Wednesday, 26 October 2016

Ziko wapi helmeti za watoto?

KWA jinsi usafiri ulivyo shida katika katika baadhi ya maeneo, wanafunzi wamekuwa wakichelewa kufika shuleni kutokana na kusoma mbali na yalipo makazi yao. Usafiri wa pikipiki maarufu kama bodaboda unaonekana kama ndio mkombozi wa kuwawahisha wanafunzi kufika huko mashuleni.


Lakini, wanafunzi hao ambao wengi ni watoto, wamekuwa wakilazimika kupanda bodaboda ili kuwahi shuleni, bila kukamilisha masharti ya kuvaa kofia ngumu, yaani helmeti. Mwendesha pikipiki pamoja na abiria wake chini ya sheria ya usafirishaji ya Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) inatamka bayana kuwa lazima wavae helmeti ili kujizuia na ajali inapotokea.
Tafiti zilizopo zinaonesha kwamba mpanda pikipiki aliyevaa helmeti ana asilimia 60 ya kutoumia iwapo atapata ajali, hususani kichwani ambako huwa ni hatari kuweza kumsababishia mhusika kifo.
Kando ya shule ya msingi ya Blessed Hill, mwendesha pikipiki mmoja anayejitambulisha kwa jina la Charles Magige aliyekuwa amebeba wanafunzi wawili kwenye pikipiki yake kwa mtindo unaoitwa mshikaki, abiria wake hao hawakuwa wamevaa kofia. Anapoulizwa kwa nini watoto hao hawana helmeti, anajibu:
"Sina helmeti ya watoto. Nina kofia kwa ajili ya watu wazima tu," anasema Magige. Ninapomuuliza kama ana mpango wa kununua hiyo kofia kwa kuwa baadhi ya wateja wake ni wanafunzi, anajibu: "Kwa kweli sijui kama kuna helmeti za watoto zinauzwa kwa hapa nchini. Sijawahi kuziona."
Magige ni miongoni mwa madereva wengi wa pikipiki ambao wameingia makubaliano na familia mbalimbali za jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kupeleka watoto wao shule na kuwarudisha nyumbani.
Pikipiki hizi zimeonekana msaada mkubwa kwa jamii kutokana na kuwawahisha watoto wengi mashuleni. Emanuel Sinda ni mzazi ambaye mtoto wake pia anasafirishwa na pikipiki kwenda shule. Yeye anasema hajawahi kufikiria kumnunulia mtoto wake helmeti, licha ya kutambua kwamba kupanda pikipiki kuna hatari kwa abiria ambaye hajavaa kofia ngumu.
"Lakini kwa mfano umnunulie helmeti, mtoto akishuka ataitunza wapi pale shuleni, yaani utunzaji wake naona kama ni shida," anasema Sinda na kuongeza: "Hapa mtaani kwetu watu wengi tu wanawapeleka watoto wao kwa pikipiki, lakini sioni hata mtoto mmoja ambaye anavaa helmeti, nadhani hata hizo helmeti za watoto hazipo hauko madukani." Sinda anashauri kwamba walimu ndio wanatakiwa kutoa elimu hiyo kwa watoto na wazazi.
"Naamini kwamba walimu wana jukumu la kutambua ni mtoto gani anaenda na pikipiki shuleni kwake, akishawatambua inakuwa rahisi kuwatumia wanafunzi hao kuwaita wazazi wao wawape elimu ya umuhimu wa watoto wao kutumia helmeti."
Katika eneo hili la helmeti za watoto, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanasheria Wanawake (TAWLA), Tike Mwambipile ambaye taasisi yake inapigania kuwepo kwa mabadiliko ya sheria za usalama barabarani anasema yeye haamini kumpakiza mtoto kwenye pikipiki kama ni jambo salama. Hata hivyo, anakiri kwamba kwa hali ilivyo ya usafiri katika miji mingi suala la kumpakia mtoto kwenye pikipiki halikwepeki ila anashauri jamii ipige kelele ili ziwepo helmeti za watoto madukani kwa wingi tofauti na ilivyo sasa.
"Tunashauri helmeti za watoto ziwepo nyingi lakini ziuzwe kwa bei ambayo ni affordable (bei rahisi)," anasema Mwambipile.
Anasema suala hilo la helmeti za watoto limekuwa linaleta mjadala mkubwa kwenye majadiliano yanayofanywa na asasi za kiraia kuhusu dereva wa bodaboda atakavyozibeba hizo helmeti za abiria wake wawili.
"Utakuta ana helmeti ya abiria mkubwa na sasa atalazimika awe na helmeti nyingine ya abiria mtoto, sisi tunaona kama itakuwa ni usumbufu, kwa nini tusije na sheria moja tu ambayo inakataza mtoto kubebwa kwenye bodaboda ili kuepusha matatizo kama haya.
