Wednesday, 14 December 2016

Inawezekana Tanzania kuuza mchele nje?

Shamba la kisasa la mpunga lililopo Dakawa mkoani Morogoro.
KILIMO cha mpunga kimeendelea kuwa muhimu kwa uchumi wa nchi.
Ni miongoni mwa vyanzo vikubwa vya chakula, ajira na kipato kwa familia nyingi za wakulima na wafanyabiashara vyakula. Mchele ambao hutokana na mpunga ni zao la pili muhimu la nafaka hapa nchini baada ya mahindi. Tanzania inatajwa kuwa ni mzalishaji mkubwa na wa pili baada ya Madagascar kwenye ukanda wa Mashariki na Kati katika uzalishaji wa zao hili.


Taarifa hiyo inatolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Florens Turuka (sasa Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) kwenye uzinduzi wa warsha ya kuzindua mradi wa ubia wa kuboresha mifumo ya uzalishaji wa kilimo cha mpunga Afrika. Katika warsha hiyo ya hivi karibuni mjini Morogoro, Dk Turuka anabainisha kwa kusema kuwa, takwimu za uzalishaji mpunga zinaonesha kuwepo ongezeko katika kipindi cha miaka sita iliyopita.
Ongezeko hilo ni kutoka tani 1,699,825 mwaka 2009/2010 hadi kufikia tani 1,936,909 mwaka 2014/2015 sawa na ongezeko la asilimia 14. “ Katika kipindi chote hicho, kiwango cha uzalishaji wa mpunga kimekuwa kikubwa kuliko mahitaji,” anasema Dk Turuka. Taarifa hiyo ya serikali inasema, mbali ya mafanikio bado zipo fursa nyingi za kuongeza uzalishaji wa mpunga hapa nchini. Eneo ambalo lipo kwenye kilimo hiki bado ni dogo ikilinganishwa na eneo lote lililopo hapa nchini lenye sifa zote za kuweza kutumika kwa kilimo hiki.
Mfano unaotolewa ni kwamba, mpaka kufikia mwaka 2007/08, ni hekta 664,667 pekee kati ya milioni 21 zinazofaa kwa kilimo cha mpunga nchini ndizo zinatumika kwenye kilimo hiki. “Hii ina maana kuwa ardhi nyingi bado haitumiki ipasavyo na hivyo kuinyima nchi fursa ya kulima mpunga kwa wingi na kuweza kuuza nje ya nchi baada ya kutosheleza mahitaji ya ndani” anasema Dk Turuka.
Katika kuelezea umuhimu wa zao hili, katibu mkuu huyo anasema, linaweza kuwa chanzo kikubwa sana cha fedha za kigeni ikiwa uzalishaji utaongezwa hivyo kuwezesha nchi kuuza nje ikizingatiwa kuwa mahitaji yake yanaongezeka. Uwapo wa vyanzo vingi vya maji kama vile mito, maji ya chini ya ardhi, maziwa, unapaswa uwe kichocheo cha uzalishaji wa zao hili kupitia umwagiliaji.
Hata hivyo, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi inabainisha kwamba, pamoja na mafanikio na fursa hizo, bado zipo changamoto mbali mbali zinazokabili kilimo cha mpunga. Hii inatokana na ukweli unaoelezwa na mtendaji huyo aliyekuwa kwenye wizara hiyo yenye dhamana na kilimo kwamba, pamoja na kwamba nchi imekidhi mahitaji ya ndani na kupata ziada kidogo, bado kiwango cha uzalishaji ni kidogo ukilinganisha na wazalishaji wengine duniani.
Uzalishaji huu mdogo unachangiwa na sababu mbali mbali kama vile utegemezi mkubwa wa mvua, matumizi madogo ya zana za kisasa za kilimo, kukosekana na matumizi madogo ya mbegu za kisasa. Pia matumizi kidogo ya mbolea, wakulima kutotumia mbinu za kisasa za uzalishaji na uhaba wa maeneo yenye kuweza kutumika kwa kilimo cha umwagiliaji ni changamoto zinazokwamisha uzalishaji kwa kiwango kikubwa.
Uingizwaji kimagendo wa mchele kutoka nje pia ni tatizo uzalishaji wa mchele nchini kutokana na kuwanyang’anya wazalishaji wa ndani soko. Kwa kuzingatia changamoto hizo, serikali imechukua hatua kadhaa kuzikabili kuboresha uzalishaji wa mpunga nchini. Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kuhakikisha uzalishaji na upatikanaji wa mbegu bora, upatikanaji wa pembejeo za kilimo, uboreshwaji na upanuzi wa skimu za umwagiliaji kwa kushirikiana na halmashauri.
