanjani wakati mechi ikichezwa ni magari ya polisi, wagonjwa na ya zimamoto ambayo yanapaswa kuwepo uwanjani kabla ya watazamaji na mashabiki wa timu kuingia uwanjani. Magari ya wagonjwa ni kwa ajili ya kubeba watu wanaoumia ama wachezaji wanaoumia mchezoni, Polisi kazi yao ni kulinda usalama wa watazamaji (mashabiki na wapenzi) wa soka lakini pia gari la zimamoto ni kwa ajili ya kuzima moto na majanga uwanjani ni muda wote wa mchezo na baada ya mchezo pindi ikitokea dharura. Katika ligi hiyo, mwandishi wa makala haya ameshuhudia gari la zimamoto likiwa uwanjani hapo huku gari la wagonjwa ‘Ambulance’ likikosekana uwanjani hapo tangu kuanza kwa michuano hiyo. Katika mchezo huo ambao kiungo Khalfan alipoteza maisha, ulihusisha timu ya Mbao dhidi ya Mwadui ambao Mbao ilishinda mabao 2-0, bao la kwanza likifungwa na mshambuliaji Khalfan na muda mfupi baadaye aligongana na beki wa Mwadui na kuanguka chini na kupoteza maisha. Taarifa kutoka jopo la madaktari la TFF zinasema mchezaji huyo alipata shambulio la moyo kali lililochukua uhai wake. Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Chama cha Soka Ilemela, Evarist Hagila anasema “Katika tukio hili TFF wanaweza kuwa na majibu, tukio limetokea watu wa huduma ya kwanza waliingia na kusaidia lakini hakukuwa na gari la kubeba wagonjwa, likatumika gari ya zimamoto, hii si sahihi, TFF ijifunze kutokana na tukio. “Nakumbuka kwenye udhamini wa Mbao pale TFF waandishi walilalamikia sana kuhusu kukosekana kwa huduma ya kwanza lakini majibu yalikuwa ni ya juu juu tu, na ndani ya saa 48 tukio kubwa kama hili lilitokea… “Mfano FIFA walitoa mashine ya kushtua moyo kama mchezaji akizimia, hatujui hiyo mashine kama ipo au haipo na haijawahi kutumika hata kwa majaribio, hili liwe fundisho, TFF wana madaktari wasomi kupitia tukio hili wajifunze. “Chama cha Soka Ilemela hatujafurahi kitendo cha mchezaji wetu kuwekwa kwenye gari za zimamoto, tumeumia na tumesikitika sana,” alisema. Katika mkutano wa waandishi wa habari, Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas alipoulizwa kuhusu kukosekana kwa huduma ya kwanza kwenye ligi hiyo ya vijana anajibu: “Ndio maana kunakuwa na kikao cha maandalizi ya mechi kama hakuna huduma ya kwanza timu zinapaswa kugoma kwani hilo lipo kisheria na kamisaa wa mchezo anapaswa kulieleza hili kwenye ripoti yake, lakini kitendo cha kucheza ni kwamba zimeridhika,”. Kukosekaa kwa huduma ya kwanza si kwa ligi ya vijana tu, hata kwa baadhi ya mechi za Ligi Kuu, kwa mfano katika mchezo wa Ligi Kuu mzunguko wa kwanza kati ya Ndanda na Toto Africans, mchezaji Brayson Raphael wa Ndanda aliumia na kulazimika kutolewa nje akagangwa na daktari wa timu na ilipoonekana anahitajika kupelekwa Hospital likaitwa gari kumchukua ambalo halikuwa na alama kuonyesha ni la wagonjwa, halikuwa na daktaroi wala muuguzi ndani yake zaidi ya askari wa kikosi cha zimamoto na machela. Kwa uzoefu madereva wengi wa Tanzania ni wagumu kupisha njia gari lililobebwa mgonjwa pasipo kuwa na alama ya kuonyesha, maana inakuwa si rahisi kujua kama gari limepakia mgonjwa. “Niliwahi kushuhudia gari la zimamoto likiligonga gari moja binafsi baada ya kung’ang’ania barabarani bila kulipisha gari hilo ambalo lilikuwa likiwahi kwenye tukio la moto, itakuwa vipi gari la wagonjwa lisilo na nembo wala wataalamu kuweza kupishwa njia na madereva wetu ili kuwahi kumkimbiza na kumfikisha majeruhi hospitali kwa haraka,” anasisitiza Hagila. Kukosekana kwa gari la wagonjwa ni hatari kwa wachezaji na watazamaji ukizingatia lolote linaweza kutokea uwanjani na inaonyesha viongozi wetu wapo kwa maslahi binafsi wanapodai kuwa hawana fedha za kukodi gari la wagonjwa.. Hili liwe funzo ili madhara zaidi yasitokee siku zijazo.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!