Kama kuna ulazima ni bora wapande bajaji," anasema mkurugenzi huyo. Samson Chiganga ni mlezi wa wanafunzi wa shule ya msingi ya Heritage, Dar es Salaam.
Anakiri kuwa katika elimu ya jamii wanayoitoa kwa wanafunzi, suala la kutumia helmet halipo na hawajawahi kuwa na mpango wa kutoa elimu kwa watoto na wazazi. Mkurugenzi wa Asasi ya Global Helmet Vaccine Initiative (GHV I) inayoshughulika na uhamasishaji wa uvaaji wa helmeti, Alpherio Nchimbi, anasema kwa sasa hapa nchini hakuna maduka yanayouza helmeti za watoto, jambo ambalo limefanya watoto wengi kusafiri na pikipiki bila kuvaa vifaa hivyo.
"Mimi hapa ninayo kwa ajili ya mtoto wangu, lakini nilinunua nje ya nchi, kuna haja ya waagizaji kuhamasishwa kuagiza hizo helmeti za watoto kwani kuna mahitaji makubwa ya watoto wanaosafiri na pikipiki kwenda mashuleni," anasema Nchimbi. Pia anasema tatizo hilo litamalizika iwapo helmeti hizo za watoto zitatengenezwa hapa nchini. Anaishauri Serikali ifanye haraka kujenga kiwanda hichoa mbacho jeshi la Magereza limeonesha nia ya kukijenga.
"Kuna mpango wa kujenga kiwanda hapa nchini naamini hili la helmeti za watoto watalizingatia,"anasema Nchimbi. Katika duka la pikipiki za Yamaha ambao wanauza helmeti, muuzaji mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Judith anasema tangu waanze biashara hiyo miaka mingi iliyopita hawajawahi kuagiza helmet za watoto badala yake wamekuwa wanaagiza helmet za wakubwa tu.
"Kwa kweli hatuna hata huo mpango wa kuagiza hizo helmeti, na hatujui kama kuna soko," anasema Judith. Alipoulizwa kama mteja anaweza kuomba aagiziwe kwa ajili ya mtoto wake Judith alijibu:
"Labda mwaka ujao tunaweza kuanza kutoa hiyo huduma lakini kwa sasa hatuna mpango huo." Meneja wa kampuni ya Fear Deal Auto Co., Khalid Sefullah ambao wanauza pikipiki za Boxer anasema wanaagiza kofia za watu wakubwa tu na hawajahi kupanga kuagiza kofia kwa ajili ya watoto. "Hizo helmeti za watoto tutamuuzia nani, sisi tunaleta hizo za wakubwa tu ndizo zenye soko, za watoto hazina soko."
Naye daktari wa kitengo cha tiba wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Mariam Kalomo anasema ni bora kila mzazi anunue helmeti kwa ajili ya watoto wake ambao wanapelekwa shule na pikipiki. "Sio vizuri watoto kuchangia kofia, ni bora kila mtu anunue kofia na akae nayo ndani yake, tujenge tabia hiyo."
Takwimu za Taasisi ya Mifupa (MOI) ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili zinaonesha kwamba kuanzia mwaka 2015 abiria ambao ni majeruhi wa pikipiki waliofikishwa katika hospitali hiyo walikuwa 954 idadi ambayo inakaribia ya mwaka 2014 ambako abiria majeruhi walikuwa 949. Kwa upande wa watoto majeruhi ambao walifikishwa katika hospitali hiyo mwaka 2014 ambao walijeruhiwa kwa pikipiki walikuwa 618 na mwaka 2015 idadi iliongezeka na kufikia watoto 657.
Watoto hao kwa mujibu wa takwimu za MOI ni wale ambao wana umri kati ya miaka 1 hadi 10. Mwanasheria wa Kikosi cha Polisi cha Usalama barabarani, Mrakibu msaidizi wa polisi, Deus Sokoni anasema kuna udhaifu kwenye sheria za usalama barabarani kwani haimtaji mtoto katika suala la kuvaa helmeti pale anapopanda pikipiki.
"Tuna sheria ya usafirishaji ambayo inasema tu kwamba mtoto chini ya miaka tisa, apande pikipiki kwa usaidizi wa mtu mzima, lakini haimlazimishi mtoto kuvaa helmet," anasema. Anaongeza kuwa kutokana na hali hiyo ndio maana wanaandaa sheria mpya ya usalama barabarani.
Anasema tayari sheria hiyo imepelekwa kwa mwanasheria mkuu wa serikali na akiridhika ataipeleka bungeni ili iweze kupitishwa.
Alisema sheria mpya ya usalama barabarani, miongoni mwa mambo mengi inataka pia mtoto avae helmeti pale anaposafiri na pikipiki.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!