Mafunzo ya kilimo pamoja na huduma za ugani ni eneo lingine ambalo serikali inasema inafanyia kazi kuwezesha uzalishaji wenye tija. Mikakati hii inatekelezeka kupitia miradi mbali mbali. Mfano, serikali kununua na kutoa zana za kisasa za kilimo kama vile mashine za kuvuna, kupura na kukata mpunga sehemu mbali mbali hapa nchini. Wizara kupitia kwa Dk Turuka inasema, moja ya mwitikio wa mahitaji ya kuongeza uzalishaji wa mpunga umetokana na juhudi za Jumuiko la Maendeleo ya Uzalishaji Mpunga Afrika (CARD).
Mkakati wa Taifa wa Maendeleo ya Kilimo cha Mpunga (NRDS) mwaka 2009 umeridhiwa. Mkakati huo unaendana na sera pamoja na makubaliano mbalimbali ya kimataifa na chini ya mpango wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO). FAO imeendelea kushirikiana na serikali katika kutekeleza miradi mbali mbali nchini, ukiwemo mradi wa ubia wa kuboresha mifumo ya uzalishaji wa kilimo cha mpunga Afrika.
Dk Turuka anasema, mradi wa ubia wa kuboresha mifumo ya uzalishaji wa kilimo cha mpunga Afrika unafadhiliwa na Serikali ya Venezuela na umekuja wakati muafaka. Hivyo mradi huu unatajwa kuwa, umekuja wakati ambao Tanzania kama nchi imenuia kuongeza maradufu uzalishaji wa mpunga.
Pia mradi huo utaongeza uelewa wa wakulima juu ya matumizi ya mbegu zilizoboreshwa, kutoa mafunzo ya kilimo cha umwagiliaji, kuwapatia wakulima pembejeo na zana za kilimo, na kuwapa mafunzo ya namna bora ya kutunza mazao yao baada ya kuvuna. Mwakilishi FAO nchini, Fred Kafeero, anasema miradi kama hiyo pia inatekelezwa katika nchi nyingine tisa za Afrika. Nazo ni Benin, Cameroon, Ivory Coast, Guinea (Conakry), Kenya, Mali, Nigeria na Senegal.
Kafeero anasema, FAO, Umoja wa Afrika (AU) na Benki ya Maendeleo ya Afrika na wadau wengine wametambua mchele kuwa kipaumbele kimkakati cha mazao makuu kwa nchi kama sehemu ya jitihada za kutekeleza ajenda ya Malabo kwa kutokomeza njaa Afrika ifikapo mwaka 2025. Anasema, hakuna sababu ya kuifanya Tanzania isiwe miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa mpunga kutokana na kujaliwa kuwa na ardhi yenye rutuba , maji mengi ya mito, mabonde na maziwa tofauti na nchi nyingine za Afrika.
Kafeero anasema mradi huo mpya umelenga kusaidia juhudi za serikali kuongeza uzalishaji wa mchele na tija kuweza kupanda mara mbili ya sasa ifikapo mwaka 2018 kupitia kilimo cha wakulima wadogo. Mradi huo umelenga katika skimu za umwagiliaji zilizomo mkoani Morogoro ambazo ni Mvumi, Msolwa Ujamaa, Ilonga, Njage , Kigugu, Mbogo-Komtonga ambazo zipo katika wilaya za Kilosa, Mvomero na Kilombero.
Pia utaanzisha madarasa ya wakulima wadogo ya umwagiliaji kwa kutumia skimu hizo na namna ya kuendesha na uzalishaji wa zao la mpuga kwa njia ya kisasa. Zitanunuliwa mashine za kusindika mpunga kwa lengo la kuongeza thamani. Masoko pia yataboreshwa, maghala yatajengwa, zitanunuliwa mashine za kuvunia ili kupunguza hasara ya upotevu wa chakula shambani.
Wakulima wa mpunga kwa njia ya umwagiliaji katika Kijiji cha Mkindo kilichopo Kata ya Hembeti, wanaeleza kuridhishwa na mikakati inayofanyika kuleta tija katika kilimo cha zao hili. Hassan Juma, ambaye ni mkazi wa kijiji hicho, anasema miradi ya kilimo cha umwagiliaji ni faraja kwao kwani inaongeza uzalishaji wenye tija.
Wakati mikakati hii ikileta matumaini kwa wakulima, ni changamoto kwa serikali kuhakikisha haibaki kuwa nadharia, bali inatekelezwa kwa vitendo na kuiwezesha Tanzania inazalisha kwa kiwango kikubwa, inajitosheleza kwa soko la ndani na kisha kuuza mchele nje ya nchi.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!