Friday, 11 November 2016

UTI inavyowatesa wanawake, watoto


MAAMBUKIZI katika njia ya mkojo (Urinary Tract Infection) ni ugonjwa ambao unawasumbua wanawake wengi na watoto katika nchi nyingi zinazoendelea. UTI huathiri mfumo wa mkojo ikiwa ni pamoja na ureter ambayo ni kama bomba linalosafirisha mkojo kutoka kwenye figo, pia kibofu cha mkojo na urethra.


Ugonjwa huu unaathiri zaidi kibofu cha mkojo na urethra, lakini unaweza pia kuathiri figo. Maambukizi haya yakiathiri sehemu za chini za kibofu cha mkojo kitaalamu huitwa simple cystitis au bladder infection, na maambukizi hayo yakitokea sehemu za juu za mfumo wa mkojo huitwa pylonephritis au kidney infection.
Ugonjwa huu husababishwa na bakteria anayeitwa Escherichia coli (E. coli) na tatizo hili husababishwa kwa kiasi kikubwa na bakteria ambao makazi yao ya kawaida ni kwenye utumbo mpana, na hivyo huwa wanapatikana pia kwenye haja kubwa.
Lakini baadhi ya watu wanaweza kupata tatizo hili kutokana na kuingiwa na fangasi ingawa pia zipo sababu nyingine chache.
Bakteria wa Escherichia coli hawasababishi peke yao UTI bali huambatana na wengine waitwao staphylococcus, saprophyti cus, pseudom onas, enterobacter na kadhalika.
Maambukizi katika njia ya mkojo lazima yawe ni kwenye njia ya mkojo na si pengine popote.
Tunapozungumzia maambukizi katika njia ya mkojo, inamaanisha ni kutoka eneo la nje ya utupu hadi kwenye kibofu na kutoka kwenye kibofu hadi kwenye figo.
Wataalamu wa afya wanabainisha kuwa, mara nyingi maambukizi haya kwa wanawake husababishwa na kutojisafisha vizuri na kuvaa nguo za ndani zilizo chafu.
Pia huweza kusababishwa na matumizi ya taulo za kike zenye kemikali ya kukata harufu ambazo huua bakteria wa asili wa eneo la uke na kuwapa fursa bakteria wanaosababisha maradhi kuzaliana kwa wingi.
Pia upungufu wa homoni ya wanawake iitwayo oestrogen husababisha bakteria wanaosababisha maambukizi katika njia ya mkojo kuzaliana kirahisi sambamba na matumizi ya baadhi ya dawa kwa muda mrefu, unywaji wa vinywaji vyenye sukari kwa muda mrefu na kutokunywa maji ya kutosha.
Uwepo wa mawe katika figo na mirija ya figo, pia ni mojawapo ya chanzo cha maambukizi haya katika njia ya mkojo na matumizi ya maji machafu wakati wa kujisafisha au kuoga ambayo huweza kuweka bakteria kwa urahisi na kusababisha mwanamke kupata ugonjwa huo.
Uchafu wa vyoo umetajwa kuwa sababu nyingine, kwani matumizi ya vyoo ambavyo ni vichafu huweza kusababisha mwanamke kupata UTI kwa sababu ndani ya choo kuna bakteria wengi ambao wanaweza kusababisha ugonjwa huo.
Mambukizi ya UTI licha ya kuwapata zaidi wanawake, huwakumba pia watoto wadogo wa kike kutokana na sababu za kimaumbile ambapo viungo vyao vya uzazi, njia ya mkojo na haja kubwa vipo jirani.
Watoto wa kiume na watu wazima ambao hawajatahiriwa nao huweza kupata maambukizi rahisi ya UTI iwapo watajisafisha kwa kutumia maji yasiyo salama ambapo huwa rahisi kwa bakteria kubaki katika ngozi inayoning'inia.
Maambukizi yanayoshambulia mfumo wa mkojo husababishwa zaidi na bakteria wanaoishi katika mfumo wa haja kubwa kwa kuingia na kujikita katika mfumo wa mkojo. Baadhi ya dalili za mtu kuambukizwa bakteria katika njia ya mkojo kubwa ni maumivu wakati wa kukojoa, mkojo kuwa na rangi ya njano kupindukia na kuwa na harufu kali ijapokuwa siyo kila mwenye dalili hizo ana maambukizi katika njia ya mkojo.
Dalili nyingine ni maumivu, kutokwa na usaha wakati wa kukojoa, kabla au baada ya kukojoa ukiambatana na maumivu na kuhisi moto wakati mkojo ukitoka, kupata vichomi katika njia ya mkojo, kuumwa kiuno au tumbo.
Mgonjwa pia anaweza kukumbwa na homa kali mara kwa mara na mwili kuwa mchovu, kwa watoto hupoteza hamu ya kula na mwili huonesha kuchoka. Wagonjwa wengine hupata maumivu kwenye kibofu cha mkojo ambapo husikia maumivu ya chini ya tumbo usawa wa kitovu na huwa hayaishi.
Matatizo haya ya mfumo wa mkojo kama tulivyoona kabla huwapata watu wote wanawake na wanaume. Watu wenye matatizo haya kila wakipima huambiwa wana UTI. Kwa wanaume huhisi hata nguvu za kiume kupungua na wanawake hupoteza hamu ya tendo la ndoa.
Kwa wajawazito ugonjwa unaweza kuhatarisha maisha yao na mtoto aliye tumboni. Bakteria wanaweza kuingilia mfumo wa damu na kusababisha madhara mengine kama vile shinikizo la damu kuwa kubwa kwenye figo na hata kusababisha ufanyaji kazi mbovu wa figo.
Madaktari wanabainisha kuwa UTI inaweza kudhibitiwa au kuponya kwa kunywa maji mengi pamoja na juisi itokanayo na matunda halisi, iwapo tutawahi kabla tatizo halijawa sugu.
Kwa maana nyingine, unaweza kujikinga na ugonjwa huu kwa kuwa na mazoea ya kunywa maji ya kutosha kila siku. Ukinywa maji ya kutosha yatakufanya uende haja ndogo kila mara na kwa njia hiyo wale bakteria watakuwa wakitoka na hatimaye kuisha kabisa. Makala haya yameandaliwa kwa msaada wa mitandao ya afya.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!