KAIMU Balozi wa Marekani nchini, Virginia Blaser amesema virusi vya Ukimwi (VVU) havijaisha nchini na Watanzania hawapaswi kubweteka kwa mafanikio ambayo yamepatikana, badala yake waongeze nguvu kuhakikisha hakuna maambukizi mapya yanayotokea nchini.
Ameyasema hayo jana wakati wa ziara yake katika Shirika la Vijana la kupambana na Ukimwi (Tayoa) lililopo Dar es Salaam, ambapo pia alizindua huduma ya simu za afya bure kupitia namba 117.
Ameongoza mjadala kuhusu namna unyanyasaji wa kijinsia unavyoweza kuchangia maambukizi ya VVU.
“Suala la kupambana na Ukimwi si la mtu, si la asasi binafsi wala serikali pekee bali la kila mmoja wetu, tunajua kwamba ugonjwa huu bado upo na ili tufanikiwe kuutokomeza kabisa lazima tuunganishe nguvu zetu wote ili tuweze kufikia malengo ya kuondoa kabisa maambukizi,” alisema.
Alisifu Tayoa kwa kuanzisha huduma ya simu za bure ambapo alisema kwa njia hiyo watanzania wengi watanufaika kwa kupiga simu bila malipo na kujua hali za afya zao. Kauli mbiu ya siku ya Ukimwi mwaka huu inasema ‘bado hatujafika mwisho’ na inasema malengo hadi kufikia mwaka 2020 asilimia 90 ya watu wawe wamepima kujua kama wana VVU.
Pia ilieleza asilimia 90 ya watu wenye VVU wawe kwenye matibabu ifikapo mwaka huo na asilimia 90 ya wanaotumia dawa wawe wamepunguza kiwango cha maambukizi ya VVU mwilini mwao.
Mkurugenzi wa Tayoa, Peter Masika, alisema kwa miaka minane sasa, kuanzia mwaka 2008 hadi 2016, shirika la PEPFAR limeisaidia Tayoa, zaidi ya watu 4,800,000 wamefikiwa kwa kupitia simu ya afya ya 117 na wamefanikiwa kutuma zaidi ya ujumbe 23,000,000 wa kuelimisha kuhusu Ukimwi.
No comments:
Post a Comment