Monday, 28 November 2016
WATUMISHI Waliosoma Vyuo Vikuu Bila Sifa Kufukuzwa Kazi
Baada ya matamko kadhaa kadhaa ya serikali kuhusu Sekta ya Elimu nchini hatimaye leo limeibuka jingine la kutimua watumishi wote wa umma waliojiunga na vyuo vikuu na kutunukiwa "degree" bila kuwa na sifa.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Elimu Prof.Joyce Ndalichako wakati akifungua maonesho ya vyuo vya elimu ya juu yaliyoandaliwa na Tume ya Vyuo vikuu nchini (TCU) yanayofanyika viwanja vya Karimjee, jijini Dar.
Maonesho hayo yanashirikisha vyuo 61 ambapo 12 kati ya hivyo ni kutoka nje ya nchi.
Katika taarifa yake Ndalichako amesema Wizara yake inawasiliana na idara ya Utumishi ili kuwabaini watumishi wote waliojiunga vyuo vikuu bila sifa na wafukuzwe kazi. "Kama wewe ni mfanyakazi uliyesoma moja ya vyuo vikuu ukafaulu lakini hukuwa na sifa ya kujiunga na chuo kikuu, tutakunyofoa hukohuko kwenye ajira yako" Alisema Ndalichako.
Kufuatia agizo hilo la Ndalichako, watumishi wote waliosoma vyuo vikuu kwa kupitia foundation courses kama Pre Entry/Remidial/Certificates, etc,wataondolewa kazini. Ndalichako amesema Foundation course haimuongezei mtu sifa ya kusoma degree. Amesema kuwa kama mtu hakupata points za kumuwezesha kujiunga chuo kikuu hata asome foundation course bado hatapata sifa, namna pekee ya kupata sifa ni kurudia mtihani wa kidato cha sita.
Agizo hilo pia litawagusa watumishi waliojiunga na elimu ya juu kwa ufaulu linganishi (equivalent pass) ambapo kwa wale waliotoka diploma na wakasoma degree bila kufikisha GPA iliyowekwa na NACTE watatimuliwa. Pia waliotoka kidato cha sita na kupata nafasi vyuo vikuu moja kwa moja lakini hawakufikisha "cut off points" zilizowekwa na TCU wataondolewa katika ajira zao.
Prof.Ndalichako amesema zoezi hilo litaanza baada ya kumaliza zoezi la uhakiki wa sifa kwa wanafunzi wanaopata mikopo. "Tukimaliza hawa wanaopata mikopo, tutahamia wasiopata mikopo kuona kama wana sifa za kusoma vyuo vikuu, baadae kwa wafanyakazi. Hata kama hukupata mkopo, lakini ulisoma chuo kikuu bila sifa hauko salama" Alisisitiza Ndalichako.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment